LATRA: Treni za Mwakyembe hazikidhi viwango vya kutoa huduma ya usafiri licha ya kuzidiwa na wingi wa abiria

ChoiceVariable

JF-Expert Member
May 23, 2017
43,042
49,727
Kwa hiyo Latra wanataka wasemaje? Aliyewaelewa atufafanulie.

Swali:
Serikali inasubiria nini Kuwekeza kwenye usafiri wa Treni Mjini ikiwa abiria wapo wa kutosha miaka 10 Sasa?

========

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miaka 10 tangu treni za usafirishaji wa abiria jijini hapa maarufu kwa jina la ‘treni za Mwakyembe’ kufanya kazi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (Latra) imesema usafiri huo haujakidhi viwango vya usafiri mijini.

Hali hiyo inakuja wakati treni hizo zikizidiwa na wingi wa abiria wanaoelekea maeneo ya Gongolamboto na Pugu, kutokana na mvua zilizoanza kunyesha, huku pia barabara ya Nyerere inayofanyiwa matengenezo ikiwa na msongamano mkubwa wa magari.

Mwananchi limeshuhudia kwa nyakati tofauti, abiria wakiwa wamejazana kwenye mabehewa ya treni hizo, huku wengine wakining’inia kwenye milango na madirisha, ilimradi wafikishwe wanakokwenda.

Treni za Mwakyembe zilianzishwa Oktoba 2012 na Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliyetaka Shirika la Reli (TRC) na Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), kuanzisha usafiri wa treni ili kupunguza msongamano wa abiria katika vituo vya daladala.

“Unajua wakati ule Serikali ilikusudia kwamba hata kama treni hazijaandaliwa kwa ajili ya safari za mjini, basi zifanye kazi kidogo kuongezea usafiri uliopo wa mabasi na barabara.

“Lakini matokeo yamekuwa makubwa kwa sababu watu wameshazoea kutumia treni pale barabara zinapokuwa na msongamano,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri wa Reli wa Latra, Hanya Mbawala alipozungumza na Mwananchi juzi.

Alisema wamekuwa wakiishauri Serikali kutafuta mabehewa kwa ajili ya usafiri wa mijini kwa kuwa yaliyopo ni kwa ajili ya usafiri wa masafa marefu.

“Hiyo tulishabainisha kwenye ripoti zetu na sisi uzuri tunaripoti kwenye Serikali tunaiambia,” alisema.

Hanya alisema licha ya Serikali kuwa na mikakati ya uboreshaji wa reli ya kisasa (SGR) na uboreshaji wa reli ya Meter Gauge (reli ya kati), mpango wa kuboresha treni za Mwakyembe kwa sasa haupo.

“Magari ya SGR ni ya masafa marefu, yaani Dar es Salaam Morogoro. Kituo cha kwanza ni Soga, halafu Ruvu, Ngerengere kisha Morogoro.

“Kwa Dar es Salaam – Pugu na Ubungo, hakuna mpango wowote mpaka sasa. Hilo ni suala la kisera zaidi, sio la usimamizi.

“Sisi tulishawaambia kwamba kwa usafiri wa mijini kuna mabehewa ya kutumia. Kwa sababu sasa hivi wimbo ni SGR,” alisema.

Alisema hata pamoja na Benki ya Dunia kufadhili uboreshaji wa reli hiyo, pia haina kipengele cha usafiri wa mijini.

Adha ya mvua
Akizungumzia msongamano wa abiria wakati huu wa mvua, Mbawala alisema ni vigumu kuzuia abiria kujazana kwenye mabehewa.

Alisema kabla mvua hazijaanza walijisahau, hivyo wanawakumbusha TRC na Tazara wajiandae na wimbi kubwa la watu kutokana na ujenzi unaoendelea wa njia za mwendo wa haraka kuelekea Gongolamboto.

“Bado tunafikiria namna nzuri zaidi, lakini tumesema angalau milango ifungwe. Behewa moja linaweza kubeba kati ya watu 90 mpaka 150, huo ndio uwezo wake, lakini nani anadhibiti idadi hiyo inakuwa ni ngumu kwa sababu kwanza hatuna utaratibu wa mashine wa kudhibiti idadi.

“Kwa hiyo tumekumbushana na wenzetu wa TRC kwamba tujitahidi, kwa sababu mabehewa yenyewe hayajaandaliwa kuwa ya usafiri wa mijini, bali safari ambayo unakaa kwenye siti, sasa wao wameacha siti ziko vilevile, kwa hiyo abiria wanaosimama ni wachache kuliko wanaokaa na inapotokea ajali itakuwa ngumu kuwaokoa kwa sababu hakuna njia za kutokea,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanazo taarifa kuwa TRC wameongeza idadi ya mabehewa na usimamizi zaidi na kuhakikisha kila behewa lina askari Polisi.

