Kumbe Zitto Kabwe aliyoongea haya fuatilia Mjadala Wa Bunge

Hansen Nasli

JF-Expert Member
Mar 18, 2012
883
337
b27e3b193b71956bc47d3748f15f2eb3.jpg


Someni na hii ya mwaka 2010

MJADALA WA KUTUNGA SHERIA YA MADINI 2010
Mkutanoni Bungeni!Aprili, 2010

Mheshimiwa Spika,

Napenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kushiriki katika kuchangia Muswada huu kama jinsi mwenyewe ulivyoita kwamba ni Muswada wa kihistoria kwa sababu inachukua muda kwa nchi kukaa na kutunga Sheria ya Madini. Tutakumbuka kwamba tulikuwa na Sheria ya mwaka 1979 tukatunga nyingine mwaka 1998 na sasa hivi mwaka 2010 ndiyo tunatunga Sheria nyingine, kwa hiyo, inaweza ikachukua miaka na inategemea na jinsi Sheria hii itakavyokuwa inaweza ikachukua muda mrefu zaidi hata kwa kipindi cha kati ya sasa na Sheria ambayo inatumika sasa kuweza kuwa na Sheria nyingine ya Madini.

Mheshimiwa Spika,

Mimi nitapita pale ambapo Kambi ya Upinzani Bungeni imepita asubuhi wakati tunatoa maoni yetu kama jinsi ambavyo yaliwasilishwa na Mheshimiwa Jussa kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani - Mheshimiwa Mnyaa, kwamba Sheria hii mpya tunaitarijia iweze kujibu zile changamoto tatu ambazo tumeziainisha na tumeweza kuonyesha ni maeneo gani ambayo tunadhani bado Sheria hii haijaweza kuyaelezea kama jinsi ambavyo inavyotakiwa. Lakini napenda nitoe pongezi za dhati kabisa kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Wabunge wote ambao walishiriki katika kuipitia Sheria hii.

Mheshimiwa Spika,

Tunavyopitisha Sheria hii leo ni tofauti kabisa na ilivyokuja mwanzo. Kuna mambo mengi sana ambayo tumefanikiwa kuyaongeza katika ngazi ya Kamati na katika hili pia napenda kuwapongeza kabisa Waziri wa Nishati na Madini - Mheshimiwa Ngeleja na Naibu wake Mheshimiwa Malima kwa kuwa wasikivu na kupokea maoni mbalimbali ya Kamati na kuweza kuyafanyia marekebisho. Hawakuwa wabishi na hii inaonyesha ni jinsi ambavyo Wizara ambazo tunawakabidhi vijana zinavyokuwa na utendaji ulio imara, imara zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,

Napenda niwapongeze kwa dhati kabisa vijana wenzangu kwa jinsi ambavyo waliweza kupokea na tulikaa sana toka siku ya Ijumaa, Kamati ya Nishati na Madini inashughulikia Muswada huu na tulikuwa tunakaa mpaka usiku! Tulikuwa hatukai Bungeni kabisa! Kwa kweli Wajumbe wote walioshiriki walifanya kazi nzuri sana. Ni masikitiko yangu tu kuwa baadhi ya Wabunge ambao wanatoka maeneo ambayo yana migodi na wamekuwa wakilalamika sana kuhusiana na masuala ya rasilimali hii ya madini hatukuwaona kabisa kwenye Kamati na hatujawaona kabisa hata hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika,

Inaweza ikaja baadaye watu hao hao ndiyo wakaanza kulalamika kwamba Sheria ni mbaya ama ni nini wakati fursa ya kushiriki katika utungaji wa Sheria walikuwa nayo. Katika hili napenda kwa dhati kabisa nimpongeze sana Mbunge wa Simanjiro - Mheshimiwa Ole-Sendeka pamoja na kwamba alikuwa ana Miswada miwili, ule wa Mifugo na Madini, lakini bado alihakikisha anakuwepo mara zote kuhakikisha kwamba analinda maslahi ya wapigakura wake. Vilevile nampongeza Mbunge wa Busanda - Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, naye pia alishiriki muda wote. Sasa natarajia kabisa kuwa wale ambao hawakushiriki wasije kuturudisha nyuma, wakubaliane na yale ambayo wenzao wameweza kushiriki na kuweza kuyapitisha.

Mheshimiwa Spika,

Licha ya yale ambayo tumekubaliana, kuna mambo ambayo hatukukubaliana ambayo tukasema kuwa tutakuja kuyazungumza ndani ya Bunge. Yale ambayo tunadhani kuwa hii ndiyo fursa ya kuweza kuyazungumza, mengine yameshazungumzwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, la Kwanza alizungumza Mheshimiwa Ole-Sendeka kuhusiana na kutoa leseni kutokana na Mashapo, leseni za uchimbaji mkubwa na Mheshimiwa Ole-Sendeka amezungumza hapa kwamba yeye report ya Bomani ndiyo Msahafu. Lakini nilikuwa naomba nirejee report ya Bomani ilisema nini kuhusiana na utoaji wa leseni za uchimbaji mkubwa SML, maana yake kulikuwa kuna malalamiko makubwa sana kama mnakumbuka.

Mheshimiwa Spika,

Ni kwamba MDA tulizokuwa tunazitoa kwa muda wa miaka 25 ni nyingi sana na bahati nzuri mimi nilishiriki kwenye Kamati ya Bomani. Tukapata maoni mengi sana ya wadau wanaosema kwamba miaka 25 ni mingi sana, haiwezekani kutoa leseni au kuwa na MDA kwa miaka 25 ni mingi mno irekebishwe na mapendekezo mengi yaliyokuja ni kwamba leseni zitolewe kutokana na Mashapo ambayo yanapatikana katika lile eneo. Sasa pendekezo letu la 4.1.3 ninasema kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Kamati ya Bomani inasema: “Leseni za Uchimbaji mkubwa SML zitolewe kulingana na Mashapo.”

