Kwanini mkeo amekimbia.

Kwanini mkeo amekimbia.

tofyo

JF-Expert Member
Joined
Jul 18, 2013
Posts
2,759
Reaction score
768
@Abdulqadir Shareef, mwanazuoni mtaalamu wa Sharia PhD holder katika elimu ya dini ya kiislam.anafanya shughuli zake chuo kimoja huko Wingereza.

chukua hii Kwa faida.

Nimeulizwa pembeni, NANUKUU:-

*Nini hukumu ya mwanamke aliyemtoroka mumewe na kukimbilia kwao kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu? Je, bado anahesabika kuwa ni mke au ameachika? Naomba ufafafnuzi!*

JIBU

BISMILLAH

Suala lako haliwezi kujibiwa moja kwa moja, maana ulicho eleza ni madai yako tu, dhidi yake; hujaeleza ameondoka kwa sababu gani, wala sisi hatujamsikia yeye madai yake dhidi yako. Migogoro ya wanandoa haiwezi kutatuliwa kuwa kusikiliza hoja au madai ya upande mmoja tu. Lazima tusikia hoja na madai ya kila upande dhidi ya upande wa pili. Maana yawezekana kuweko sababu mbali mbali zilizo mfanya aondoke kwenye nyumba ya ndoa; miongoni mwake ni kutoweza kuvumilia udhalimu, unyanyaso, maonevu, uhesharati, kunyimwa haki zake, ect., ect. Hivyo, haitawezekana kukupa jibu la moja kwa moja, kutegemea madai yako tu.

Baada ya kusema hayo, sasa nijaribu kutoa darsa, ya jumla, kuhusu migogoro ya wanandoa na nini kinatakikana kufanywa, inapo tokea hali ya kutoelewana baina ya wanandoa, wenyewe kwa wenyewe, na wakashindwa wao wenyewe kutanzua kutoelewana kwao.
Kwanza kabisa inapaswa kutambua kuwa kuishi pamoja watu wawili hakuwezi kusalimika na vijimakosa baina yao; maana wao ni wanadamu, SI malaika. Kila mwanadamu hasalimiki na kukosea; ila mbora wa kukosea ni yule mwenye kupenda sana kutubu:
عن أنس بن مالك رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال : ( كل بني آدم خطاء وخير الخطائين التوابون ) رواه الترمذي (2499)
Imepokewa kutoka kwa Anas bin Malik رضي الله عنه akisema: "Amesema Mtume ﷺ : "Wanadamu wote ni wanakosea kosea, na mbora wa wenye kukosea kosea ni wenye kupenda kutubu (kuomba msamaha)" Ameipokea Tirmidhi, H. 2499.

Hivyo, kukoseana mume na mke ni jambo lisilo weza kuiepukika; ni jambo la kawaida. Na njia pekee na ya haraka ya kundoa suitafahum kama hizo, ni mmoja kuregeza kamba na SI kung'ang'ania kuivuta upande wake. *ITAKATIKA, na kamba hukatikia palipo pabovu!* Na njia rahisi na ya mkato ni kuambiana "basi yaishe, kama unaona kuwa mimi ndiye niliye kosa basi nisamehe, na kama wewe ndiye uliye kosa basi na mimi nakusamehe." Venginenvyo ni kunyamaziana na kuvumiliana. Kufanya hivyo, kunapunguza hasira na kila mmoja kurudi kujitathmini upya.

