Kucheleweshwa na mapunjo ya fidia; Malalamiko ya waathirika wa Mabomu ya Mbagala

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
1. Utangulizi
Ndugu Waandishi wa habari, tarehe 28 Januari 2023 nilitembelea Mbagala kufuatiwa na Chama chetu kupokea malalamiko kutoka kwa waathirika wa mabomu.

Kilio chao kwa muda mrefu tangu kutokea kwa milipuko ya Mabomu ya Mbagala ni kutolipwa fidia, wengine kutolipwa viwango vya haki na kuwepo kwa watu waliolipwa ambao hawakuathirika na milipuko hiyo wala sio wakaazi wa Mbagala.

Itakumbukwa kuwa athari za mabomu zilitokea tarehe 29 April 2009 kutokana na kulipuka kwa ghala la silaha katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba 671 KJ iliyopo Mbagala. Milipuko hiyo ilisababisha vifo, majeruhi, kuharibiwa kwa makazi, kuharibiwa kwa mali za watu pamoja na athari za kiafya kama vile magojwa ya kifua, upofu wa macho, Saratani na kadhalika.

Wastani wa kaya 12,000 ziliathiriwa na miIipuko hiyo katika eneo la Mbagala pekee, kutokana na athari hizi ndipo Serikali iliamua kuangalia ustawi wa watu hao kwa kuwapatia fidia, vifuta machozi na ahadi za kushughulikia matibabu.

Ndugu Waandishi wa habari, ACT Wazalendo kupitia Ofisi ya Wasemaji wa Kisekta ilifuatilia suala hili kwa kuchambua taarifa mbalimbali (orodha ya waathirika, malipo, risiti za malipo, kiasi cha bajeti kilichotumika na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali-CAG) na baadaye kutembelea baadhi ya waathirika hao, tumeshangazwa sana kuona kwa zaidi ya miaka 14 tangu kutokea kwa milipuko hiyo kuna waathirika wapatao 1, 361 hawajalipwa fidia yao stahiki. Kwa, ufupi malalamiko yao yapo kwenye maeneo yafuatayo;

• Kuwepo kwa malipo kiduchu.

• Utaratibu mbovu wa tathmini ya athari za mabomu

• Utaratibu wa malipo kutoeleweka (hakuna utaratibu unaoeleweka). Wapo waliolipwa miezi kadhaa baada ya bajeti.

• Usiri wa malipo

Ndugu Waandishi, katika ziara yangu nimeona wakaazi waliopatwa na ulemavu kutokana na athari za mabomu, nimeshuhudia makaazi yaliyoharibiwa ambayo hadi leo wamiliki wameshindwa kuyakarabati kutokana na kucheleweshewa fidia, tumekadhiwa nyaraka pamoja risiti za malipo zinazoonyesha waathirika hao kulipwa Shilingi 1,400(Shilingi elfu moja mia nne tu,) 2,700(Shilingi elfu mbili mia saba tu,) 1,900(Shilingi elfu moja mia tisa tu.)

2. Serikali inadanganya na kuwaumiza waathirika
Katika Bunge la mwaka 2022/2023 Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri, Bunge Sera na Uratibu Mhe. George Simbachawene akijibu maswali kwa niaba ya Waziri Mkuu alilidanganya Bunge kwa kusema kuwa waathirika walikuwa watu 12,647 ilihali waathirika wa mabomu hawakufika watu 10,000 hii si mara ya kwanza kwa Serikali kudanganya hata aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge) Mhe. William Lukuvi aliwahi kusema kuwa kima cha chini walicholipwa waathirika wa mabomu ni Shilingi Milioni 40 wakati uhalisia kabisa watu wamelipwa mpaka shilingi 1,400(Shilingi elfu moja mia nne tu,) 1,950(Shilingi elfu moja mia tisa na hamsini tu,) 2,700(Shilingi elfu mbili mia saba tu) na risiti za malipo hayo kiduchu zipo.

Malalamiko mengi ya wananchi yanathibitishwa na ripoti ya CAG 2012/13 iliyoonyesha Malipo ya fidia kwa waathirika wa mabomu ya Mbagala kiasi cha Shilingi Bilioni 8 hayakuwa na nyaraka muhimu za kuthibitisha kama kweli malipo hayo yalifanyika kwa walengwa. Kinyume chake adhabu hiyo wanapewa wananchi kwa kunyimwa stahiki zao, vitisho na kebehi.