Mheshimiwa Spika,

Sasa Serikali yenyewe imetekeleza hilo, imetekeleza uamuzi wa Bomani. Kwa hiyo, wale waumini wa Report ya Bomani labda inabidi turudi tena kwa Bomani tumwambie Rais atuunde kwa siku chache, tunaweza kulirekebisha hili, lakini kwa kweli kwa hili Serikali imehamisha kama jinsi ilivyopendekezwa kwenye report ya Bomani. Kwa hiyo, nilikuwa ninapenda niwaelimishe wenzangu hivyo na kwamba kwa vyovyote vile katika utungaji wa Sheria kuna compromise kama nilivyosema kuna mambo ambayo Serikali ilikuja nayo, tukawakatalia tukayarekebisha. Kuna mambo ambayo sisi tumekuja nayo wakayakubali, kuna mambo ambayo hatujakubaliana lakini kwa hili tukiwanig’niza tunakuwa tunawaonea kwa sababu wamelitoa katika taarifa ya Bomani kama jinsi ambavyo tuliwaomba na tulivyowataka watekeleze taarifa ya Bomani.

Mheshimiwa Spika,
Lingine ambalo hatujakubaliana ni suala zima la jinsi gani ambavyo tunahakikisha kwamba rasilimali za madini zinafaidisha wale watu ambao rasilimali ile imepatikana kwao. Msemaji wa Kambi ya Upinzani amezungumza na nilikuwa naomba nichangie hili pia kwamba Kamati ya Bomani ilipendekeza kwamba sehemu fulani ya mrahaba irudi katika maeneo ambayo yana migodi na tulipendekeza asilimia 20 ya mirahaba hii. Serikali imelikataa, lakini haina maelezo ya kina ya kwa nini imelikataa. Sisi tunadhani hili ni jambo jema na jambo hili litapunguza sana kelele za wananchi kwa sababu wataweza kuona kwamba sehemu ya rasilimali inachimbwa katika maeneo yao, inarudi. Tulikuwa tumependekeza kwamba asilimia 20 ya mapato yanayotokana na madini yarudi kwenye Halmashauri za Wilaya kule madini yanapopatikana.

Mheshimiwa Spika,

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba hili Serikali iendelee kulifikiria na ililete katika Muswada huu. Jambo la msingi hapa ambalo ni conception ni kwamba hatutaki asilimia 20 ya mapato yanayokusanywa kama kodi. Kama kodi ya mapato, revenues na charges nyingine, tunachokitaka ni asilimia 20 ya mrahaba kwa sababu mrahaba siyo kodi, kimsingi mrahaba ni compansation ya unyonyaji wa yale madini kule chini siyo kodi. Kwa hiyo, hii inaweza ikarudi kule, na hairudi kwenda kuwagawia watu waende wakazitumie, inarudi kwa ajili ya kwenda kwenye Halmashauri, kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika,

Nitakupa mfano mzuri sana. Ni kwamba eneo lolote ambalo madini yanapatikana, Halmashauri za Wilaya zinapata taabu sana kwa sababu idadi ya watu katika yale maeneo inaongezeka. Maana yake ni kwamba idadi za hospitali zitaongezeka, idadi ya mashule itaongezeka na idadi ya huduma za maji itaongezeka. Kwa hiyo, leo huwezi kupanga bajeti ya Wilaya ya Kahama sawa sawa na Wilaya ya Kigoma. Haiwezekani kwa sababu Wilaya ya Kahama mahitaji ya watu wa Kahama ni kubwa zaidi kuliko ya watu wa Kigoma kutokana na upatikaji wa ile rasilimali pale na watu kuongezeka zaidi.

Mheshimiwa Spika,

Ndiyo maana tunasema kwamba sehemu hii iweze kwenda, na wala hii haitakuwa mara ya kwanza. Watu wote ambao wana vitalu vya uwindaji asilimia 25 ya mapato yanayotokana na vitalu yanarudi kule ambako rasilimali ile inapatikana. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba hili liweze kuangaliwa ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanafaidika. Hili hatukukubaliana katika Kamati, ndiyo maana tumelileta hapa ili Bunge zima liweze kutafakari na kuona ni jinsi gani tunaweza kulifanya.

Mheshimiwa Spika,

La pili ambalo hatukuweza kukubaliana ni suala la uanzishwaji wa Mineral Development Fund. Waziri amelieleza pamoja na lile la Mamlaka, lakini alivyolieleza ni tofauti na jinsi ambavyo Serikali iliji-commit kwenye Kamati kwa sababu ninayo nakala hapa ya Serikali inasema kwamba “on establishment of Mineral Development Fund the Government will make a commitment to establish the Fund in the future.” Katika maelezo ya Waziri wa Nishati na Madini alipokuwa anazungumza hapa, leo amegusiagusia Mineral Development Fund hakutoa commitment ambayo aliiahidi kwenye Kamati, kwa hiyo, tunachokitaka tunajua kwamba uanzishwaji wa sovereign Wealthy Fund siyo kitu kidogo. Kama Serikali ingekuwa imejiandaa toka mapema miaka miwili iliyopita toka report ya Bomani imewasilishwa, leo tungeweza kuwa na Muswada ambao umehusisha uanzishwaji Sovereign Wealth Fund, lakini angalau Serikali ingeweka commitment ndani ya Bunge hapa kusema kwamba Sovereign Wealth Fund ni jambo ambalo linakubalika.

