KISA CHA OMBAOMBA WA KIZUNGU NA MAFISADI WATANZANIA

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
Nimezaliwa na kukulia Tanzania. Nimekutana na jamii za watu mbalimbali. Moja ya jamii niliyowahi kukutana nao ni ombaomba. Kukutana na wanamama wana baba vijana na watoto wakiombaomba mijini ni jambo lililozoeleka. Nimetembea kwa muda mfupi mfupi nje ya Afrika. Nako nimekutana na ombaomba. Kwanza nilikuwa nakutana na ombaomba wa kiafrika.

Kwangu niliona kawaida. Niliona ni kawaida watu kuomba. Kisanga kikanikuta siku moja mtaani New York. Nikakutana na ombaomba kadhaa wa kizungu. Kwanza haikuingia akilini. Kadri nilivyoendelea kushangaa ikawa inakuwa wazi kuwa hao ni ombaomba. Nikasikia ukakasi! Nikaona Huruma! Nikasikia ‘bunyugwizi’.

Nikatamani kuwapatia msaada utakaowasaidia kuondoka mitaani kuombaomba. Nikiwa natafakari hilo nikarudi Hotelini kwangu na kuwasimulia wenzangu. Nikakutana na mmoja anayeshangaa kama mimi. Lakini mwenzetu mwingine akatushangaa. ‘’Kwa nini mnashangaa mzungu kuombaomba?’’ Tukagundua kuwa TUNASHANGAA KWA SABABU HATUKUZOEA! Tulijiona wajinga.

Napenda sana kulinganisha hali hiyo na hali inayoendelea hapa Tanzania.
Hata kabla ya wanasiasa kubeba agenda ya ufisadi na rushwa; wananchi walishaanza kuchoka. Rushwa imetapakaa kila mahala. Kila sehemu zinakotoka huduma muhimu. Polisi, mahakama, Hospitali na kwingineko. Tulikuwa tunaelekea kufikia mahala ambako Rushwa inakuwa MILA ya Tanzania.

Ufisadi nao ulianza kuzoeleka. Watanzania wanafahamu kuwa garama za umeme ziko juu kwa sababu ya ufisadi. Wahuni fulani wameweka ‘cha juu’ kwenye capacity Charges. Watanzania wanajua kuwa reli yetu imekuwa inang’olewa ili wenye magari ya kubeba mizigo waweze kubeba mizigo. Wanajua kuwa ni kwa sababu hiyo bidhaa nyingine ziko juu. Watanzania wanajua mengi ambayo mtu mmoja anaumiza wengi ili anufaike yeye.

Watanzania wamezoea kuambiwa huduma za jamii haziwezi kuboreshwa kutokana na mapato kidogo. Wanahimizwa na watawala kuwa waongeze uzalishaji. Mapato ya serikali yamekuwa yakiongezeka lakini wimbo kuwa bado nchi ni maskini ndiyo maana hospitali hazina madawa umeimbwa sana tena sana.

Watanzania wanaona ongezeko la idadi ya viongozi kama mawaziri, mikoa, wilaya kila mwaka. Pengine watanzania wanasema fulani kateuliwa kama fadhira kwa sababu alimsaidia kiongozi kuingia madarakani.

Watanzania wamezoea. Wamezoea kuona viongozi wa kisiasa wakiongezewa mapato lakini wafanya kazi wakisota na mapato kiduchu. Mbunge kazi yake kukaa bungeni. Analipwa sitting allowance tena hata kama kwa kuingia na kusaini kisha kumsusia Naibu spika bila ya sababu zinazoeleweka. Za nini!? Hakuna maswali.

Kilichotokea kuwapoza watanzania ni wanasiasa wa vyama vya upinzani kuyabeba na kuyatoa kwenye mikutano ya hadhara. Watanzania wakatulia. Wakawa na matumaini.

Tukafanya uchaguzi. Tukampata rais. Akaanza kuyashughulikia matatizo yaliyowakandamiza watanzania miaka yote hiyo. Watu wakaanza kurudisha matumaini. Angalau waliowaibia wanaanza kushughulikiwa. Watu waliokuwa wanakwepa kodi wanaanza kubanwa. Wamebanwa na wengine wakalipa. Watumishi serikalini wanaanza kufanya kazi kwa woga na ndio mwanzo wa kurudisha nidhamu. Wanyonge wanaanza kuwa na matumaini na kutarajia hata wale mafisadi papa watafikiwa.

Mara wanajitokeza watanzania wenzetu wanaanza kumsonga Rais. Wengine ni wanasiasa tena wa upinzani na walikuwa wakiimba wimbo huo huo wa ufisadi. Tena wanasema Rais anatekeleza sera zao. Halafu wanaanza kumgeuka. Wanasema anavunja haki za binadamu.

Kwa nini? Watu wanaohisiwa wamesimamishwa kazi ili kuchunguzwa. Wanataka awaache waendelee kuiba. Watu wanaovurunda kazi wanaondolewa kwenye nafasi za uteuzi.

Ukiangalia sana unaona ni kwa sababu watu hawa walizoea kuwaona wanyonge wengi wakipata mateso. Lakini sio wakubwa wachache ambao wanaishi maisha ya ajabu huku wanyonge wakiteseka. Wengine wanasema hakuna haja ya kuwakamata mafisadi au kuwabana wakwepa kodi. Tuweke mifumo itakayozuia ufisadi huo. Wanashindwa kuelewa kuwa mfumo upo na ukitumika utazuia ufisadi.

Sababu ya ufisadi ni kutotumika mfumo wala sio kukosekana mfumo. Mfumo ni huu unaotumika kuwabana. Wote wanaoshangaa hatua zinazochukuliwa na Rais na kumlaumu wanahitaji kujua kuwa shida yao ni moja tu: KWA SABABU HAWAKUZOEA! Kuzoea kuona mafisadi papa wakichukuliwa hatua.

Kuzoea kuona wafanyabiashara wakubwa wanabanwa wanapokwepa kodi. Kuzoea kuona waziri anavuruga anatimuliwa. Mfumo wowote kama hautasimamiwa hakutakuwa na mabadiliko. Tukubaliane. Sheria itendewe kazi na tufumbe macho kama hatuwezi kuvumilia kuona ikifanya kazi.
 
Back
Top Bottom