Hili la watumishi wa TANESCO kutumia umeme bure ni jipu linalotakiwa kutumbuliwa. Hivi kweli watumishi wa umma wote kwenye taasisi / idara wanazofanyia kazi wangekuwa wanapata bure huduma wanazozitoa/ kuziuza ingekuwaje? Yaani kwa mfano wa idara ya afya watibiwe bure, wajenzi wa TBA wajengewe nyumba zao bure, walimu watoto wao wasome bure, wa maji wapatiwe maji bure, watengeneza sukari wapatiwe sukari bure, wa BOT wapatiwe fedha bure kwa unit 700 za fedha/ month na kadhalika?
Hili la watumishi wa TANESCO kutumia umeme bure ndilo linalosababisha kila wakati watake kupandisha bei ya umeme kila kukicha kwani wao hawajui machungu yake. Hawajui kuwa kwa sasa familia ya kawaida inayotumia umeme kwa kupikia, taa, fridge 2, washing & drying machine, TV 2, computer 2, water heaters na aircondtitioners inalipa shs 900,000/ hadi 1.2 m kama bili ya umeme kwa mwezi sawa na mshahara mzima wa graduate wa digrii kama si kuzidi.
Sasa TANESCO wanataka watu wasiwe na hivyo vitu majumbani mwao? Mbona ni vitu vya kawaida tu kama tunataka maisha bora kwa kila mwananchi. Na vitu hivi vimejaa madukani kwa bei nafuu kabisa lakini ukivinunua unashindwa kuvitumia kwa sababu ya TANESCO. Ndiyo maana watu na heshima zao walikuwa wanachezea mita za TANESCO. Wamefunga LUKU bado wanapandisha bei. Kinachotakiwa ni kuteremsha bei hizi kwa kiwango angalao cha 50%.
TANESCO ni kikwazo kikubwa cha maisha bora ya wananchi. Ni muhimu nao walipe bili za umeme kwa kiwango hicho hicho kama sisi kuanzia Mkurugenzi wao. This will bring senses into their minds.
Halafu tunataka watu wasikate miti kulinda mazingira. Wataachaje kukata miti ili wapate nishati angalao ya kupikia chakula? Umeme tumeusambaza hadi vijijini kwani ni wa nini? Kwani ni wa kuwashia taa tu? Mbona kuna taa nzuri tu za mchina za bei nafuu zinazotumia mionzi ya jua. Si kwamba tunapeleka umeme hadi vijijini ili kuboresha maisha ya hawa wananchi wakawaida? Ili angalao nao wawe na ka TV angalao ka inchi 12 badala ya redio ya mbao, wawe na angalao na kajiko ka plate moja badala na kuhangaika siku nzima kutafuta kuni na kuwa na macho mekundu kwa kupuliza mafiga? Sasa hili litawezekanaje kama kutumia vitu hivyo itabidi walipe TANESCO some Tshs 100,000/ au zaidi.
Hili jambo serikali ya awamu ya tano inawabidi walivyalie njuga kweli kweli.Bei zitelemke by at least 50%. Mikataba mibovubovu ya umeme kama ya IPTL, Dowans, Songas etc ifutiliwe mbali hata kama tutalazimika kuwalipa. Plants zote za kuzalisha umeme zimilikiwe na serikali. Hayo makampuni yaliyokuja kutuuzia umeme wa dharura yaondoke kwani dharura ilishakwisha kitambo. Ulishaona wapi dharura inakuwa ni ya kudumu kama si pale TANESCO tu? Waondoke tutawalipa pole pole tukitaka. Tusiogope kupelekwa mahakama ya kimataifa ya biashara: watatuelewa tu kwani tumenyonywa sana na haya makampuni.