Mafisadi rudisheni pesa zetu???-

Mtade_Halisi

Member
Feb 23, 2008
28
0
Mfanyabiashara maarufu akabidhi mil 700/-
BAADHI ya waliochota mabilioni ya fedha serikalini chini ya mpango wa kuagiza bidhaa mbalimbali nje ya nchi yaani Commodity Import Support (CIS), wameanza kulipa madeni yao baada ya serikali kutishia kuanika majina yao.

Habari za uhakika kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi zilizoifikia HabariLeo zimethibitisha kuwa watu kadhaa ambao walichukua fedha za CIS lakini baadaye wakaacha kwa makusudi kulipa wamejisalimisha Hazina mara tu baada ya serikali kutishia kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuanika hadharani majina yao kama hawatalipa madeni yao ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

Miongoni mwa wadaiwa hao wamo wafanyabiashara maarufu nchini na wanasiasa.

HabariLeo imethibitishiwa na maofisa wa Hazina kwamba mara tu baada ya tangazo la kudaiwa kutoka magazetini, baadhi ya wadaiwa walijitokeza haraka na kusema sasa wako tayari kulipa.

“Kuna huyu tajiri (jina tunalo) ilipotangazwa tu akaja na hundi ya Sh milioni 700,” Ofisa mmoja wa Hazina alisema na kuongeza wengine kadhaa wenye viwango vya chini pia wamejitokeza.

Inaaminika kwamba baadhi ya wadaiwa walitumia kampuni bandia kujipatia fedha na kutoagiza bidhaa kama ilivyotarajiwa na serikali.

Kampuni 980 zilikopeshwa mabilioni hayo kuanzia miaka ya 1980 mpaka mwaka 1993. Fedha hizo zilitolewa na wahisani mbalimbali chini ya mpango huo ili kuipa uwezo serikali wa kuimarisha uchumi wake.

Miongoni wa nchi hizo ni Japan ambayo imekuwa inatoa misaada mingi kwa Tanzania.

Lengo la wahisani kutoa fedha hizo ilikuwa kuzipatia taasisi, kampuni, viwanda na biashara mbalimbali uwezo wa kuagiza bidhaa na mali ghafi kutoka nje kwa kuwa wakati huo nchi ilikuwa na upungufu mkubwa wa fedha za kigeni.

Hata hivyo wafanyabiashara wengi waliochukua fedha hizo ambazo zilitolewa kama mkopo wa masharti nafuu ambao hauna riba, lakini kinyume cha matarajio wafanyabiashara hao walishindwa kuagiza bidhaa yo yote kutoka nje kama ilivyokusudiwa na serikali badala yake wakazitumia fedha hizo kwa manufaa binafsi.

Kuanzia mwaka 2002 serkali ilikabidhi mpango huo wa fedha chini ya Benki ya Raslimali (TIB), lakini tangu wakati huo wadaiwa wameshindwa na wengine wamekataa kwa makusudi kulipa madeni hayo.

Mwaka huu benki hiyo ililazimika kupeleka wakusanya madeni mjini Dodoma kwa ajili ya kushauriana na baadhi ya wadaiwa walioko bungeni.

Kwa mujibu wa maofisa wa Hazina uchotwaji wa mabilioni hayo ya CIS ulikuwa ufisadi wa mwanzo wa aina yake kufanyika nchini na tangu wakati huo baadhi ya wafanyabiashara walijineemisha hali iliyowafanya waendelee kujichotea fedha zingine serikali kwa kutumia mianya mbalimbali na udhaifu wa watendaji.

Kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na serikali wakati huo, mkopaji akishindwa kulipa kwa kipindi cha miezi 18 tangu achukue mkopo alilazimika kulipa riba ya asilimia 17.

Fedha hizo zilizokuwa zinakusanywa kutokana na deni hilo zilikuwa zinachangia mapato ya Serikali pamoja na miradi maalum ya maendeleo baada ya makubaliano na wahisani husika.

Kwa mujibu wa tangazo la Serikali la kuwataka wakopaji warejeshe fedha hizo, wafanyabiashara wengi walikacha kurejesha licha ya Serikali kufuatilia.

Kwa sasa Serikali imewataka wadaiwa kuwasiliana na taasisi mbalimbali kama Mamlaka ya Mapato (TRA) na Benki ya raslimali (TIB) au Wizara ya Fedha na Uchumi kwa ajili ya kupata kumbukumbu ya madeni.
 
Back
Top Bottom