KWELI bado lipo tumaini. Hata kwa watu ambao walitarajia kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kingeweza kuvunjika vipande vipande na kila mtu kugawana mbao, inawapasa wavute pumzi kidogo na kuona kilichotokea na kukiri kuwa labda CHADEMA watasalimika. Kwamba kweli CHADEMA kitasalimika ni muda tu utaamua, lakini kwamba kimenusurika hadi hivi sasa licha ya mawimbi makali na pepo za msimu zinazopunga kila kona ni wazi kuwa CHADEMA kinapitia wakati wake mgumu kabisa wa mabadiliko na maisha yake, kuliko wakati mwingine wowote ule.
Ni katika kutafakari haya yote ambayo yametokea hadi hivi sasa naweza kusema kuwa yapo mambo mazuri, yapo mabaya, yapo ya kuudhi na mengine ya kuchekesha na kwa kweli yapo ya kusikitisha vile vile. Nina uhakika wasomaji wangu pia watakuwa wameona kwa upande wao mambo kama haya. Tutafanya makosa makubwa tukidhani tu kuwa kuna jambo moja zuri au moja baya au kuangalia kwa uamuzi wa rangi nyeupe na nyeusi tu, bila kuangalia labda kama kuna kijivu mahali fulani.
Mazuri katika sakata hili
Yapo mambo mazuri ambayo yametokea kutokana na sakata hili la CHADEMA. Kati ya mengi naweza kutaja machache tu. Kwanza, hatimaye lile joto lililokuwa limepanda kwa muda mrefu ndani ya chama hicho limepata mahala pa kutokea. Kwa muda mrefu kumekuwa na hali ya kutunishiana misuli, kuumana maneno na hata kutegeshana na kutegeana. Viongozi wa taifa wa chama walikuwa wanaonekana wamegawanyika, lakini kila mmoja akikana kuwa hakuna mgogoro ndani ya chama.
Ni kana kwamba walikuwa wameamua kuwa wote watakuwa mbuni vichwa mchangani lakini mwisho wa siku ilibidi kushughulikia kile ambacho kilikuwa kinasumbua chama. Kwamba chama kimeweza kukaa chini na kuwajadili na kuchukua hatua kali dhidi ya viongozi wake wa kitaifa ni jambo zuri. Ni jambo zuri kwa sababu moja kubwa, kwamba sasa wana CHADEMA na wapenda mabadiliko wote ni lazima waamini kuwa hakuna ‘superstar' ndani ya chama na yeyote ambaye ataleta matatizo atashughulikiwa. Kama wameweza kufanya hivi kwa Naibu Katibu Mkuu ni lazima wana CHADEMA wawe tayari kuamini kuwa maji yale yale yaliyotumika kumnyonyoa yeye yanaweza siku moja yakatumika kumng'oa Mwenyekiti, Katibu Mkuu au kiongozi mwingine yeyote. Huu ulikuwa ni mstari ambao ulisubiriwa kwa hamu, watu waone kama utavukwa.
Jambo jingine zuri ni kuwa viongozi waliovuliwa madaraka wangeweza kabisa kuja na hasira na kutoa kauli za kutotambua uamuzi wa kikao kile na kudai kuwa wao bado ni viongozi halali wa ngazi husika. Wangeamua kumwaga mboga na wao kwa vile wenzao wameshamwaga ugali! Hawakufanya hivyo na badala yake, walitoa kauli ambazo kwa kweli hazikuwa kali kama watu walivyotarajia kwani walichukua muda kupima na kutulia – ndio mwanzo wa hekima. Jambo hili ni zuri na ndio maana nimesema kwa hakika bado yapo matumaini. Utulivu huu walioonesha – japo sikupenda watoe matamko yoyote hadi watakapokuwa wamejibu maelekezo ya Kamati Kuu- umesaidia kwa kiasi kuonesha njia nzuri ya huko mbele. Jambo hili ni zuri.
Mabaya katika sakata hili
Kati ya mambo mabaya yaliyotokea katika sakata hili ni kwamba lilifikia hapa lilipofikia. Hadi hivi sasa sijaelewa – japo nimejitahidi sana kujielewesha – kwa nini suala hili limefikia hapo lilipofikia hadi kulazimisha kuchukua hatua kali zaidi? Hivi hakukuwa na njia nyingine ambayo ingeweza kutumika mapema zaidi kudhibiti kile kinachoitwa uasi au kama wengine wanavyoona harakati za kutaka mabadiliko ndani ya chama?
