kukomesha udhalilishaji wanaofanyiwa wafanyakazi wa Zanzibar walioko nje

aleesha

JF-Expert Member
Oct 17, 2016
792
1,144
Serikali ya Zanzibar SMZ imesema itaendeleza ushirikiano uliopo kati yake na mabalozi wa Tanzania waliopo nchi za kiarabu ili kuona wafanyakazi kutoka Zanzibar walioko huko wanafanya kazi katika mazingira mazuri kwa kuodokana na udhalilishaji kwa baadhi ya waajiri wao.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana Wanawake na watoto, Shadya Mohamed Suleiman katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, wakati akijibu swali la Mwakilishi nafasi za Wanawake Kisiwani Pemba Bihindi Hamad Khamis.

Bihindi alitaka kujua kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi wa wananchi wa Zanzibar wanaokwenda nchi za Kiarabu kufanyiwa vitendo cha udhalilisha na kuteswa, alihoji Serikali ya Zanzibar ina mkakati gani wa kukabiliana na tatizo hilo linawakumba wananchi wake.

Akijibu swali hilo alisema kuwa miongoni mwa njia ambazo tayari Serikali wamekuwa akizifanya juu ya kukabiliana na hali hiyo ni kuweka ushirikiano mkubwa na Balozi za Tanzania ziliopo katika nchi husika ili kuona wananchi wa Zanzibar wanapatiwa huduma nzuri kutoka kwa waajiri wao.

Alisema kuwa faida kubwa umeanza kupatikana kupitia Balozi hizo, na kudai kuwa jitihada zaidi zitafanyika ili kuona kila mzanzibar anayekwenda nchi za Kiarabu kufanya kazi anakutana na mazingira mazuri ya kazi.

Alisema kuwa Wizara yake imekuwa ikijitahidi sana katika kutoa elimu kwa wananchi hasa wanaotaka kwenda nchi za nje juu ya kufika ofisi kwake kwa lengo la kupatiwa mikatabaa maalum ya kwenda nchini humo ili kuwa njia rahisi ya kutambulika pindi wakikumbwa na matatizo.

“Nawaombeni sana wenzetu Wawakilishi nanyi mtoe elimu majimboni mwenu kwa wananchi juu ya kuwa tayari kufika ofisini kwetu kwa lengo la kujitambulisha rasm wakati wa kwenda kufanya kazi nje ya nchi, kwani njia hiyo itaweza kuwasaidia kuondoja na matatizo huko waendako, hivyo nawaombeni sana nanyi mfanye kazi hii ya kutoa elimu kwa wapiga kura wenu”alisema.

Akitoa ufafanuzi zaidi Waziri wa Wizara hiyo, Mauldine Castiko alisema kuwa wafanyakazi wengi wanaopata matatizo wakiwa nchi za kiarabu ni wale wasiofuata taratibu za kisheria katika kusafiri.

Alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakikwepa kufika ofisini kwake kwa ajili ya kupata muongozo mzuri ambao utamsaidia katika kumlinda ndani ya nchi hizo, lakini wamekuwa wakiogopa kufika hapo bila ya kuwa na sababu maalum.

Alisema kuwa jitihada kubwa wanatendelea kuzifanya kwa kutoa elimu kwa wananchi mbali mbali ili kuona wale wote wanaosafiri kwenda nje ya nchi kuondoka kisheria, pamoja na kupata ulinzi mzuri wakati wakiwa katika kazi zao nje ya nchi.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Shadya alisema kuwa hivi sasa uwezo wa Serikali ni mdogo kifedha ila hali ikiruhusu watafanya ziara maalum ya kutembelea maeneo ya kazi nje ya nchi kwa kushirikiana na kamati maalum ya baraza hilo ili kuona mwenendo mzima wa usalama wa wafanyakazi wa Zanzibar walioko huko.

Naibu huyo alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub aliyehoji kuna mpango gani wa Wizara hiyo kuondokana nchini humu wakiunga na wajumbe wa kamati ya Baraza ili kwenda nchi hizo kuona usalama wa wafanyakazi kutoka Zanzibar ulivyo nchini humo.

Zanzibar Daima
 
Back
Top Bottom