Kwa watanzania wapenda michezo, my condolences..

Apr 5, 2017
8
15
Salaam wana JF

Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na gumzo kubwa juu ya ‘pointi 3’ za Simba Sports Club alizopewa baada ya kushinda malalamiko (na sio rufaa kama inavyopotoshwa) dhidi ya Kagera Sugar baada ya kumchezesha bwana Fakh anayedaiwa kuwa na kadi tatu za njano.

Awali ilielezwa kwamba kadi hiyo ya tatu ilipatikana katika mchezo wa FA na sio Ligi kuu, pia uongozi wa Kagera walikataa katakata kufanya makosa ya kizembe kama hayo, lakini kamati ya Protea baada ya kujiridhisha wakawapa alama 3 Simba Sports Club. Hatua hiyo ilipingwa vikali na Kagera Sugar kwa kutaka kesi hiyo irejewe upya kwani wanaamini walionewa.

Sasa hebu tuliache hili la nani ana haki na nani hana, halina maana kwetu na ni upotevu wa muda kulijadili. Tuijadili Simba na TFF kwa mapana yao.

A: SIMBA SPORTS CLUB (SSC)

Hawa walishinda lalamiko lao la awali na kamati ya Protea ikawapa alama 3, Simba walishinda kwa kupeleka vielelezo tena nasikia mpaka binaadamu walihojiwa ikiwa wanakumbuka kilichotokea katika michezo ya ligi kuu. Maamuzi yalisuasua lakini yalitoka na Kagera wakawa wamepoeza mchezo ule walioshinda katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Simba wakaibuka washindi katika Meza za Protea.

Baada ya TFF kupitia Bodi ya Ligi kupokea rufaa ya Kagera, wakaahidi kulifanyia kazi na kuhakikisha suala hili linapatiwa uamuzi wa haki kwa kurejea vithibitisho vyote vilivyowasilishwa katika kamati ya Protea na kuangalia ikiwa kuna namna yeyote haki ilipindishwa… EEeee bwana eee hao Simba kusikia hivyo hilo povu lao utasema wameambiwa wawasilishe ripoti ya hesabu za mapato na matumizi.

Simba SC wanaogopa nini? Ikiwa kamati ya Protea ilitenda haki kuwapa ushindi kwanini waogope TFF kupitia upya kesi hiyo? Hawana Imani na nani? Au wanaogopa kugundulika kwa kitu gani? Kwanini povu limewatoka kabla ya TFF kuamua?? Kuna kitu wameona kimebumbuluka na kitawaumbua? Wanakosa vipi imani na kwa baba ikiwa walimwamini mtoto? Je, walidanganyia pipi kwa mtoto ambayo kwa baba haitafaa au baba hadanganyiki?

Msemaji wa Klabu ya Simba Ndg. Haji Manara aliongea masuala mengi sana na hata akavuka mstari, akatuambia TFF “wamejazana wahaya” eti ndio sababu ya kutaka kuwapa haki Kagera, kwani Manara anajua uamuzi utakuwaje kabla hata haujamuuliwa? Nini kinampa uhakika huo? Je, ni uhaya wa viongozi wa TFF au sarakasi za Simba zinakwenda kuwaumbua? Je, ni Uyanga wa viongozi wa TFF ndio unaifanya Simba isiwe bingwa wa soka Tanzania?

Kwahiyo Simba wanataka kutuaminisha kwamba labda tukipata viongozi wasio na makabila na wasiotoka mkoa wowote ule ndio watakuwa mabingwa? Au Wao wana orodha ya makabila bora yatakayowapa ubingwa?

Kwanini Manara hakuzungumzia Usimba uliojaa Bodi ya Ligi na kwenye Kamati ya Protea? Yanga mara ngapi wananyongwa na Kamati hii na hatusikii Klabu ikija hadharani na kusema kuna Usimba katika Kamati? Ni mara ngapi pia Simba imenufaika na Usimba wa kamati hii lakini watu wamechuna tu? Leo hata kabla ya maamuzi kufanyika tayari Simba wanaanza kutetemeka, wanaogopa nini? Siamini kama kuna watu walio na sifa za uongozi kwa wakati huu ambao si aidha Simba au Yanga, hivyo ni ujinga mkubwa kuweka suala hili mbele, lakini ni pia ni upumbavu kuhusisha ukabila na uweledi, tena wakati ambao wewe ni mshukiwa.