Hoja nyingine ya dhihaka inayotolewa na Serikali ni kwamba, watu hawa hawapaswi kudai fidia kwa kuwa si haki yao wanachopaswa kulipwa ni kifuta machozi. Hii ni dhihaka kubwa, kwa wananchi hawa.

Mabomu haya Mbagala ni janga la kibinadamu lililosababishwa na vyombo vya Serikali hatuwezi kusababisha janga kama lile halafu Serikali ije na jibu jepesi kwamba ni hisani kutoa fidia.

Aidha, jambo baya zaidi inaumiza kuona baadhi ya viongozi wa Serikali kuanzia Halmashauri ya Temeke, Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani kutumia vitisho kushughulikia suala hili kwa kutaka kuzima vilio vya wananchi.

Tuna mfano wa hivi karibuni tulitaarifiwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya waathirika wa mabomu Mbagala kuitwa na wawakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Temeke, Mkuu wa Polisi Mkoa Maalum Temeke na watendaji wengine. Wajumbe hao waliamriwa na kuambiwa waache kabisa kujihusisha na madai yao vinginevyo hatua kali za kuwazimisha au kuwapoteza zitachukuliwa huku wakipewa karatasi za viapo kinyume na taratibu.

3. Msimamo na Kauli ya ACT Wazalendo
ACT Wazalendo tumesikitishwa sana kwa kitendo hiki kinachofanywa na Serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kwa muda wote kushindwa kuwangalia waathirika hawa, kwa kuwa tunafahamu wapo ambao tayari wamepoteza maisha kutokana na serikali kutowatazama kwa muda mrefu licha Bunge kuidhinisha bajeti jumla ya Shilingi Bilioni 17 na zilishatolewa kwa awamu takribani sita lakini hadi sasa Serikali imewaacha gizani waathrika wengine. Fedha zote hizi zimeenda wapi? Hii haikubaliki na hivyo tunaitaka Serikali ichukue hatua zifuatazo;

i. Tunamtaka Waziri Mkuu Ndg, Kassimu Majaliwa kulifuatilia na kuchukua hatua za kiuwajibikaji kwa watendaji walioshughulikia suala hili ambao kuna harufu za udanganyifu, ubaguzi na uonevu. Hili ni kundi la watu 1360, Serikali ni ya wananchi na ina wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila kuwabagua na kuona haki inatendeka.

ii. Tunatoa rai kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi maalum wa Fungu la RAS wa Dar es Salaam kuona namna wa malipo ya fidia ya Wahanga wa Mabomu ya Mbagala yaliyofanyika.

iii. TAKUKURU ilipokea malalamiko ya uwepo wa rushwa na ilianza kufuatilia suala husika ni wakati sasa ikamilishe uchunguzi wake ili kubaini wahusika na mchakato mzima wa utoaji malipo kwa fidia kwa watu wasiohusika na mabomu ya Mbagala, taarifa mbalimbali za ushahidi ikiwepo majina 1,571 yaliyolipwa mwaka 2017 na 2018 ambayo si ya wakaazi wa kata 19 zilizokumbwa na kadhia ya mabomu zilifikishwa ofisini kwao na waathirika waliopunjwa fidia.

iv. Tunawataka watumishi wa serikali kusikiliza madai ya wananchi na kutoa ufafanuzi stahiki. Hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika wa Kitengo cha Maafa wanaotoa vitisho kuwapoteza, kuondoa uhai, kuwaapisha kinyume cha sheria, kuwajeruhi kama jitihada za kuwanyamazisha viongozi wa wahanga waliopunjwa fidia ili kuwavunja moyo wanapodai haki zao.

v. Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria imulike na kuhakikisha masuala ya Maafa yanashughulikiwa kwa haki na uwazi pasina kuwabagua wananchi, katika mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Maafa ya 2015, mswada wa Sheria ya usimamizi wa maafa wa 2022 ueleze wazi tofauti ya mkono wa pole na fidia yanapotokea majanga mbalimbali ili kuepuka upenyo unaoweza kutumika kuwanyima fidia stahiki waathirika wa matatizo ambayo yanatokana na uzembe wa serikali.

Ndg. Dorothy Jonas Semu
Waziri Mkuu Kivuli - ACT Wazalendo.
01 Februari, 2023
Dar es Salaam.
 
Back
Top Bottom