Kuendelea kuvutana, kwa sababu ya jambo dogo tu, kunaweza kupelekea mahali pabaya, hata kufufua mengine ambayo yalikwisha pita au hayakuwa yanajulikana baina yao.
Na sababu nyingi za magomvi ya wanandoa ni ukosefu wa kujuwa haki za kila mmoja juu ya mwenziwe; khasa mume. Wanaume wengi huamini kuwa mke ni sawa na mtumishi au muajiriwa, anaye weza kumuamrisha lolote alitakalo, na kumtuma kama punda. Siyo kweli. Mke ni mwenza wa maisha halali ya ndoa, na ni upande wa pili wa mume: Kila upande una haki zake na wajibu juu yake kwa mwenziwe. Uwislamu umebainisha wazi haki hizo, tokea haki na majukumu ya mke kwa mume, hadi haki na majukumu ya mume kwa mke.
قال تعالى : ( وَلَهُنَّ مِثْلُ الَّذِي عَلَيْهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ ) البقرة/228
"Na wanawake wanao haki katika Sharia (kutoka kwa waume zao) kama ile haki iliyo juu yao (kwa waume zao). Na wanaume wana darja zaidi kuliko wao..." (Al-Baqara, 2:228)
Daraja zaidi, imefasiriwa na wanazuoni kuwa ni majukumu ya kumtunza mke kwa hali na mali; chakula, makaazi na mavazi, na kumlinda kwa kila njia halali. Na hii ndiyo maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu:
الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ(ألنساء، 4 :34 )
"Wanaume ni WASIMAMIZI wa wanawake, kwa kufadhiliwa na Mwenyezi Mungu baadhiyao juu ya baadhi, na kwa mali yao wanayo itoa..." (Ab-Nisa', 4:34)

قال ابن عباس رضي الله عنهما في الآية : أي : " لهن من حسن الصحبة والعشرة بالمعروف على أزواجهن مثل الذي عليهن من الطاعة فيما أوجبه عليهن لأزواجهن " ، وذكر القرطبي : أن الآية تعم جميع حقوق الزوجية
Amesema Ibn 'Abbas kuhusu Aya ya 228: "Na wanawake wana haki, juu ya waume zao, ya kuishi nao kwa usuhuba na upendo mwema na kwa maingilano ya maelewano mazuri ya kawaida, sawa sawa na haki za waume zao juu yao za kuwa watiifu kwa yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyawajibisha juu yao kwa waume zao." Na Imam Al-Qurtubi, amesema kuwa "Aya hii inakusanya haki zote za uwanandoa kwa kila mwanandoa."

Hivyo, aya hizo mbili zimefafanua wazi wazi kuwa kila mmoja ana haki kutimizwa na mwenziwe, na kila mmoja ana wajibu wa kutimiza haki kama hizo kwa mwenziwe; ili kwayo papatikane ulinganifu, usawa na uwiano wa haki na majukumu juu ya kila mmoja kwa mwenziwe. Unapo vurugwa uwiano huo na mwanandoa mmoja dhidi ya mwenziwe ndipo panapo anza kuzuka migogoro na magomvi, ambayo yasipo sawazishwa kwa haraka na yakawa yanapuuzwa na hivyo kulimbikika siku baada ya siku, ndipo inapo ishia kutoweza kuvumiliana.
Kwa upande wa mwanamume ni rahisi kwake kuvunja ndoa kwa kutoa talaka. Kwa upande wa mke, hata hivyo, si rahisi kuvunja ndoa kwa kutamka talaka. Kujivua kwake uwanandoa kunahitajia utaratibu maalumu unao itwa: خلع ambao nimeuelezea kwa kirefu mahali pengine. Kwa ufupi, ni utaratibu wa kudai talaka kupitia mahakama ya Qadhi, endapo hakuna matumaini ya kuelewana, kutokana na sababu halali za kisheria, na khasa ikiwa yeye ndiye mkoswa kwa kutotimiziwa haki zake, au kwa kuteswa na kunyanyaswa.

Hivyo, ni wajibu juu ya kila mwanandoa kuwa, siyo tu MUADILIFU, bali pia mvumilivu, mstahamilivu wa makosa madogo madogo ya mwenziwe, na kuwa mwepesi wa kusamehe ili kuzima moto unaotaka kuwashwa na Sheytani, baina yao. Hakuna kitu anacho kipenda sana Sheytani kama kuwagombanisha wanandoa wawili, wenyewe kwa wenyewe. Hivyo, asisaidiwe!

