Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Ni'lenaye kisirani, mshari pia jeuri,
Ala vitu hadharani, subuhi na adhuhuri,
Na swaumu hapatani, ila apenda futari,
Jike langu mtihani, haifungi ramadhani.
Kufunga ati hafungi, ila daku atakula,
Kwa chakula hajivungi, tena hana masihala,
Vituko afanya vingi, namuachia Jaala,
Jike langu mtihani, haifungi ramadhani.
Daku hachezi mbali, yu macho alfajiri,
Linafakamia wali, viazi na kachumbari,
Kwa kula namkubali, huyu kiumbe hatari,
Jike langu mtihani, haifungi ramadhani.
Si mgonjwa yu mzima, ila kufunga hataki,
Nimeshachoka kusema, fimbo hazihesabiki,
Mahabani nimezama, siwezi kumtaliki,
Jike langu mtihani, haifungi ramadhani.
Kuswali pia haswali, atembea kichwa wazi,
Si mzuri wa kauli, kwa ndugu hata wazazi,
Ninaishi na fidhuli, na kumuacha siwezi,
Jike langu mtihani, haifungi ramadhani.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whats 0622845394 Morogoro.