Kwamba inafikia mahali watu wanatofautiana kiasi cha kuwa na uhasama wa wazi, kurushiana vijembe vya maneno, kweli watu hao wanaweza kusema wanataka kuongoza harakati za mabadiliko? Kuna msemo kuwa ‘nyumba iliyogawanyika haiwezi kusimama'; msemo huu ni wa kweli kwa maana nyingi sana. Muda ambao ndugu wanaweza wakakaa kugombana wenyewe kwa wenyewe na kuumizana ndio muda ambao adui anaweza kutumia kuwanyang'anya mali, kuwaibia na hata kuwadhuru. Tumeona hili vizuri sana kwamba CCM wananufaika mno na mgawanyiko ulioko ndani ya CHADEMA kiasi kwamba hawaoni tatizo kabisa kuunga mkono upande mmoja wakiamini kwa kufanya hivyo wanaongeza mgogoro. Na baya zaidi ni kweli wapo wana CHADEMA ambao hawaoni tatizo kuungwa mkono na CCM kwa kisingizio kuwa wanapigania maslahi ya taifa!
Kitu pekee ambacho hutaona wanaCCM wanakifanya ni kuwakaribisha hao wana CHADEMA waingie CCM ambako watapewa nafasi ya kugombea uongozi wa chama kitaifa au kuwa nyota wao. Kwa sababu wakiingia huko na huko nako tayari kuna mastaa wao na wao wenyewe pia wana migogoro yao ambayo kwa sababu ya mgogoro wa CHADEMA hatuisikii sana; lakini ipo.
Haya ya CHADEMA hayakupaswa kufika hapa na kuachwa kufika hapa. Yangeweza kabisa kumalizwa kidugu, kirafiki na kiumoja siyo sasa hivi ambapo watu wengine hata hawasalimiani tena! Na wote wanadai wanataka kuing'oa CCM madarakani!
Ya Kuudhi katika sakata hili
Kati ya mambo yanayoudhi ni ule ushabiki uliopitiliza wa wafuasi wa makundi mbalimbali ndani ya CHADEMA. Kwa sisi wengine ambao tunasoma mitandao na kufuatilia mambo haya kwa karibu, kwa kweli inachukiza kuona jinsi watu wanaodai kuwa wako chama kimoja na tena ni viongozi wakiwa wametengeneza kambi ambazo zinachukiana kupita kiasi. Kinachoudhi ni kuwa kambi hizi zimetengenezwa na viongozi wanaopenda wafuasi! Matokeo yake wafuasi wanajibizana, wanatambiana na wanatishana hadi inakera na kuudhi kwa wakati mmoja. Inaudhi kwamba makundi haya ya mashabiki wa watu (kumbuka si mashabiki wa itikadi fulani) wamekuwa watii kwa watu hawa hadi wamekuwa kama kasuku wanaorudia maneno ya wanaowafundisha! Wengine wamefikia mahali hadi wanazungumza kama viongozi wao! Wengine wanaigiza hadi sauti za viongozi wao.
Cha kuudhi ni kuwa kati ya hawa wapo ambao utii wao uko si kwa sababu wanaamini itikadi au maono ya viongozi wao bali kwa sababu matumbo yao na mifuko yao yanawategemea watu hawa. Hivyo, wamekuwa watetezi wa kimaslahi zaidi, siku minofu hiyo ikikatwa watatafuta mahali pengine pa kuegemea. Hili linaudhi!
