Kisa cha muuza sambusa

Zogoo da khama

JF-Expert Member
May 20, 2013
623
582
Palikuwapo na muuza sambusa mashuhuri jijini Arusha. Mgahawa wake ulipakana na kampuni moja kubwa. Kutoka na ladha murua ya sambusa zake, wafanyakazi wengi, kama si wote katika kampuni anayopakana nayo, kila siku walifika mgahawani pake kununua sambusa.

Siku moja, meneja wa kampuni naye alifika mgahawani kununua sambusa. Akiwa anaendelea kutafuna sambusa yake, alimuuliza muuza sambusa, ambaye ndiye mmiliki wa mgahawa, "Bwana Sajam, mbali ya kuonesha umahiri katika upishi, pia umeshihirisha uhodari wako katika utawala hata ukaweza kuukuza na kuuboresha mgahawa wako kiasi hiki. Hivi, hauoni kama unapoteza muda wako mwingi na kipaji chako kwenye kijibiashara kidogo cha kuuza sambusa? Hebu fikiri, kama ungekuwa umeajiriwa kwenye kampuni kubwa kama mimi, saa hizi ungekuwa meneja mwenye mafanikio makubwa mno."

Muuza sambusa alitabasamu huku akiendelea kupanga sambusa zake, kisha akasema, "Mimi nafikiri biashara yangu ni bora kuliko kazi yako. Unajua kwanini? Miaka kumi iliyopita, nilianza biashara ya kuuza sambusa kwenye kikapu kidogo kwa kuwazungukia wateja. Kipindi hicho nawe ndiyo ulikuwa umeajiriwa rasmi. Wakati huo mimi nilikuwa nikijipatia shilingi elfu moja kwa mwezi mzima, na wewe ulikuwa ukilipwa shilingi elfu kumi kila mwisho wa mwezi. Ndani ya miaka hii kumi, sote tumepitia mabadiliko makubwa; mimi nimeondokea kuwa muuza sambusa mashuhuri ninayemiliki mgahawa wangu, ilhali wewe umepanda cheo na kuwa meneja. Kwa sasa, wewe unalipwa milioni moja kwa mwezi, nami pato langu kwa mwezi ni hiyohiyo milioni moja na wakati mwingine napata juu ya hapo."

Meneja akiwa hajaiona tofauti ya kipato baina yao hata muuza sambusa yule akasema biashara yake ni bora zaidi, bwana Sajam aliendelea kufafanua:

"Hebu itazame kesho ya wanangu halafu ulinganishe na ya wanao - nilianza maisha kwa adha ya mtaji mdogo wa biashara. Lakini, mwanangu hatokuja kupitia hayo tena. Ikifika wakati mwanangu akaja kuichukua na kuisimamia biashara hii, hatohitaji kuanza alifu kwa kijiti. Ataendeleza mgahawa na kuuboresha zaidi. Tofauti na wewe, ambapo mafanikio ya kampuni unayofanya kazi, yatakwenda kwa watoto wa bosi wako, na si kwa wanao. Na kamwe, hautoweza kumpa mwanao hicho cheo cha umeneja akiendeleze, kama atataka itambidi naye aanzie sifuri ili kuitafuta miamoja. Kama ambavyo wewe ulitaabika kwa miaka kumi kufikia cheo hicho, mwanao naye atahitaji kutaabika miaka mingi kutafuta nafasi kama hiyo. Sasa hebu tazama, wakati mwanangu anaanzia hapa nilipoifikisha biashara yangu, mwanao wewe atakuwa ndo kwanza anaanzia safari ya sifuri kuyatufa mafanikio. Na mpaka akafikie kuwa meneja, atamkuta mwanangu akiwa mbali mno. Haya, niambie nani anapoteza muda na kipaji chake baina yetu?"

Meneja alilipia sambusa aliyokula, na kuondoka bila kuaga.
 
Back
Top Bottom