Kuna mapenzi na kujitoa sadaka

minded tips

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2018
Posts
506
Reaction score
876
Mambo wana janvi, wote ni matumaini yangu ya dhati kua muwazima.

Kama kichwa cha habari kinavyosema hapo juu utofaut niuonao kati ya mapenzi na kijitoa sadaka.

Let's go...

Unapenda? Hayo ni matamanio yako. Unapendwa? Hiyo ni bahati yako. Wajibu ambao unapaswa kuutambua ni kumpenda anayekupenda.

Nifafanue hili; kumpenda anayekupenda haina maana kumwelekea akupendaye hata kama moyo wako haupo radhi. La! Bali kumwelewa na kumjibu kwa lugha bora isiyo na dharau, kiburi au manyanyaso.

Atakuja mtu atakayeonesha hisia kwako. Pengine wewe hutakuwa tayari au utakuwa na mwingine aliyezaja nafasi. Ni jukumu lako kumwelewesha akuelewe. Tumia lugha yenye kutambua na kuheshimu hisia zake.

Si vibaya ukamwambia kuwa kama usingekuwa na mtu, pengine yeye ndiye angestahili nafasi hiyo. Usiruhusu anayekupenda aumie. Hata hivyo, haimaanishi uumie wewe ili yeye asiumie au aumie uliyenaye ili kumfariji aliyekuja kukuomba mapenzi.

Muhimu kwenye maisha yako unapoyaelekea mapenzi au unapozikabili changamoto za kimapenzi ni kutambua nafasi yako; usiwe katili na usijitoe sadaka. Usimfanyie ukatili anayekupenda na usijitoe sadaka kwake kisa anakupenda.

Unalotakiwa kuzingatia zaidi ni kuwa hutakiwi kujitoa sadaka kwa mtu unayempenda. Lazima kutofautisha mapenzi na kujitoa sadaka. Maisha yako yanapokosa umuhimu kwa ajili ya mtu unayempenda hapo si mapenzi bali kujitoa sadaka.

KUPENDA NI KUJIPENDA

Unampenda mtu wakati huo unakuwa tayari kupoteza maisha kwa ajili yake. Hapo unataka huyo unayempenda akupende kweli? Inatakiwa uanze kwanza kujipenda, ujithamini na uyathamini maisha yako.

Unapompenda mtu na kutaka awe mwenzi wako, maana yake unataka unayempenda aingie kwenye maisha yako. Sasa ataingiaje kwenye maisha yasiyo na thamani? Kama upo tayari kufa kwa mapenzi ni sawa kusema mapenzi yanazidi thamani maisha yako.

Upo ulazima wa wewe kumwonesha kuwa maisha yako ni yenye thamani. Umfanye aingie ndani yako ili mkiridhiana basi muende pamoja. Hutakuwa na cha kumshawishi ikiwa wewe mwenyewe maisha yako unayaona si kitu.

Kupenda ni kujipenda; ndiyo, unapotaka mtu akupende inabidi wewe mwenyewe uwe unastahili kupendwa. Akuone unajipenda na avutiwe nawe. Hawezi kuvutiwa nawe kama hujipendi. Unapokuwa hujipendi, maana yake hujioni wa thamani. Wewe mwenyewe unajiona huna thamani, yeye thamani yako ataiona vipi?

Mpende unayempenda lakini jipende zaidi wewe. Mwoneshe unayempenda kuwa unamhitaji lakini mdhihirishie kwamba unajihitaji zaidi wewe. Usimfanye aone unamhitaji yeye kiasi kwamba wewe hujihitaji tena.

Mara nyingi watu huwadharau wenzi wao ambao huonesha kuwahitaji kuliko wanavyojihitaji. Huwaona hawana thamani, hivyo huwatenda wanavyotaka. Sasa kuzuia dharau na manyanyaso ya mapenzi kutoka kwa unayempenda, vizuri utangulie kumwonesha kuwa unajipenda na unajihitaji zaidi.

IPO SAYANSI HII

Wewe unampenda kwa sababu umevutiwa na uhusika wake. Jinsi alivyo imekuwa sababu ya wewe kuona anatosha viwango vyako vya mahitaji ya mwenzi wa mapenzi.