Na ni vibaya sana kwa mwanamume kumbughudhi, kumsimbulia, kumnyanyasa au kumdharau mkewe, kwa sababu ya jambo fulani dogo, au tabia fulani ndogo. Mtume ﷺ amesema:
( لَا يَفْرَكْ – أي : لا يبغض - مُؤْمِنٌ مُؤْمِنَةً ، إِنْ كَرِهَ مِنْهَا خُلُقًا رَضِيَ مِنْهَا آخَرَ ) رواه مسلم ،1469
"Asimbughudhi muumini wa kiume muumini wa kike; ikitokea akachukizwa na tabia yake moja kutoka kwake anaweza kuridhiwa tabia hiyo na mtu mwenine." Ameipokea Muslim, H. 1469.

Yaani kama mtu hawezi kuivumilia tabia fulani ya mkewe, basi ajuwe kuwa anaweza kuwepo mtu mwengine ambaye ataridhika nayo. Au akiwa hapendezwi na tabia moja, basi kutakuwepo tabia nyengine atayo pendezwa kutoka kwake. Ilimradi asichukulia tabia moja kuwa ndio sababu ya kumbughudhi, kumnyanyasa na kumuonea. Na hakuna jambo kubwa linalo weza kusaidia kujenga na kuimarisha nyumba ya ndoa, baina ya mume na mke, kama kujipamba kwa tabia nzuri: حسن الخلق . Ndiyo maana Mtume ﷺ akasema:
( أكمل المؤمنين إيماناً أحسنهم خلقاً وخياركم خياركم لنسائهم ) رواه الترمذي (1162) عن أبى هريرة
"Mkamilifu bora wa Imani, miongoni mwa Waumini, ni yule mwenye tabia nzuri! Na mbora wa wabora wa wenye tabia nzuri ni yule aliye mwema zaidi kwa wakeze!" Ameipokea Tirmidhi, kupitia kwa Abu Hurayra رضي الله عنه .

Riwaya nyengine inamalizia kwa kusema:
خيركم خيركم لأهله، وأنا خيركم لأهلي (رواه أبو داؤد)
"Mbora wengu ni yule aliye mbora kwa aila yake. Na mimi ndiye mbora wenu kwa aila yangu." Amiipokea Abu Daud.

Na maana ya حسن المعاشرة = yaani maingilano ya maelewano mazuri ya kawaida, ni kufumbia macho na kutofuatilia mambo madogo madogo, na kuacha hulka ya kukemea na kukaripia kila jambo, dogo au kubwa; isipo kuwa inapo vunjwa haki ya Mwenyezi Mungu. Kufanya hivyo, kwa kila dogo na kubwa ni sawa na kujidai utakatifu! Hakuna kiumbe mtakatifu!

Hivyo, suala lako la kusema: *Nini hukumu ya mwanamke aliyemtoroka mumewe na kukimbilia kwao kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu? Je, bado anahesabika kuwa ni mke au ameachika? Naomba ufafafnuzi!*, haliwezi kujibiwa pasi na kupata maelezo kutoka kwa huyo unaye dai kuwa amekukimbia. Lazima ijulikane amekukimbia kwa sababu gani? Lazima asikike yeye mwenyewe sababu yake ya kukimbia nyumba ya ndoa. Pamefanyika nini, kutoka upande wako kujaribu kusawazisha sababu hiyo? Umefanya nini kumfuatilia, moja kwa moja, au kupitia kwa wazee na ndugu zake, bali hata kupitia waja wema? Na vyovyote iwavyo, "kukimbia" huko hakuwezi kuwa ndio talaka. Hilo ndio jibu, pekee, unaloweza kupewa, kwa hivi sasa, kutokana na suala lako, dhidi ya mke wako.

والله أعلم
وبالله التوفيق
السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم‎ ‎
Imejibiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef
I RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza chochote, bali kuiweka –kama ilivyo- kwenye FB yako au kwenye ‎WhatsApp au kwenye Kumbi za Mitandao ya Jamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kuelimisha na kusambaza Dini. ‎Changia kusambaza Ilimu ya Dini, ili mchango wako uwe Sadaka yako Endelevu: صدقة جارية.‎
kcwajawema@gmail.com

.
 
Back
Top Bottom