London: Watano wafariki shambulio la kigaidi Westminister

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,410
Watu watano wamethibitishwa kufariki dunia na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa baada ya mshambuliaji kuvurumisha gari na kuwagonga watu katika daraja la Westminister jijini London.

Mshambuliaji huyo kisha alimdunga kisu afisa wa polisi lakini baadaye akauawa kwa kupigwa risasi na polisi katika maeneo ya Bunge.

Afisa wa polisi aliyeuawa ametambuliwa kama Keith Palmer, 48.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema shambulio hilo lilikuwa "la ukosefu wa maadili" na lilishambulia maadili makuu ya uhuru wa kufanya maamuzi, demokrasia na uhuru wa kujieleza.

Polisi hawajafichia jina wala maelezo zaidi kumhusu mshambuliaji.

Kaimu naibu kamishna wa polisi ambaye anasimamia kitengo cha kukabiliana na ugaidi katika Polisi wa Jiji Kuu, Mark Rowley, amesema anafikiria wanamfahamu mshambuliaji na kwamba huenda alihamasishwa na makundi ya kigaidi ya kimataifa yenye uhusiano na itikadi kali za Kiislamu.

Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.

Shambulio hilo lilitokea mwendo wa saa 14.40 GMT pale mshambuliaji mmoja aliyekuwa na gari la rangi ya kijivu aina ya Hyundai i40 alipolivurumisha gari hadi eneo la kutumiwa na wanaotembea kwa miguu kwenye Daraja la West Minister, karibu na Majengo ya Bunge.

Aliwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine wengi.

Baadaye aligongesha gari lake kwenye uzio nje ya Majengo ya Bunge.

Baadaye, mshambuliaji huyo alikimbia, akiwa na kisu, hadi kwenye Bunge ambapo alikabiliwa na polisi.

Afisa wa polisi Palmer, ambaye hakuwa na silaha, alidungwa kisu na mshambuliaji huyo. Alifariki baadaye.

Mshambuliaji alipigwa risasi na kuuawa na polisi waliokuwa na silaha hapo karibu.

Bw Rowley ametoa heshima zake kwa Palmer, na kusema: "Ni mtu aliyetoka kwake nyumbani leo kwenda kazini akitarajia kurejea nyumbani baada ya kumaliza zamu yake, na alikuwa na kila haki kutarajia kwamba hilo lingefanyika."

Waziri wa mambo ya nje Tobias Ellwood, mwanajeshi wa zamani ambaye kakake aliuawa katika shambulio la kigaidi la Bali mwaka 2002, alijaribu kumpa Palmer huduma ya kwanza.

Mwanamke mmoja alifariki baada ya kugongwa na gari la mshambuliaji huyo kabla ya gari hilo kufika eneo la majengo ya Bunge.

Alithibitishwa kufariki na daktari katika hospitali ya St Thomas'.

Bi May alishutumu shambulio hilo na kusema juhudi kama hizo za kuvuruga maadili ya Uingereza hazitafanikiwa.

Aliwashukuru maafisa wa polisi waliofika eneo hilo baada ya tukio na kusema: "Sote tutasonga mbele pamoja, hatutayumbishwa na ugaidi na hatutakubali chuki na uovu kututenganishwa."

Waziri huyo mkuu aliongeza: "Haikuwa ajali kwamba shambulio hili lilitekelezwa eneo hili.

"Gaidi huyu aliamua kushambulia katikati mwa jiji kuu ambapo watu wa mataifa yote, dini zote na tamaduni zote hukusanyika kusherehekea maadili ya uhuru wa maamuzi, demokrasia na uhuru wa kujieleza."

Bi May anatarajiwa kutoa hotuba baadaye leo katika Bunge la Commons.

Chanzo: BBC/Swahili
 
Back
Top Bottom