Serikali italifanya kwa hatua hizi na hizi na faida ya Sovereign Wealth Fund ni kuweza kusaidia kuwekeza katika maeneo ambayo labda ni magumu kuweza kuwekeza, inaweza ikajenga ma- university ambayo yanatasaidia kujenga uwezo wa Watanzania. Inaweza ikajenga mabarabara, inaweza ikapeleka huduma za maendeleo katika maeneo ambayo yapo kule, lakini pia fedha ambayo inatokana na hii Sovereign Wealthy Fund inaweza kutumika kuwekeza kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika,

Mfano mzuri tulionao na nilizungumza na Governor wa Benki Kuu kwamba wakati Kampuni ya African Barrick Gold imetangaza kuuza hisa zake katika soko la hisa la London, kama tungekuwa na Sovereign Wealthy Fund yetu, tungeweza kushiriki katika ununuzi ule moja kwa moja kutokana na Sovereign Wealthy Fund yetu. Tungekuja huku zile free carried interest zingeongezea katika zile ambazo tayari tunazo na zile za negotiation na Serikali na wenye leseni zingeongezea zaidi, kwa hiyo, tungeweza kumiliki sehemu kubwa sana ya migodi ambayo inamilikiwa na hiyo kampuni ya African Barrick Gold. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu sana Serikali iangalie uwezekano huu na itoe commitment kama ilivyoahidi kwenye Kamati.

Mheshimiwa Spika,

Kwa sababu kwenye Kamati ilisemwa very firmly ilivyofika hapa Bungeni wakaizungumza juu juu, kwa hiyo, tunatarajia Waziri ataweza kutoa hiyo commitment.

Mheshimiwa Spika,

Lingine ambalo ninadhani litakuwa la mwisho, kutokana na muda ni suala la section 25 inayohusiana na prohibition. To prohibit access to information, sasa kama Taifa tumeshaji- commit kwenye transparency kwenye sector ya exertive industry, tunafahamu kwamba Serikali ipo katika utaratibu au mchakato wa kuleta Sheria kwa ajili ya kuiweka Kisheria ile extractive Industry transparency initiative kama jinsi ambavyo Msemaji wa Upinzani alivyozungumza hapa asubuhi. Lakini tayari ile section 25 itaweza kubana hata hiyo Sheria tutakayoitunga kwa sababu ile inakataza katakata information zozote kuweza kutolewa. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kui-relax ile section 25 ili isiweze kutuletea taabu wakati tunafanya utekelezaji wa extractive Industry to transparency initiative ambapo tayari Kamati imeshaundwa na Mheshimiwa Judge Bomani ameshateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii. Kwa hiyo, kwa heshima ya Judge Bomani Serikali ingeweza ku-relax kile kipengele kuhakikisha kwamba hatutapata matatizo katika uanzishwaji wa hii IT.

Mheshimiwa Spika,

Hapo hapo kuna wakala wa Serikali ambao tumeuanzisha baada ya matatizo ya Alex Stuart, gharama ambazo tulikuwa tunalipa kwa Alex Stuart. Lakini taarifa ambazo Alex Stuart waliweza kuzitoa, tumeanzisha wakala wa Ukaguzi wa Migodi lakini wakala huu katika Sheria nzima hakuna hata sehemu moja ambayo wakala huu unatajwa kama jinsi ambavyo Msemaji wa Upinzani alisema. Kwa hiyo, tulikuwa tunahitaji mabadiliko mahususi ya maeneo mahususi yafanyike na hasa pale kwenye ruhusa ya kuingia kwenye migodi siyo watu wa TRA tu, siyo Kamisha wa madini tu na watu wake bali pia na watu wa wakala hii.

Mheshimiwa Spika,

Kama wakala wa jiolojia ametajwa kwenye Sheria, kipi ambacho kinazuia wakala hii ya kukagua migodi hii kuweza kutajwa kwenye Sheria? Masuala ya Mamlaka yameelezewa vizuri sana na Msemaji wa Upinzani Bungeni. Hili ni suala ambalo halijawa addressed kabisa, ndiyo suala ambalo lingeweza kutusaidia kuhakikisha kwamba sekta hii inasimamiwa vizuri. Lakini mabadiliko makubwa ambayo tumeyafanya kwenye Muswada na usikivu wa Wizara ya Nishati na Madini, Waziri pamoja na Watendaji wake wote ambao tulikuwa nao, tulikuwa tunakesha nao kwa kazi hii. Imeonyesha ni jinsi gani ambavyo kwa pamoja Bunge, Kamati ya Nishati na Madini pamoja na Serikali tumeweza kuhakikisha kwamba tumeboresha Muswada huu na iwapo mambo haya ambayo tumeyazungumza na kuona kwamba bado hatujakubaliana nayo, bado yale yanayohitaji commitment ikatolewa commitment, yale yanayohitaji mabadiliko ya Kisheria yakafanyiwa mabadiliko ya Sheria ya sasa, kwa kweli tutakuwa na Muswada mzuri sana ambao utasababisha tuweze kumiliki vizuri rasilimali zetu za madini na kama mabadiliko haya yakifanyika hatutakuwa na sababu ya kukataa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

Kikao cha Tisa – Tarehe 23 Aprili, 2010

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kifungu hicho cha 10(2) kama kilivyoboreshwa kwenye schedule of amendment, lakini kifungu hiki hakionyeshi lile suala la listing at a stock exchange. Tutakuja kukuta tutakapofika kifungu 109 ambacho kinapingana na kifungu cha 10(2). Kwa hiyo, nadhani kwamba tunahitaji kukiboresha kifungu cha 10(2) ili ile element ya listing ihamie kwenye 10(2) na kuiondoa kwenye 109. Kwa sababu, ukizisoma zote kwa pamoja, ama moja inakuwa ni redundant au ina-contradict.