Simba wangekataa haya masuala ya “Uhaya” na “Uyanga” tangu yalipoanza, yaani wakati Mwesigwa anakuwa Katibu mkuu wakati Rais ni Malinzi basi wangetwambia kwamba hawa watu ni Wahaya na pia ni wana Yanga kwahiyo hawana Sifa za kuongoza TFF, tungewaelewa. Lakini kutueleza hivyo muda huu ambao wanataka kwenda kufanya maamuzi juu ya kesi ya Simba ni kutaka kuwagombanisha na wananchi, yaani tuone kwamba Kagera wamerudishiwa pointi zao kwa kuwa viongozi wa TFF ni wahaya na Simba watapokonywa hizo pointi kwa kuwa viongozi wa TFF ni wana Yanga, hapa mnailazimisha TFF hata kama itabaini ukweli isiutoe kwa hofu hii mnayoitengeneza.

Haya, hilo la Manara achana nalo maana tayari anaelekea kufungiwa, na ninasema afungiwe tu na ikiwezekana Simba iadhibiwe ikiwa itaonekana wamekosea katika matamshi yao mbele ya vyombo vya habari.

Sasa kuna suala la maandamano, tena hili bwana linaratibiwa na Rais wa Simba mwenyewe Bw. Evance Aveva kwa nguvu zote tena barua nzito yenye wino mwekundu, mweupe na mweusi, si mchezo mwanangu mwenyewe.

Bado sijajua walitaka maandamano yaenda kulalamikia kitu gani cha maana specifically ila wao ndio walikaa na wakasema wataandamana lakini tena wamesema hawataandamana.

Rais Aveva akiwa Mwanza (kule alipodondoka na kupoteza fahamu baada ya Mzamiru kutia kambani goli la tatu) alionekana kukataa suala hili la kudai pointi za mezani, Aveva alijua kufanya hivyo ni kujiaibisha tu na kujichora kwani ni jambo ambalo halipo.

Lakini Geofrey Nyange “Kaburu” akasema aachiwe yeye show nzima na ataicheza na pointi zitapatikana. Nyange alikuwa Kanda ya ziwa pamoja na Aveva, lakini mchezo wa Simba na Toto Africans Kaburu nadhani hakuwepo, tayari alikuwa amekwenda Dar kusimamia zoezi la upatikanaji wa alama tatu ambazo Aveva alisema haziwezekani. Kweli bwana, Kamati ya Protea ikakaa na kuanza kusuka mipango ya ushindi wa Simba.

Alichosahau Aveva ni kwamba unapokuwa na kiongozi kama Kaburu hutakiwi kuwa na presha juu ya masuala madogo-madogo kama pointi za mezani, kufutwa kwa adhabu, kuchagua mechi za kucheza unapokuwa na kadi nyekundu, kutupiliwa mbali kwa rufaa zinazowahusu, na mambo mengine kama hayo, ni kiongozi anayeweza kubadili Asali kuwa Mwarobaini, na pilipili iliwe na soda kama keki, sina shaka nae kabisa.

Ninachojiuliza ni kwamba Aveva anatoa wapi ujasiri wa kuzililia pointi tatu ambazo ndani ya moyo wake anajua hawakuzistahili? Au inawezekana labda ametumiwa ujumbe mfupi na Kaburu ukisema “Kazi yangu ilikuwa ni kuzitoa pointi Kagera kuzileta kwetu, ulisema hatutaweza na tumeweza, sasa kazi yako ni kuzilinda zisiondoke. Mimi sina la ziada”..

Labda baada ya ujumbe kama huo ndio Aveva kaona na yeye acheze sehemu yake kwa kutuaminisha kwamba wao walikuwa pamoja kwenye kuzitafuta na kutaka kuitisha maandamano kulilia zisiondoke. Hapa tutampongeza Kaburu kwa juhudi zake za kuipa Simba ubingwa wa Protea.

Na ikiwa hili litashindikana, ninaanza kuona ipo siku tutamaliza msimu wa ligi kuu lakini hatutampata bingwa mpaka Kamati ya Protea ikae na kuamua, au ikiwezekana bingwa atapatikana pembeni ya njia panda ya makutano ya barabara ya Bibititi na Azikiwe, ndio mpira wetu unaelekea huko.

Mbali na kushukuru kusitishwa kwa maandamano haya, ninafurahi kwamba sijawaona walioandamana maana ningewadharau mpaka mwaka huu unaisha, ningewaona wapumbavu mpaka mwezi Desemba, ningewatukana mpaka mkesha wa mwaka mpya, ni aibu kubwa na fedheha ya uhakika. Wapo wana Simba waliosikitishwa na hili na kuapa kuacha kuishabikia tena timu hii kwa huu “upuuzi” wanaotaka kuufanya.