Juhudi za kumpata Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TRC, Jamila Mbarouk kufafanua hali ya usafiri huo, hazikufanikiwa, kwani tangu juzi alipopigiwa simu alisema hawezi kujibu kwa kuwa yuko kwenye kikao.

Jana alipotafutwa kwa simu alimtaka mwandishi amtumie maswali kwa simu na hata alipotumiwa hakuyajibu.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa simu yake haikuwa hewani, hata Naibu Waziri wake, David Kihenzile naye hakupatikana.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Godious Kahyarara, alipotafutwa hakuwa tayari kuzungumzia hilo, kwa kile alichoeleza alikuwa kikaoni.

"Nipo katikati ya kikao kuhusu migogoro ya mipaka, kwa hiyo sitaweza kuzungumzia lolote. Naomba nikirudi tuwasiliane tutazungumza kwa kina," alisema.

Tazara walia ukata
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Uhusiano na Umma wa Tazara, Conrad Simuchile juzi Novemba 6 ilikiri kuwepo kwa hali mbaya ya usafiri wa treni ya abiria kati ya Tazara na Pugu.

“Tanzania-Zambia Railway Authority (Tazara) inasikitika kukwama kwa usafiri kwa treni ya abiria ya Dar es Salaam hivi karibuni nyakati za asubuhi.

“Kukwama huko ni ishara ya changamoto inazokabiliana nazo Tazara, tunafanya kazi tukiwa na mtaji mdogo kiasi cha kushindwa kuwekeza kwenye treni za kisasa au hata kuboresha treni zilizopo.

“Matokeo yake ndio hali iliyopo ambapo treni zilizopo hazina uhakika kama ambavyo tungependa, hali inayosababisha kukwama kama huko,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, Simuchile alisema katika taarifa hiyo kuwa kuna mpango ulioandaliwa kuifufua Tazara, ambapo mawaziri wa pande mbili wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Hakainde Hichilema wa Zambia wamepanga kuhusisha wawekezaji kutoka China kupitia makubaliano ya kibiashara.

“Makubaliano hayo ya kibiashara yamepangwa kuanza Novemba, 2023. Tuna uhakika kwamba juhudi za pamoja kati ya Serikali za Tanzania na Zambia, kwa kushirikiana na wawekezaji wa uhakika na wadau zitafufua na kuikuza Tazara na kutuwezesha kumudu ongezeko la mahitaji kwa abiria na mizigo katika eneo hilo,” alisema.

Chalamila aingilia kati
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema changamoto za usafiri wa treni katika kipindi hiki cha mvua kubwa imeleta adha kwa wakazi wa Chanika, Gongolamboto, Kivule, Mwanagati na Kitunda na ndiyo maeneo ambayo wanapendelea sana kutumia usafiri wa treni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kufungua kongamano la kimataifa linalohusu utumwa mamboleo katika historia ya Afrika ya sasa uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema wanafanya taratibu za kupangilia kikamilifu ratiba za treni hiyo pamoja na kuongeza mabehewa na kuweka utaratibu wa kutenganisha wazee na wagonjwa.

"Pia tunafanya jitihada za kuhakikisha reli ina uwezo wa kupitika muda wote na kuwa usafiri wa uhakika zaidi," alisema.

Mbali na treni, Chalamila alisema katika usafiri wa mabasi yaendayo haraka, hadi sasa mabasi zaidi ya 30 tayari yameshakarabatiwa miongoni mwa mabasi 70 aliyoagiza yarekebishwe alipotembelea kituo cha mabasi hayo cha Kimara Oktoba 12, 2023.

CHANZO: Mwananchi
 
Mwendokasi washafanya lobbying, wanajua wakianza na daladala zikaondoka, abiria watakomaa na hiyo treni kutokana na huduma mbovu za mwendokasi na gharama za kufika mjini zitapanda maradufu kuokana na kuunganisha mabasi.
 
Hivi serikali ya CCM nje ya siasa za majungu na fitina, kuna jambo lingine mnalifanya kwa umakini na mafanikio makubwa kweli? Yaani miaka nenda, kila sekta ni madudu tu.
 
Nchi ya ajabu sana hii, badala ya kuitumia treni hiyo kama pilot project inayowapa majibu ya kuwepo mahitaji makubwa kwa huo usafiri jijini, wao wapo kupiga siasa.

Heri hizo njia za mwendokasi kutumika kama miundombinu ya usafiri wa treni kuliko hayo mabasi.
 
Back
Top Bottom