MWENYEKITI:
Mheshimiwa Waziri, sijui umeipata vizuri hiyo?

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Zitto kwa sababu tumekuwa naye kwa muda, hasa wakati wa maandalizi haya ya Muswada huu na hasa wakati Mkutano huu unaendelea. Sasa hapa, ninaelewa, kuna mahusiano, lakini tukifika huko, nitaelezea maudhui ya kifungu cha 109. Yako mambo ambayo kifungu cha 109 kime-envisage, lakini hayako necessarily captured hapa. Kwa hiyo, kuna mazingira fulani yanaweza kutokea, lakini tutaweza kuelezea.

MWENYEKITI:

Kwa hiyo, hiki ni cha ujumla kuhusu development agreement na specifics ziko kwenye 109.

MHE. KAMBWE Z. ZITTO :

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Bila kuiondoa hoja ya Mheshimiwa Cheyo bado inasimama lakini naona kuwa mazungumzo yanayoendelea ni kama kwamba hii negotiation kati ya Waziri na licence holders. Mabadiliko yanasema the Government and licence holders maana mazungumzo yanayoendelea sasa hivi ni ya Waziri hapana ni the Government isije ikaonekana kwamba spirit tunampa kibali Waziri kwenda ku-negotiate mabadiliko yana sema negotiated upon between the Government and Mineral Rights holders lakini bado hoja ya Mheshimiwa Cheyo naomba iendelee kupatiwa majibu.

MWENYEKITI:

Nilidhani unasaidia lakini, Mheshimiwa Karamagi hebu tuchote uzoefu hapa.
Ibara ya 10

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Spika, taarifa.

MWENYEKITI:

Taarifa Mheshimiwa Kabwe.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Taarifa tu kwa sababu naona kila Mjumbe wa Kamati yako anazungumza kana kwamba tunampa power Waziri. Kama nilivyosema hapo awali ukisoma 10(1) ndiyo inasema Minister may wala siyo shall kwa sababu jambo hili tumelizungumza sana kwenye Kamati ya Nishati na Madini na hata kuondoa neno Waziri kuliweka Government was a purpose ku-make sure kwamba tunalinda hilo ili asiwe ni mtu mmoja. Kwa hiyo, unatakiwa sasa kusoma moja ni Minister may.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Lakini mbili the level of free carried interest kwenye Amendment ukurasa wa tatu. The level of free carried interest and State participation in any mining operations under a special Mining licence shall be negotiated upon between the Government and Mineral rights holder and not between the Minister, kwa hiyo, tusiondoke hapa, kuna spirit inasema Waziri anakwenda ku-sign, naomba hilo liwe clear maana yake naona kila mtu anarejea Waziri,Waziri, Waziri.

MWENYEKITI:

Mheshimiwa Waziri Mkuu.

WAZIRI MKUU:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tatizo hapa unajua ukiumwa na nyoka hata jani likigusa unaogopa. Kwa hiyo, hoja ya Mheshimiwa Cheyo inatokana na hofu ambayo hatuwezi kuipuuza haraka haraka, kwa hiyo, nafikiri twende na yote mawili. Ndugu yangu anajaribu kuonyesha kwamba Government, Waziri kwa hiyo tukiita Government, tukiita Minister bado hofu itabaki palepale tu, the best that we can go with ni kwenye kanuni wakati wa kutengeneza kanuni tuonyeshe bayana kwamba jambo litatengenezewa mfumo wa kuwa na a Government negotiating team ambayo itakuwa ime-take into account inter ministerial salt of setup akiwemo na Attorney General na wataalam na vitu vingine kama hivyo ili kutupa comfort kwamba jambo hili limesimamiwa vizuri katika level ya negotiation. ( Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Naona tukiiweka hivyo itatupa mwelekeo mzuri zaidi na tutakuwa much more comfortable.

MWENYEKITI:

Nadhani, alichotusaidia hapa Waziri Mkuu kinatusogeza karibu ya pale ambapo Bunge zima lingekusudia, kwamba uhuru huu ukiachwa wazi hapa, kwanza Government ukiwa na Waziri Mbabe si anasaini tu, Ndiyo! Hivi Waziri akienda kusaini hao wanaolalamika wanakwenda wapi, No, no, no! Tumekuwa kwenye Serikali tunajua, unaweza ukasaini kwa niaba ya nchi na ukasema hiyo ndiyo power yangu, sasa mpaka ije kuwa mgogoro tayari nchi imekwishapata matatizo. Kwa hiyo, ni kweli kabisa tukiweka kwenye Kanuni kama anavyopendekeza Waziri Mkuu, inamfunga sasa huyo Waziri ingawa bahati mbaya pia anaweza ku-repeal regulations, lakini pengine Kamati ya Mheshimiwa Simbachawene hapo itamwona, afadhali hiyo kidogo. (Kicheko)
(Kifungu kilichotajwa hapo juu kilipitishwa na Kamati ya Bunge Zima pamoja na marekebisho yake)