Simba wanataka kujificha kwenye mwamvuli wa kuonewa na TFF ili kutusahaulisha kwamba walikuwa mbele ya Yanga alama 8, na wakashindwa kuzilinda ndani ya michezo minne ya mwishoni wa mzungunguko wa kwanza, uzembe na ujuaji ndio unaitafuna timu si vinginevyo! Hizi stress naona mnataka kuzishushia TFF lakini kumbukeni hata mkipewa alama hizo bado mtashindwa kubebwa ubingwa kwasababu “mmelaaniwa”.

Ni hiyo “laana” peke yake ndio inawafanya mvurugane na kuwa na mwenendo mbaya mpaka mwisho wa ligi. Tubuni msamehewe, ubingwa ni kazi rahisi sana!

B: TANZANIA FOOTBALL FEDERATION (TFF)

Katika sinema hili, TFF kupitia kamati ya Nidhamu na hadhi za wachezaji maarufu kama kamati ya saa 72 au sasa ili kuokoa muda na ueleweke vizuri, unaweza kuiita Kamati ya Protea. Hawa jamaa wameonekana wazi kuwa na kigugumizi juu ya uamuzi wa ishu yenyewe.

Kikao cha kwanza kilifanyika kwa muda mrefu tu, lakini wakaja na jibu moja kwamba “Banda hatoruhusiwa kucheza mchezo wowote mpaka hapo atakapo adhibiwa” sasa ukiangalia kwa makini hii ni adhabu tayari, na kama Simba walikuwa hawajaingia katika Kamati hii nina hakika wangepinga hii hukumu ya Banda, huwezi kumfungia mchezaji wakati unatamka wazi unaendelea na uchunguzi, sasa ukija kubaini hana makosa utamlipa fidia?? Hii ilikuwa ni ujinga tu, lakini Simba hawakutia neno, walikuwa wanasubiri mpango wao uwekwe hadharani.

Siku zikapita, Saa 72 zikakata, na homa ikapanda bado kamati wapo kimya, wiki ikaisha. Ikafuata wiki nyingine yenye utulivu watu wote masikio na macho juu ya meza ya Protea, na hatimae hukumu ikatangazwa, Simba wakawa washindi…. Yaani walifungwa Kaitaba pointi zikabaki Bukoba, wao wakashinda Protea pointi zikaletwa Dar, who laughs last laughs louder wanasema wenyewe.

Sasa ukifuatilia utaratibu wa maamuzi juu ya suala hili, utaona uzembe mkubwa wa utunzaji wa kumbukumbu na utawalaumu sana TFF.

Lakini tusichotaka kufikiri ni kwamba taarifa hizi zinatumwa kwa email, hakuna namna zinaweza kupotea au kupindishwa, huhitaji kuwaita waamuzi waje waseme wanakumbuka nini juu ya mchezo uliochezwa muda mreefu uliopita, ni mazingira machafu ya rushwa na kubadili taarifa za uhakika, na ndio maana iliwachukuwa muda mrefu kwasababu walikuwa wanajaribu kurekebisha taarifa, ndio mawazo yangu hayo.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba SC, Ndg. Zacharia Hans Poppe yeye anasema “Mfungua email hakuwepo Dar wakati kamati inakaa, hivyo alitakiwa alirudi ilia je afungue email zake”, yaani Hans Poppe anajaribu kusema kwamba pale TFF kuna mtu ameajiriwa kwa ajili ya kufungua email, na asipokuwepo basi email haifunguliwi.

Mimi najiuliza hawa TFF wanatumia email za aina gani?? Yaani ilishindikana kabisa huyu “mfungua email” angalau aforward email ile kwa kamati hata kama yeye hayupo? Na ni yeye peke yake mwenye access na hiyo email hakuna mwingine?? Na hakuna ruhusa ya kuituma kwa kamati ya Protea??

Hapa inonekana kabisa Kamati ya Protean a Simba SC lao lilikuwa ni moja, na ndio maana unaona hata emails wameshindwa kuziamini eti wanaita watu waje waseme.

