Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482
Tuesday, June 21, 2016
Na VALENTINE OBARA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw Kofi Annan, amekosoa jinsi Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walivyoachwa huru wakati kesi yao ilipokuwa ikiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Kwenye mahojiano na shirika la habari la ‘Financial Times,’ Bw Annan alikosoa pia mahakama hiyo kwa kutojitahidi vilivyo kulinda mashahidi kutokana na vitisho.
“Rais na naibu wa rais ndio walikuwa washtakiwa kwa hivyo walitumia juhudi nyingi na rasilimali kujinasua kutoka kwa kesi hizo,” akasema.
ICC huwa na seli za kisasa zenye vifaa kama vile kompyuta na vyombo vya kupikia, ambako washukiwa wanaweza kuzuiliwa wakati kesi zao zinapoendelea kusikizwa.
Bw Annan ndiye aliyeongoza upatanisho kati ya aliyekuwa Waziri Mkuu Bw Raila Odinga na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, na kupelekea kuundwa kwa serikali ya mseto iliyo maarufu kama serikali ya ‘nusu mkate.’
Upatanisho huo ulifanywa kutokana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo chama cha ODM kikiongozwa na Bw Odinga kilisisitiza kilishinda kwenye uchaguzi wa urais ilhali Bw Kibaki wa chama cha PNU ndiye aliyetangazwa mshindi na iliyokuwa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), iliyosimamiwa na marehemu Bw Samuel Kivuitu.
Rais Kenyatta na Bw Ruto walikuwa miongoni mwa Wakenya sita waliofunguliwa mashtaka katika ICC baada ya wabunge kutupa nje pendekezo la kushtaki washukiwa wa ghasia hizo humu nchini.
Annan aitetea ICC
Kulingana na shirika hilo la habari lililo Uingereza, Bw Annan alitetea ICC dhidi ya malalamishi yanayotolewa na viongozi wa Afrika wanaotaka kuondoa ushirika wao katika mahakama hiyo iliyo The Hague, Uholanzi.
“Ninakumbusha Waafrika kuwa ni makosa kwao kusema viongozi wa Afrika pekee ndio hushtakiwa,” akasema, na kuongeza viongozi hao ‘hawafai kujifanya wao ndio wa kwanza’ kushtakiwa wala kuwa kuna ubaguzi mahakamani humo.
“Sisitizo limekuwa katika kulinda viongozi lakini nani atazungumza kwa niaba ya wanyonge?” akasema.
Kesi dhidi ya Bw Ruto ambaye alishtakiwa pamoja na aliyekuwa mwanahabari Joshua arap Sang, ilisitishwa Aprili baada ya majaji kuamua hapakuwa na ushahidi wa kutosha kutoka kwa upande wa mashtaka unaoongozwa na Bi Fatou Bensouda.
Mnamo Desemba 5, 2014, Bi Bensouda aliondoa mashtaka dhidi ya Rais Kenyatta na kusema sababu yake ilitokana na jinsi mashahidi walivyohongwa, kutishiwa au kuuawa ili wasishiriki kwenye kesi hiyo na baadaye Machi 2015, majaji waliamua kuisitisha.
Hata hivyo, Bi Bensouda alisema kuna uwezekano wa kesi hizo kufufuliwa katika siku za usoni ikiwa atafanikiwa kupata ushahidi mpya.
Chanzo: swahilihub.com
Swahili Villa