Inatakiwa naye avutiwe na uhusika wako. Akupende kwa jinsi unavyojipenda na kujihitaji. Hiyo ndiyo sayansi ya uhusiano wa kimapenzi. Inataka sana kuizingatia na kuiheshimu, vinginevyo mapenzi hupoteza maana.

Jiulize; wewe umempenda yeye kwa sababu umemuona anajipenda, yeye atakupenda vipi na hujipendi? Huoni utakuwa humtendei haki? Jipende ili naye aone yupo na mtu sahihi.

Ninapozungumzia kujipenda, kujijali na kuyajali maisha yako, sizungumzii ile hali ya kupendeza na kujiweka nadhifu. Nazungumzia utayari wa kuyalinda na kuyahifadhi maisha yako kwa nafasi ya kwanza.

Akija kwako na kukuta unayapa heshima kubwa maisha yako, naye atajifunza kuyaheshimu. Akikukuta unajichukulia poa, atakuchukulia poa. Mwoneshe kuwa wewe si mdoli wa kuchezea, atakuelewa na kulinda hadhi yako.

Zipo hisia za watu kwamba ukimpenda mtu na kujinyenyekeza mpaka kujionesha wewe si lolote kwenye maisha bila yeye, itamfanya akupende. Badala yake wengi wameumizwa kwa tabia hiyo. Kuna ambao ukiwaonesha uhusika huo basi wanaweza kuuchezea moyo wako kombolela. Watakugeuza mlinda kopo.

Moyo wako siyo wa kubutuliwa kama kopo la kombolela. Lazima uthibitishe kwamba wewe ni mtu mwenye misingi, hivyo kama anakuja kwako awe tayari kubeba gharama ya kuulinda utu wako kama wewe unavyoutunza. Onesha misingi ya utu wako na namna unavyotaka akuchukulie ili yakimshinda mapema umwambie kwaheri!

SOMA KISA HIKI

Nilipokea simu kutoka kwa Vedasto (si jina lake halisi), mkazi wa Njombe, alinisimulia kisa chake na mpenzi wake anayeitwa Shuja. Alianza kusema: "Kaka naumia sana. Siwezi kuishi bila mpenzi wangu lakini naye hanitaki."

Ikabidi nimsikilize Vedasto kwa umakini wa hali ya juu. Akanisimulia jinsi alivyoishi na Shuja. Na namna alivyoamua kuyaacha mambo yake mengi ili kumridhisha mwanamke wake huyo.

"Nilikuwa na mipango ya kwenda chuo mwaka jana ila nilighairi ili nipate muda wa kumhudumia, maana niliamini ananihitaji sana," alisema Vedasto, akaendelea: "Yote ambayo nimeyafanya yeye anaona hayana thamani na sasa ananiacha, mimi nitaishi vipi?"

Vedasto alisema kuwa Shuja alianza kukosa uaminifu, akawa na wanaume wengine. Kuna mara kadhaa alimfumania kabisa. Pamoja na kumfumania, yeye alimsamehe kwa imani kwamba angebadilika na kuwa mwanamke bora wa kufaa kuitwa mke wa ndoa.

Siku moja usiku wakiwa wamelala, simu ya Shuja iliita. Hakujua mpigaji ni nani. Shuja alipokea simu. Spika ya simu ilikuwa inatoa sauti kubwa, hivyo pamoja na kwamba haikuwa loudspeaker, aliweza kusikiliza kila kilichokuwa kinazungumzwa hadi na mtu aliyepiga ile simu.

"Hakuwa na uoga na mimi hata kidogo. Fikiria alizungumza kwa uhuru na mwanaume mbele, tena mazungumzo yenyewe ya mapenzi. Kwa masikio yangu nikasikia yule mwanaume kwenye simu akimpongeza kwa penzi tamu alilompa siku hiyo. Hapo nikagundua kumbe siku hiyo alitoka kukutana na mwanaume.

"Kumbe mimi nilikuwa narudi nyumbani ananinunia kwa sababu anakuwa ametoka kwenye mambo yake mabaya. Waliongea wakapongezana. Wakaahidiana wangekutana tena baada ya siku mbili. Roho iliuma nusura ya kupasuka. Nilimshika Shuja kwa nguvu, nikatamani nimpige lakini nikaona haukuwa uamuzi sahihi," alisema.