Mimi ninachokiamini ni kwamba Email ilitumwa Kabla mtu yeyeto hajajua kama Simba atafungwa na Kagera na kama Fakh atachezeshwa mechi ile, lakini watu wanaokuja kuhojiwa tayari haya yote yametokea, what do you expect??
Ndio maana utaona baada ya TFF tena kutangaza kupokea rufaa ya Kagera na kusema itapitia upya, Simba wamechanganyikiwa vibaya sana mpaka wanaongea “vumbi mixer pumba weka na povu” hawataki kabisa kesi hii irejewe, maana wataumbuka! Yaani hawataki kutoa mwanya kabisa hili suala litazamwe upya, wanatumia nguvu kubwa mno kuhakikisha kilichoamuliwa ndicho kiwe.

Pamoja na uzembe mkubwa wa baadhi ya watendaji wa TFF, kama Simba wana hakika haki ni yao basi wataipata tu hata kama watakuja FIFA kusikiliza.. ila mchezo wa TFF na Simba ndio unaotuharibia sasa taswira ya mpira wetu.
TFF ni lazima ijitathmini na itazame upya kamati hii ya Protea, suala hili limegubikwa na mashaka makubwa na mengi tu ambayo huhitaji diploma kuyang’amua.

Simba na kamati hii wawekwe kwenye kapu moja na kama itagundulika wana hatia wote waadhibiwe kwa mujibu wa kanuni za TFF, lakini pia TAKUKURU wakaribishwe ili wabaini ni kwa namna gani Yai limeweza kubadilika na kuwa Kitunguu maji.

Swali ni je, TFF kuna msafi wa kuthubutu kufichua uchafu huu? Lakini tunapoelekea uchaguzi kuna wakati faida inakuwa kubwa kuliko hasara, labda watavaa sura za bati ili watende haki ambayo kimsingi itawasaidia kupata kura kadhaa wakati wa uchaguzi.

Maamuzi juu ya hili yatategemea na mipango imekamilika vipi ili kushinda uchanguzi, kama wataweza kushinda bila wao basi Kagera watapatiwa haki yao, lakini kama wao ndio wapo kati kamailivyokuwa kwa uchaguzi uliopita, basi poleni sana Kagera na msirudie tena kuifunga Simba mechi za mwishoni hizi, iwe mwisho msimu huu msije mkashushwa daraja!!

Mpira umekufa, na jamaa wanaenda kuuzika.. Poleni sana wapenzi wa soka la ukweli.. please accept my heartfelt sympathy and sorry for your loss.

MY CONDOLENCES...

Jeff Gemo Mnyama Machine
The One Man Army
Affirmative Gemo The Great!
[HASHTAG]#SeriesFreeLife[/HASHTAG]
Season Two | Episode 7
dc1a729179011d90c317621c00fcf0f6.jpg
 
Ndugu yangu umechambua vyema yaliyojiri, lakini mimi sina cha kuongeza wala kuchangia kwa kuwa sehemu kubwa ya mada imehusu MPIRA WA MEZA ambao sina ujuzi nao kwani unachezwa indoors huko Protea.

Ama kama ungeuliza yaliyotokea Kaitaba Stadium, kamwe nisingekaa kimya maana ya pale yalifanyika mbele ya kadamnasi. Kapigwa mtu 2-1 kakimbilia polisi.

Ndugu zangu wa Msimbazi: "KUTOA MIMBA HAKUKUREJESHEI USICHANA WAKO, BALI UNABAKI KUWA MAMA WA MAREHEMU'. Hata leo aje nani na kuamua kuwa nyie ndio mnastahili kushinda mezani, ukweli utabaki pale pale kuwa 'Kaitaba iligeuzwa Mto Ngono na Simba Koko akapigwa Kat -r_ro'
 
Ndugu yangu umechambua vyema yaliyojiri, lakini mimi sina cha kuongeza wala kuchangia kwa kuwa sehemu kubwa ya mada imehusu MPIRA WA MEZA ambao sina ujuzi nao kwani unachezwa indoors huko Protea.

Ama kama ungeuliza yaliyotokea Kaitaba Stadium, kamwe nisingekaa kimya maana ya pale yalifanyika mbele ya kadamnasi. Kapigwa mtu 2-1 kakimbilia polisi.

Ndugu zangu wa Msimbazi: "KUTOA MIMBA HAKUKUREJESHEI USICHANA WAKO, BALI UNABAKI KUWA MAMA WA MAREHEMU'. Hata leo aje nani na kuamua kuwa nyie ndio mnastahili kushinda mezani, ukweli utabaki pale pale kuwa 'Kaitaba iligeuzwa Mto Ngono na Simba Koko akapigwa Kat -r_ro'

Hahahha duh hatari
 
Back
Top Bottom