Ya Kusikitisha katika sakata hili
Jambo kubwa la kusitikisha kutokana na sakata hili ni kuwa CCM na serikali yake wanaendelea kutawala wapendavyo. Wakati CHADEMA wanafukuzana wenyewe, wanatafunana na kung'atana CCM wao wanaendelea kumkamua ng'ombe aitwaye ‘Mtanzania' kama wapendavyo. Tumesikia juzi kuwa serikali imekubali kupandisha bei ya umeme na wakati huo huo, tayari tumeona jinsi sera mbovu zilizoshindwa za CCM zilivyoharibu taifa. Kuanzia kwenye elimu, maji, ulinzi na usalama na kwingine kote sera za CCM zimekuwa na madhara makubwa zaidi kuliko kitu kingine chochote. Sera pekee ambayo inaonekana kufanikiwa ni ile ya ‘uwekezaji wa wageni'. Serikali imejitahidi kwa kila namna kuwavutia wawekezaji wa kigeni kiasi kwamba watendaji wake wanapokebehi wawekezaji wa ndani hakuna anayeshtuka; nani anawahitaji wa ndani kama wa nje wanaleta yote wanayohitaji.
Lakini hili pia tunaweza kuliona kama ni ubovu wa sera ya uwekezaji wa kigeni – kama sera yenyewe ipo kweli. Sasa wakati CCM inaweza kufanya lolote CHADEMA kama chama kikuu cha upinzani kinasubiri kikao cha Bunge ili waonekane wanapiga kelele, wagome na kutoa hotuba motomoto. Wanafanya hivyo huku wenyewe wakiwa hawapatani na mwisho inaonekana wanachozungumza kila mmoja ni maoni yake na siyo mkakati wa kichama (party strategy). Matokeo yake juhudi za wabunge mbalimbali wa upinzani zinaonekana kutukuza majina yao zaidi kuliko kukijenga chama. Imefikia mahali wao wenyewe tena hawapatani hadi bungeni! CCM wanagongagonga meza tu na kuitikia ndiyo!! Nani atawazuia! Nani ataonesha ubaya wa sera zao? Kweli kuna mpinzani anayeamini kuwa sera za CCM ni mbaya na ni janga kuu la taifa letu? Hili linasikitisha!
Ya kuchekesha katika sakata hili
Yapo pia mambo ya kuchekesha, kubwa zaidi ni lile linalotokana na hayo yote hapo juu. CHADEMA inaamini kuwa inaweza kuvuruga kwa kiasi chochote kile na watu bado wataendelea kusimama nyuma yake na kusema "people's power". Hisia hizi zinatokana na kupendwa. Wakati mwingine mtu anayependwa anaweza kabisa asijue kabisa ameharibu kwa kadiri ya kwamba watu wanaendelea kumpamba kwa maneno mazuri na kumfanya ajione ni muhimu. Mtu wa namna hiyo anaweza kuchelewa sana kujijua kuwa kaharibu na hata siku akija kujua kuwa ameharibu, atakuwa amekwishachelewa sana.
Tatizo la mtu wa namna hiyo ni kiburi cha kupendwa. Kuna msemo kuwa mtu anayependa ‘haoni wala hasikii'; hili ni kweli pia kwa mtu anayependwa hasa akijua anapendwa na mtu ambaye katika mazingira mengine asingeweza kupendwa. Mtu huyu anayependwa siku atakapokuja achwa hawezi kuamini; na anaweza kuumia kweli kweli na hata kuwa mtu wa kisasi. Kwa sababu hakuwahi kuamini mtu aliyemuonesha mapenzi namna hiyo kweli anaweza kumuacha solemba.
CHADEMA isipoangalia itajikuta iko katika hali ya namna hii – kama haiko tayari – kwamba kwa vile inajua inapendwa na watu wengi basi viongozi wake hawaamini kuwa wana matatizo ndani yao au katika uongozi wao. Binafsi naamini tuliyoyashuhudia siku hizi chache zilizopita ni kilele cha ulevi huu wa mapenzi; wahusika wote wanaamini wanapendwa! Wote wamezungukwa na watu wanaowaimbia nyimbo za kuwapenda na kuwafanya wajisikie ‘spesho'! Kwa baadhi yetu tuliosoma Saikolojia watu wa namna hii ni vigumu sana kujiangalia na kubadili tabia kwa sababu wakibadili tabia na watu wakaacha kuwapenda itakuwaje? Kwa kadiri ndugu zetu hawa wataendelea kuzama katika hizi hisia za kupendwa ndivyo itakavyokuwa vigumu zaidi kwa wao kujipima na kubadili tabia, mitazamo na matendo yao. Kwa nini wabadili wakati wao wanapendwa? Hili linachekesha. Ama linatisha.
Source: Raia mwema