Kufukuzwa wapinzani bungeni liwe somo kwa wabunge wote

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
KWA mara nyingine wawakilishi wa wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametimuliwa bungeni kutokana na utovu wa nidhamu. Hali hii imewanyima wananchi wa majimbo saba haki yao ya msingi ya kusikilizwa kero zao zilizokuwa ziwasilishwe na wawakilishi hao.

Hali hii ni ya kusikitisha sana kwa kuwa hayakuwa mategemeo ya Watanzania kuwaona wawakilishi wao wakifukuzwa katika chombo hicho chenye dhamana ya kutunga sheria, kusikiliza na kujadili matatizo ya wananchi.

Lengo la kila mbunge baada ya kuchaguliwa na wananchi ni kuwawakilisha vema wananchi wao kwa kufikisha matatizo ili yajadiliwe na hatimaye kupatiwa ufumbuzi. Ni bahati mbaya kuona baadhi ya wabunge kutumia nafasi hiyo vibaya na hatimaye kufukuzwa.

Wananchi waliwachagua wawakilishi hawa kwa kuwa waliwaamini kuwa wanaweza kuwawakilisha vizuri, lakini matokeo yake wanakwenda kinyume. Ni ukweli kuwa ili mbunge aweze kutoa kero yake na kujadiliwa ni lazima afuate taratibu na kanuni walizojiwekea.

Mbunge akiwa mkaidi, asifuate kanuni na taratibu za kibunge matokeo yake ndio haya ambapo mbunge huishia kutolewa nje hali itakayomfanya ashindwe kutetea wananchi wake. Hili linapaswa kuwa somo kwa wabunge wengine wenye hulka kama hiyo.

Ikiwa mbunge ana hoja yake imekosa nafasi au uhalali wa kuwasilishwa bungeni kiungwana, anatakiwa kufuata njia sahihi katika kudai haki yake. Na hili sio kwa wabunge wa upinzani pekee, bali hata wa chama tawala, CCM.

Pamoja na makosa yanayofanywa na wabunge katika shughuli za kila siku za bunge, adhabu zinazotolewa zinaonekana kubwa kupindukia. Kwa maoni yangu adhabu hizi zinapaswa kuangaliwa tena kulingana na kosa la mbunge husika.

Atakayefanya makosa achukuliwe hatua stahiki, kulingana na kosa lake ili kuzuia makosa kama hayo kujitokeza katika siku zijazo, lakini kwa makosa ya wabunge hawa wa upinzani Bunge lilipaswa kuwaadhibu kwa huruma ili kutowanyima wananchi wao haki ya kuwakilishwa bungeni.

Kwa mfano, wabunge kama Ester Bulaya na Tundu Lisu kupigwa marufuku kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti pamoja na Bunge lijalo ni kuwaumiza wananchi wa majimbo yao ambao naamini wana kero nyingi ambazo zingeweza kujumuishwa katika bajeti ijayo.

Wabunge wengine ambao adhabu zao kwa maoni yangu ni kubwa kuliko makosa yao ni Pauline Gekul, Godbless Lema, Zitto Kabwe na Halima Mdee ambao wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vya Bunge la Bajeti.

Naamini Bunge lingeweza kuwachukulia hatua za kinidhamu bila kuathiri uwepo wao bungeni kwa kuwa kutokuwepo kwao kunaumiza watu wengi. Wananchi hawapendi wawakilishi wao kugeuka na kuwa wanamasumbwi bungeni, lakini pia hawapendi kuona uwakilishi wao bungeni unatoweka kwa kuwa Bunge ndicho chombo pekee kinachoweza kutatua kero zao za kila siku.

Napinga Bunge kugeuzwa kijiwe cha kuvunja sheria na kanuni kwa kuwa kazi kubwa ya chombo hicho ni kutunga sheria ambazo ndizo zinazotumika kuendesha nchi. Hivyo lazima chombo hicho kiakisi dhima yake ya msingi kabisa kwa kuwa na nidhamu na kufuata sheria.

Pale inapotokea changamoto kama hizo, naliomba Bunge kuwachukulia hatua wabunge waliohusika, lakini kwa lengo la kuwabadilisha na kuwajenga wawe wabunge wema na sio kuwakomoa wananchi kwa kuwafukuza kabisa wawakilishi wao na tegemeo lao katika kutatua kero zao za kila siku.
 
Back
Top Bottom