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Spika,

Hivi sasa tunapozungumza Dar es Salaam, kuna matapeli wakubwa sana wa madini, kuna watu ambao wanakuja kutoka nchi mbalimbali na hasa kutoka Russia na wananunua madini kinyume cha taratibu na wanapigwa kweli, wanaibiwa kweli, kwa hiyo kipengele hiki cha sheria napingana kabisa na Mheshimiwa Cheyo, kipengele hiki kinadhibiti ufahamu wa madini ambayo yameuzwa na kinadhibiti watu ambao wanafanya utapeli wa madini ambao sasa hivi umeshamiri sana Dar es Salaam, watu wanaibiwa mpaka milioni mia nane na kadhalika. Jambo ambalo tunapaswa kuliweka, kwanza kama viongozi ni lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya maamuzi ambayo tunayafanya lazima yawe magumu ili watu wetu wafuate taratibu wasiwe informal, hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Lakini jambo la pili hii sheria inaishusha sasa ofisi ya Kamishna kutoka Dar es Salaam mpaka chini kunakuwa na zonal, kwa hiyo sisi Waheshimiwa Wabunge tuwashauri watu wetu kama anachimba choo akakutana na diamond, kama mvua imenyesha akakutana na dhahabu aende haraka kuripoti kwa Zonal Commissioner wa levy, au aende akaiuze kwa license dealer , kwa sababu akiiuza kwa license dealer ndiyo sisi tunapata royalty, akiuza kimya kimya hatupati royalty ndiyo maana hasa ya hiki kipengele.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kwa hiyo, naomba kama ulivyosema hiki kipengele ni sawa na kinaondoa woga wa Mheshimiwa Cheyo kwa mambo ya building materials na chumvi kwa sababu section ya pili inakifuta, kwa hiyo, Bunge likipitishe.

MWENYEKITI:

Tumsikilize Mheshimiwa Cheyo kwanza maana yake ndiye aliyeanzisha hii hoja.

Ibara ya 18

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI:

Taarifa.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mheshimiwa Kaboyonga ametoa reference ya liberalization ya dola, kinachoua uchumi wetu sasa hivi ni hiyo liberazation. Ukienda nchi nyingine leo hununui dola kama unavyonunua Tanzania. Hatuwezi kurudi nyuma kuendelea kui- re-enact ile sheria. Lakini what is cleaning our economy kwenye currency kwenye Forex ni liberalization ya dola. Kwa hiyo, hatuwezi kuruhusu makosa ambayo tumeyafanya kwenye liberalization ya dola tukiirejea kwenye dhahabu. Tunachozungumzia hapa ni mali za nchi ambazo hatuwezi tu kuachia watu tu wakauziana uziana tusipate royalty inayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Bahati mbaya sana Mheshimiwa Lembeli hakuwepo kwenye Kamati ya Nishati na Madini na kwake kuna mgodi, nilishangaa sana kwa nini hakuwepo kwenye Kamati ya Nishati na Madini wakati tunajadili kitu kama hiki. Suala kama hili tumelijadili kwa undani na kuweza kuona jinsi ya gani ya kuweka water tight kuhakikisha kwamba rasilimali zetu tunaweza tukazilinda vizuri. Nakubaliana kabisa kwamba lazima tuangalie kwenye kanuni jinsi gani wananchi wetu wa kawaida kabisa kule chini ambako hamna structure jinsi gani ambavyo wanaweza kufaidika. Lakini tukiacha sheria wazi, tunakuwa tunakwenda kuwalinda matapeli wa Dar es Salaam ambao kila siku wanaharibu sifa ya nchi kwa kuwapiga watu kwa utapeli wa dhahabu.

MWENYEKITI:

Mimi jamani nashauri tufuate mwongozo wa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye vitu kama hivi kwa sababu kwenye kanuni ukitaka kulichukulia jambo hilo ni jipesi zaidi kumlinda mwananchi ambaye sio tapeli, si basi tu amepata bahati tumwachie Waziri kwenye kanuni aliweke vizuri. Hapa tusibadili chochote. Lakini kwenye kanuni liwepo. Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,
nashukuru Serikali imesikia na italifanyia kazi kwenye kanuni. (Makofi)

(Ibara iliyotajwa hapo juu ilipitishwa na Kamati ya Bunge Zima bila mabadiliko yoyote)

