TataMadiba
JF-Expert Member
- Feb 7, 2014
- 9,866
- 5,742
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed amemtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoa taarifa za kuwapo kwa tishio la kundi la al Qaeda kuingia nchini kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili vyombo hivyo, vishughulikie hatari hiyo.
Aboud amesema kwa kuwa Lowassa anaelewa madhara ya ugaidi na ana taarifa za kina kuhusu kundi hilo, ni vyema akazipeleka kwenye vyombo vya usalama.
“Kuna nchi za jirani ambazo zimekumbwa na madhara ya ugaidi, sasa kama kuna watu kama akina Lowassa na wengine wenye maono kama hayo au kuwa na taarifa za ziada za magaidi basi wapeleke Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi,” alisema Aboud
Mwishoni mwa wiki, Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, alionya kuwa ipo hatari Zanzibar ikatumiwa kuwa njia ya kuingia magaidi wa aina ya Al-Qaeda nchini.
Lowassa alidai kuwa hilo linaweza kufanyika, endapo jitihada maalumu hazitafanyika sasa katika kumaliza mkwamo wa kisiasa visiwani humo na kuzuia uwezekano wa kuvunjika kwa hali ya amani.
Lakini, Waziri Aboud aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisisitiza kuwa Zanzibar ina amani na utulivu na kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imejipanga kuhakikisha hali ya utulivu na amani inaendelea kudumu.
“Kama serikali kupitia vyombo vyake vya usalama, vina utaratibu wake wa kuhakikisha inashughulikia watu wote wanaofanya uhalifu na vitendo vya uvunjifu wa amani kwa mujibu wa taratibu za nchi,” alieleza.
Alisema SMZ itahakikisha inatekeleza agizo la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) la kufanyia uchaguzi wa marudio na kuwapo kwa vitisho kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani.
“Tutatekeleza agizo la Tume ya Uchaguzi (ZEC) na niwahakikishie wananchi kuwa Zanzibar itaendelea kuwa na amani na utulivu kuanzia sasa, wakati wa kupiga kura na baada ya kupiga kura na kupokea matokeo,” alibainisha.
Zanzibar inatarajia kufanya uchaguzi wa marudio wa kuchagua Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani Machi 20, mwaka huu, baada ya ule uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa siku tatu baadaye kwa tangazo la Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kutokana na kuwapo kwa kasoro kadhaa.