Anazidi kueleza kwamba usiku hakulala kwa maumivu ya moyo. Shuja alimsonya kisha akalala zake. Asubuhi palipokucha, Shuja akachukua nguo zake na kuelekea nyumbani kwao. Alijaribu kumzuia asiondoke lakini hakufanikiwa.

Vedasto anasema alimfuata Shuja nyumbani kwao, akampigia magoti kumuomba msamaha arudi nyumbani japo hakumkosea, lakini hakuelewa. "Huwezi kuamini kaka, ili kumwonesha nampenda ilibidi nijichome kisu kifuani, damu zikatoka, nikamwambia nimefanya vile kumwonesha nampenda na nipo tayari kufanya lolote kwa ajili yake.

"Kila nilichofanya hakukielewa. Jioni ya siku hiyo nikiwa nyumbani nimejiinamia na jeraha langu la kisu kifuani, polisi walikuja kunikamata. Kumbe Shuja, mama yake na mjomba wake waliniripoti polisi. Nilipewa kesi ya jaribio la kujiua na kumtishia maisha Shuja. Nilikaa mahabusu siku moja ndugu zangu wakaniwekea dhamana nikatoka," alisema Vedasto.

Akahitimisha: "Sijui kama nitaishi bila Shuja. Nampenda sana pamoja na tabia zake mbaya. Moyo wangu unang'ang'ania niwe na yeye."

NILICHOMSHAURI VEDASTO

Kwanza nilimuuliza kama anafahamu kuwa kanuni ya kuheshimiwa inaanza kwa mtu kwamba sharti ajiheshimu. Alipokubali, nilimuuliza kama anajiheshimu, aliponijibu anajiheshimu nikamaambia anasema uongo.

Nikamuuliza kama anajipenda, alipojibu anajipenda nilimkatalia. Nikamuuliza kama anajikubali. Jibu lake pia nililikataa. Nikamuuliza kama ana wazazi, akajibu anao, nikamuuliza kama anawapenda. Alisema anawapenda wazazi wake lakini nikamwambia anaongopa.

Nilimwambia Vedasto kuwa isingekuwa rahisi kufanikiwa kumweka Shuja kwenye himaya yake wakati anamwonesha kutojijali binafsi na maisha yake. Shuja atajiuliza: "Mtu yupo tayari kufa sasa wa nini? Mtu maisha yake hayathamini sasa wa kazi gani?"

Nilimweleza Vedasto kuwa unyonge, kujiliza na kudhihirisha mahangaiko kwa unayempenda humjengea kiburi na kuona huna cha kupindua kwake. Dawa ya anayekuchukulia poa ni kumwonesha ni kwa kiasi gani unajipenda na kujikubali.

Inauma sana kumwacha unayempenda aende alikoamua. Hata hivyo kumpigia magoti, kujiliza, kujinyenyekeza na kujichoma kisu haisaidii kumrejesha. Unachoweza kufanya ni kuamua aende akiwa anakuheshimu au aende akikudharau.

Ukitaka akuheshimu ni jukumu lako kuficha maumivu. Mwambie aende. Ndani moyo wako unaungua lakini vumilia. Ukiwa peke yako hata machozi toa. Akiwa mbele yako pambana na maumivu ya moyo ili asiyaone. Akiondoka atajua alimchezea mtu anayejipenda.

Nilimwambia wazazi wake wanampenda sana. Amekuwa mkubwa, anayo nafasi ya kuwapa faraja. Si jambo jema wazazi kumuona mtoto wao akitaka kujiua kwa sababu ya mapenzi. Ni kweli inauma, lakini anayekutenda lazima apate ujumbe kuwa wewe ni wa thamani. Muhimu zaidi ni kwamba unaweza kuishi bila yeye.

Mwisho kabisa nilimwambia maisha lazima yaendelee. Maisha hayawezi kufika mwisho kisa mpenzi wako ameamua kukuacha. Ukitaka mpenzi wako akupende na akuheshimu, anza kujiheshimu na kujipenda. Mwoneshe maisha yako ni muhimu na unayapenda sana kuliko mapenzi yake.
 
umejiunga jana tuu.....nasubiri nyingine ndefu zaidi.......
[emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23] [emoji23]
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…