UGONJWA wa kipindupindu umeibuka katika Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam na mgonjwa mmoja kulazwa katika Zahanati ya Vingunguti.
Aidha, limetengwa eneo maalum kwa ajili ya kupokea na kuhudumia wagonjwa hao kama wataendelea kuongezeka. Akizungumza jana na Nipashe, Kaimu Meya wa Ilala, Omari Kumbilamoto, alisema kutokana na kugundulika kwa mgonjwa huo wametenga eneo maalum la kuhudumia wagonjwa iwapo wataongezeka.
Alisema hadi sasa wamebaini kuwa chanzo cha ugonjwa huo ni baadhi ya wananchi kutiririsha majitaka ambayo yanakwenda kwenye maji yanayotumiwa na wananchi. Kumbilamoto ambaye pia ni diwani wa Vingunguti, alisema hatua za awali zilizochukuliwa ni kunyunyiza dawa kwenye maeneo ya maji machafu yaliyotuama ikiwamo kuchukua hatua kwa wanaotiririsha maji hayo kutoka kwenye vyoo.
Aidha, alisema wanawaelimisha wananchi kunyunyiza dawa, kuchemsha maji, kunawa kwa maji ya moto kabla ya kula na kuhakikisha usafi wa mazingira kila wakati. Kwa mujibu wa Meya huyo, kwenye maeneo ya masoko wamewaelekeza wahusika kuhakikisha takataka hazikai kwa muda mrefu na usafi wa wafanyabiashara na watumiaji wengine. "Tulichobaini ni kwamba wakati wa mvua hizi, baadhi ya wananchi walikuwa wanazibua vyoo vyao na kutiririsha maji taka ovyo, hii inasababishwa na ukweli kuwa VingungutI
"Tumechukua hatua kwa watu wanne tuliowakamata kwa kuwapiga faini ya Sh. 30,000 kwa kosa la kutiririsha majitaka, na wengine walikamatwa na kuwekwa ofisi za kata na kuachiwa," alibainisha.
Alisema baada ya kukamatwa na kuachiwa walipewa masharti ikiwamo kuhakikisha wanarekebisha mifumo ya majitaka. Kuhusu athari za mafuriko, alisema baadhi ya maeneo ya manispaa hiyo yameathiriwa na mvua hiyo ikiwamo eneo la Mtambani na Miembeni, nyumba 12 kujaa maji.