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mheshimiwa Waziri alipokuwa anamjibu Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka amezungumza kwamba TMAA haiwezi kuwekwa hapa kwa sababu inaundwa na sheria nyingine. Lakini ndani ya sheria hii tumeiweka ile Geological Survey Agency ambayo nayo pia imeundwa kwa sheria nyingine. Ndani ya sheria hii tumeiweka TRA ambayo nayo pia umeundwa kwa sheria nyingine. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kutokuweka TMAA kwa sababu hiki ndiyo chombo ambacho kinahakikisha wawekezaji mitaji ambayo wanaweka, dhahabu au Tanzanite au chochote kile ambacho wanakichimba kinaweza kikawa na transparent. Hiki ndio chombo ambacho tumekiunda na initiative yao wenyewe Serikali wanamzaa mtoto halafu wanataka kumuua, wanataka kumnyima kazi za kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Hakuna sababu yoyote ile ambayo Serikali inaweza ikaitoa kutokuweka TMAA hapa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kama sehemu ya Authorising Officer, naungana kabisa na Mheshimiwa Ole-Sendeka kwamba Wakala huyu ambaye tumemuweka kwa ajili ya ku-Maximize Government Revenue awekwe. Kwa nini huyu tu atoke? Geological Survey yupo kwa sababu anaonyesha kwamba kuna maeneo, TRA yupo. Lakini mtu ambaye anamwambia TRA kwamba huyu mwekezaji amedanganya au hajadanganya anaondolewa. Kuna kitu gani? Kuna bad faith hapa. Nilikuwa naomba kwamba Waziri akubali TMAA iwekwe kwenye mazingira yote ambayo yanatakiwa kuwepo. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Namshukuru tena kwa mara nyingine Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka pamoja na Mheshimiwa Kabwe Zitto. Kwanza hakuna sababu yoyote ya kwa nini sijui ikafiriwa kwamba TMAA hapa haionekani. Kama tulivyoeleza kwamba Serikali ilikuwa inatafakari kwa sababu jambo hili kiserikali tumeliongea sana tumezungumza sana. Mheshimiwa Kabwe Zitto amekwenda hatua mbele kidogo kwa sababu Mheshimiwa Christopher Ole-Sendeka alikuwa anachoongea ni hawa Authorised Officer. Ukisoma kwenye interpretation clause, waliopo kule Authorised Officer ni wale wafanyakazi chini ya Commissioner wa Madini, wapo wengi ambao wanaweza kufanya shughuli. Lakini kwa hili ambalo linahusu TMAA nasema hakuna ubaya wowote kuwepo hapa. Lakini Serikali ilichokuwa inasema ni kuomba muda kwa sababu mchakato huu kwa nini unaendelea? Tulikuwa tunasema mtupe muda huo tuendelee kutafakari, lakini sio kusema kwamba jambo hili haliwezi kuingia hapa, hatujasema hivyo. Serikali iko tayari kuliweka hapa.

MWENYEKITI:

Kama Mheshimiwa Waziri anaweza kuteua Mtanzania yeyote wala siyo Mtanzania pengine any person, hivi TMAA ikiingia hapa kuna taabu gani jamani kuwa na rights of inspection?

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekubali kwamba tutafanya reference kwa TMAA.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kambi ya Upinzani Bungeni tulizungumzia suala la kifungu cha 25 ambacho Waziri ametolea maelezo ambayo sisi tunadhani kwamba hatujaweza kuridhika nayo. Kwa sababu kifungu cha 25 kinazuia information, ndiyo kifungu ambacho kinatengeneza ile secrecy kwamba Mikataba ni siri kati ya Serikali na mwekezaji na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama tulivyoeleza katika mchango wetu kwamba tayari Serikali yetu imeshajiunga na Exceptive Industry Transparency Initiative, kwa hiyo, tulishauri mawasilisho ya Kambi ya Upinzani na tunarejea kushauri hapa katika vifungu kwamba kifungu cha 25 kifanyiwe marekebisho kwa ajili ya kuhakikisha kwamba taarifa ambazo zitatakiwa kwa ajili ya exceptive Industry Transparency Initiative zisibanwe na kifungu hiki kwa sababu ndiyo taarifa ambazo zitatufanya tufahamu ni kiasi gani ambacho makampuni yamelipa Serikali na ni kiasi gani ambacho imepokea kutoka kwa makampuni na kuondoa hili wingu la kuwa na wasiwasi wa kutokujua ni revenue kiasi gani ambalo Taifa letu linapata kutokana na sekta ya madini.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwamba katika hiki kifungu cha 25 itafutwe njia ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali atatusaidia hapa kwa ajili ya reference ya information itakayotakiwa kwa ajili ya ITI isikataliwe kutolewa kwa sababu jinsi kilivyo hapa hatutaweza kupata information kwa kuweza kujua kwamba ni mapato gani ambayo nchi inapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

La kwanza, tulichosema na Mheshimiwa Zitto anajua, tumeongea sana kwenye Kamati ingawa kama alivyosema ni kati ya mambo ambayo pengine hatukufikia muafaka mzuri. Lakini tulisema kwanza suala lenyewe la ITI, hii tasinia ya uzinduaji, tumesema kwanza itatungiwa sheria yake ambapo moja nyingine tunaamini kwamba itatuwekea pia utaratibu wa namna ya kupata hizo information kupitia huo utaratibu. Lakini la pili tukasema kwa mazingira ya sasa tuliyonayo, kwa mfano kama mtu anataka labda taarifa kuhusu mkataba fulani, Bunge lako Tukufu hili lina utaratibu sasa hivi na Serikali mtu kama atahitaji taarifa fulani hilo tumeshasema utaratibu upo.
Lakini pili tukasema kwa huko mbele tunakokwenda, taarifa za mikataba ambayo ndio itakuwa inaingiwa, tutakuwa tunatoa baadhi ya taarifa hasa zile za msingi kwa Halmashauri katika maeneo ambayo migodi itakuwa imejengwa. Sasa sisi tukaamini kwamba katika hatua hiyo tutakuwa tumepiga hatua fulani katika kuendeleza hii concept ama hii dhana ya kuweka mambo wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tulidhani kama tulielewana katika hilo ingawa sio kwa kiwango ambacho Mheshimiwa Zitto anakielezea, kwa hivi sisi tulielezea mtazamo wetu ulivyokuwa kwamba sheria hii ya ITI itakuja, lakini pia kuna fursa nyingine ambazo sasa hivi mtu anaweza kupata kama anataka taarifa kuhusu jambo fulani na inategemea pia ni taarifa gani kwa sababu nadhani ukienda mbele pale sub-section inayofuata imeelezea taarifa zile ambazo zinaweza kupatikana na kwa namna gani. Kwa hiyo, tunaamini kwamba hatua tuliyokuwanayo haikuwa jambo baya sana kufikia hatua ambayo Mheshimiwa Zitto anasema.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tulichokuwa tunakiomba ni katika ile sub-section (2) pale anaposema: “nothing in sub-section one shall operate to prevent the disclosure of information where the disclosure is meant”. Kuna zile (a), (b), (c), (d), (e) tuongeze for the purpose of international obligations that the United Republic has committed to. Hicho ndio tulikuwa tunakiomba kitokee. Ni general statement, lakini kwa watu ambao watakuwa wanataka information for that purpose na hapo automatically ITI itakuwa imeingia. Just for the purpose of the international obligation that the United Republic has committed itself to.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Nafikiri ni vizuri kuwa waangalifu sana kwenye maeneo haya, kwa sababu mambo haya ni ya biashara ambazo hata hizo international obligations wanaotafuta informations hizo, wanaweza kukuletea madhara makubwa sana. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri disclosure, exceptions ambazo zimepatikana kwenye sub-section (2) zile zinatosha, kwa sababu hiyo international obligations zitapatikana hapo.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Moja ya mabadiliko makubwa ambayo tumeyafanya, ni kubadilisha kanuni ya kukokotoa mrahaba ambayo itatupatia mapato mengi sana kama jinsi ambavyo Mheshimiwa Cheyo alivyozungumza iwapo pia tutawataka hao wengine waweze ku-migrate.
Lakini pia tulibadilisha hivyo kwa sababu hatukuwa na control na zile gharama zilizokuwa zinaondolewa katika kupata mrahaba na sasa hivi tumekwenda kwenye gross value, lakini hatuna reference price ambayo tutakuwa tunai-refer. Madhara yake ni nini? Madhara yake ni kwamba makampuni yanaweza kuwa yanauziana kwa affiliates, kwa hiyo unaweza kukuta kampuni ambayo inachimba Tanzania ikamwuzia sister company ambayo labda yuko Australia kwa bei ndogo tofauti na bei ya soko la dunia. Kwa hiyo matokeo yake tutapata mrahaba kidogo. Ndiyo sababu hapa tunapendekeza kwamba tuwe na reference price ambayo ni published price. Anyway, we can choose any. Sisi tumependekeza London Metal Exchange, lakini you can choose any.
Kwa hiyo, kusema kwamba mnayafanyia kazi, hapana. Hili ni suala la msingi sana kwa ajili ya ku-maximize revenue yetu. Kwa hiyo nilikuwa nadhani Mheshimiwa Waziri hili mngeweza tu kulikubali ili liweze kutusaidia na iwe rahisi kwa nyinyi wenyewe pia kuweza ku-calculate huo mrahaba.

MWENYEKITI:

Lakini linatosha kwenye Kanuni, kwa sababu London Metal Exchange inaweza kubadilika ikawa Zanzibar Metal Exchange. Ndiyo, haya mambo lazima tuwe na biashara na sisi. Lazima tuwe na actual accounts zikae pale pengine Zanzibar. Imekaa vizuri, sasa ukiji-commit kwa London baada ya vizazi viwili baadhi ya sehemu za nchi yetu zinakuwa zina mvuto wa kuweka exchange, utakuwa umejibana. Kwa hiyo, ukiwa kwenye kanuni, unaweza kuweka.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kambi ya Upinzani haikuwa na nia ya kuji-commit kwa London peke yake na maelezo yako ni sahihi kabisa. Tuwe na reference published price. Wao wanaweza waka-choose any. Inaweza kuwa ni Ujiji Metal Exchange. Lakini cha msingi pawe na published price ambayo Wizara itakuwa inaitumia ili kuepuka hiyo kuuza bila kuwa na arms lengths principles. Hilo tu ndiyo ombi letu.

MWENYEKITI:

Lakini ikae wapi sasa? Tusaidie hilo, sisi ikiwa kwenye kanuni...

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mwenyekiti tuna choice mbili, ndani ya Muswada kwenye kipengele tunaweza tukasema referring to publish prices ndani ya kanuni Waziri akatengeneza kanuni ambazo na kwa sababu atakuwa na uwezo wa kuzifanyia amendments from time to time ataamua ni price ipi ambayo inatupa favour Tanzania kuliko nyingine yoyote. Lakini reference ya kwenye ile provision ingekuwa ni muhimu sana ili Waziri awe anafanya vile kwa mujibu wa Sheria. Maana yake tukiiacha hivi jinsi ilivyo tunaweza tukatumia bei za affiliets ambazo wanauziana.

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kama nilivyosema, suala hili kwanza lina maslahi kwetu, kwa sababu linatuongezea kiasi ambacho tunapata kutoka kwenye madini. Ndiyo maana tukasema tutalifanyia kazi na mahali pake ni kwenye kanuni kwa sababu hiki kitu ni variable.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaji-commit sisi kwamba tunalifanyia kazi.

MWENYEKITI:

Nadhani inatosha hiyo.

(Kifungu kilichotajwa hapo juu kilipitishwa na Kamati ya Bunge Zima bila mabadiliko yoyote)

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kifungu cha 102 kinahusiana na dispute settlements. Katika maelezo ya Kambi ya Upinzani, tulizungumzia umuhimu wa kuanzishwa kwa Tribunal, ambapo Mheshimiwa Waziri, ameji-commit katika uanzishwaji wa Tribunal, tunakubaliana na hilo kwa sababu hatuwezi kuianzisha sasa.
Lakini katika amendments ambazo zimekuja na nilikuwa nashauriana kidogo hapa na Mheshimiwa Jussa kuhusiana na Kamishna kutoa ile order yake kuwa enforced na Mahakama, ambapo wameondoa: “The order shall be enforced” na wameweka course to be enforced. Sasa tunaona kama ni kitu kile kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na-withdraw; Mheshimiwa Jussa, ameniambia kwamba Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu, ameshampatia maelezo na iko okay.
(Kifungu kilichotajwa hapo juu kilipitishwa na Kamati ya Bunge Zima bila mabadiliko yoyote)

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Spika, kuna jipya kwenye hilo hilo.

MWENYEKITI:

Nitaruhusu jipya tu.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Na nilisema wakati tunazungumzia kipengele cha 10(2) na Waziri akaahidi kwamba atatoa maelezo kwamba hivi vipengele ni viwili tofauti. In principle hivi vipengele ni redundant ukisoma 109; The Minister shall, in consultation with holders of special mining licence tume-define special mining licence ni uwekezaji wa kuanzia dola milioni 100, na tumesema kwamba watu watakaoingia MDAs ni watu wenye kuwekeza kuanzia dola milioni 100 na tayari kwenye masharti ya kupata mkataba tumeshasema kwamba Serikali itachukua hisa pale kwenye masharti ya kupata mkataba. Kwa hiyo, the whole 109 yaani 102 na 109 haviendani kabisa ndiyo maana nilikuwa nimesema mwanzo wakati wa kifungu cha 102 kwa ajili ya kuweza ku-align hizi section mbili lazima ziwe aligned kwa sababu tunazungumzia kitu kile kile, sasa Waziri akasema kwamba kuna maelezo tofauti ambayo anayo lakini hajayatoa na humbly kabisa kama Waziri ana maelezo tofauti aweze kuyatoa lakini nadhani kuna umuhimu mkubwa sana wa ku-align hivi vipengele viwili 102 na hiki kipengele cha 109.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba maelezo ya Waziri. (Makofi)

MWENYEKITI:

Mheshimiwa Kabwe Zitto, mgongano wewe unauona wapi sasa hebu tamko hizo.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kifungu cha 109 kinasema The Minister shall, in consultation with holders of special mining licence. Ukiangalia schedule of amendment tume define sasa kwa mara ya kwamba mining holder wa mining licence anapaswa kuwa na investment ya kiasi gani. Ukienda kwenye kuingia mikataba na tumesema ni dola milioni 100, ukienda kwenye kuingia mikataba tumesema kwamba uwekezaji wa dola milioni 100 and above ndiyo tulichokisema kwa hiyo, holders wa mining licence ndiyo mwenye mkataba kwa maana ya ile.
Sasa huku kifungu cha 109 tunarejea the only thing ambayo iliongezeka hapo ni a listing ambayo tunapaswa kuiweka kule wakati Serikali inafanya negotiation ya free carried interest state participation na tulisema kabisa kwamba ni state participation na listing inapaswa kuwa sehemu moja hatupaswi kuwa na vipengele viwili tofauti. Lakini Waziri alisema atatoa maelezo kwamba hii ina maana tofauti sasa nilikuwa nahitaji hiyo maana tofauti ni ipi ambayo ilikuwa maana yake Waziri hajaeleza hiyo maana tofauti.

MWENYEKITI:

Maana ya tofauti ndiyo hiyo listing.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Listing 109 inapaswa kuwa lined na 102 ili listing iwe wakati tunaingia mikataba Mwenyekiti hapa ni technically tu.

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Ambacho niliahidi ndiyo nataka nikitolee maelezo kwa Mheshimiwa Kabwe Zitto kwamba kwanza kuna vitu viwili tofauti hapa, kile kifungu cha kumi inaweza kuwa hatua za awali ambapo shughuli za biashara haijachanganya mpaka ukajisajili kwenye soko la hisa. Hapa kifungu cha 109 shughuli imeshaanza namna gani kwamba tumeshakuwa na sifa hilo la kwanza.
Lakini la pili, namuelewa Mheshimiwa Kabwe Zitto assumption anayoitumia hapa ni kwamba kila mwenye mtaji zaidi ya dola 100 lazima awe na mkataba wa MDA si lazima kwa sababu anaweza kuja mwekezaji ana fedha yake akaangalie ile package ya physical regime yetu akakubali akaridhika tu akasema mimi nimeridhika na utaratibu wenu huu wa kodi zenu wa ushuru wenu nawekeza bila kutokuhitaji mkataba maalum wa MDA. Sasa haya ndiyo maelezo ambayo nilikuwa nimeweka kama akiba ya kuja kumsaidia Mheshimiwa Kabwe Zitto ili twende kwa uelewa mmoja.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Serikali inatuchezea.

MWENYEKITI:

Wewe bila ridhaa yangu unasimama mara tatu.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Samahani Mwenyekiti, samahani, umeniruhusu sasa?

MWENYEKITI:

Sijakuruhusu.

(Kifungu kilichotajwa hapo juu kilipitishwa na Kamati ya Bunge Zima pamoja na marekebisho yake)

(Mwisho wa Mjadala)

* Sheria mpya ya madini ilipatika, ikijulikana kama sheria ya madini namba 14 ya mwaka 2010 ambapo hatimae ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 23, 2010, na kusainiwa na Rais Mei 20, 2010.
 
Bado nasubiri kuona chege akiwa kisutu!na ccm hii ya pole pole inayojinasibu kama ccm mpya ikimchukulia hatua Kali!
Ndipo nitakubali kama sasa tunaingia ukurasa mwingine.......
Vinginevyo itakua kanzu mpya ila sheikh yule yule

KWasasa ngoja niweke akiba ya maneno
 
Back
Top Bottom