Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 43,037
- 34,741
MIAKA 50 iliyopita lilikuwa ni jambo lisilofikirika au kubashirika kwamba siku moja nchi za Ulaya Magharibi zingebembeleza ziokolewe kiuchumi na China, lakini ndivyo ilivyotokea karibuni.
Nina hakika wasomaji wangu wanaofuatilia kwa karibu habari za mtikisiko wa Eurobarani Ulaya ambao unakaribia kuleta anguko la pili la uchumi wa dunia, walisisimshwa na kitendo cha nchi za Ulaya Magharibi kuibembeleza China izidhamini kifedha.
Nasema miaka 50 iliyopita, hiki kingekuwa kituko cha aina yake kwa China ya Kikomunisti kuombwa iiokoe Ulaya Magharibi kiuchumi, lakini si zama hizi na wala si China hii ya sasa ambayo kwa kipindi cha miaka 33 iliyopita imefanikiwa kuimarisha uchumi wake hadi kushika nafasi ya pili duniani nyuma ya Marekani.
Takwimu zinaonyesha kwamba akiba ya fedha za kigeni ya China sasa imefikia dola trilioni 2.3. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha pia kwamba China inashikilia nafasi ya kwanza duniani ya kuwa muuzaji mkubwa wa bidhaa nje ya nchi (export) na nafasi ya pili duniani katika kuagiza bidhaa za nje (import).
Takwimu pia zinaonyesha kwamba China ya sasa inashika nafasi ya kwanza duniani kwa kuwa na uchumi unaokua kwa kasi (asilimia 10 kwa mwaka) kuliko nchi nyingine zote duniani.
Takwimu hizi ndizo zinazowatoa jasho wachumi mbalimbali duniani wakiitafakari kasi ya maendeleo ya kiuchumi ya
China baada ya kulegeza masharti ya biashara mwaka 1978; yaani miaka 33 iliyopita.
Wanajiuliza: Kwa nini China imefanikiwa wakati nchi nyingine duniani zilizolegeza pia masharti ya biashara kwa muda mrefu, bado zinasuasua (mfanoTanzania)?
Kuna wanaodai kwamba mambo yanakuwa rahisi China kwa sababu ya nguvu-kazi ya bei nafuu (cheap labour); lakini hoja hiyo inasambaratishwa na ukweli kwamba hata India kuna nguvu-kazi ya bei rahisi, lakini kasi ya kukua kwa uchumi wake haifui dafu kwa ile ya China.
Vyovyote vile; sababu inayokubaliwa angalau na wengi, ni kwamba, tofauti na nchi nyingine zilizolegeza masharti ya biashara, viongozi wa China ni makini, wanajituma na wamepania kuifanya nchi yao kuwa na uchumi imara kabisa duniani.
Kwa ufupi, unaweza kusema kwamba China ina viongozi bora (competent leaders) – viongozi wasio na mzaha na watendaji wababaishaji au mafisadi.
Kwa maneno mengine, kama siri ya maguvu ya ajabu ya Samson wa Biblia ilikuwa kwenye nywele zake, siri ya kukua
kwa kasi kwa uchumi wa China imo katika ubora wa viongozi wake.
Sasa, kama kusimamia vyema utendaji kazi, kuwaadabisha watendaji wababaishaji na kuwaadhibu wakwazaji maendeleo na mafisadi, ni udikteta, basi, kwangu mimi, udikteta wa namna hiyo ni "udikteta poa" (benevolent), na unafaa barani Afrika; hususan katika Tanzania ambako ubabaishaji na ufisadi vimekithiri.
Chukulia, kwa mfano, suala la ufisadi. Katika China hakuna suluhu na mafisadi. Sote tunakumbuka, kwa mfano, jinsi nchi hiyo ilivyomfunga jela miaka 18 kiongozi maarufu wa chama, Chen Liangyu, baada ya kumtia hatiani mwaka 2008 kwa kosa la ku-fisadi fedha za Mfuko wa Jamii.
Hapa Tanzania hali ni tofauti. Viongozi wa chama tawala CCM wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, bado wanatamba na vyeo vyao mpaka sasa.
Mfano mwingine wa China ni ule wa Julai 2010 ilipomhukumu kifo (na akauawa) ofisa mwandamizi wa jiji la Chongqing kwa tuhuma za ufisadi na ubakaji.
Kwa mtazamo wangu, kama hatua kama hizo za China zinaweza kutafsiriwa kuwa ni za kidikteta, basi, ni ‘udikteta poa'. Udikteta wa sampuli hiyo unaweza kusaidia kuzinusuru baadhi ya nchi za Afrika (ikiwemo Tanzania) ambako viongozi badala ya kusimamia sera za serikali za kujenga uchumi imara, wao wako bize kujitafutia utajiri kwa njia za kifisadi.
Lakini jambo jingine kubwa lililoisaidia China ni uamuzi wake wa kuwapeleka watu wake wengi katika mataifa yaliyoendelea duniani kiviwanda (Marekani na Ulaya) ili kuchota utaalamu na teknolojia ya kisasa; ikibidi hata kwa njia za ushushushu.
Njia hii iliiwezesha China kupiga hatua haraka mno za kuanzisha viwanda vingi vyenye kutumia teknolojia ya kisasa, na ndiyo maana imeweza sasa kushika nafasi ya kwanza duniani kwa kuuza bidhaa nyingi nje. Inaaminika kwamba, kwa sasa, ni bidhaa chache mno duniani ambazo China haiwezi kuzitengeneza.
Ndugu zangu, katika nchi zetu hizi za maeneo ya Afrika Mashariki, naiona nchi ya Rwanda ikifuata nyayo za China za kuhakikisha inakuwa na viongozi wenye dhamira ya kweli ya kuiendeleza nchi yao kwa kasi.
Sitashangaa miaka 30 ijayo Rwanda ikawa na uchumi ulio imara kushinda nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; au hata Afrika ya Kusini mwa jangwa la Sahara.
Wako wanaomwita Rais Kagame kuwa ni dikteta, na yawezekana wana hoja zao za kimsingi; lakini kwangu mimi nikiangalia maendeleo ambayo kiongozi huyo ameiletea Rwanda katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, naweza kuukubali udikteta wake kuwa ni ‘poa' kama ule wa China; jambo ambalo ni muhimu katika kujenga nidhamu ya uchapaji kazi na katika kupambana na ufisadi.
Wakati ambapo China iliwatuma watu wake kwenda Marekani na Ulaya Magharibi ‘kuiba' teknolojia ya kisasa ili kufanikisha mapinduzi yake ya viwanda, Rwanda nayo ilianza kwa kuwashawishi wananchi wake waliokuwa wakifanya kazi za kitaaluma Ughaibuni, kurejea nyumbani kuijenga nchi yao.
Ukilichunguza baraza la mawaziri la Rwanda, utagundua kwamba baadhi ni vijana wanataaluma waliokuwa wakifanya kazi nyeti sehemu mbalimbali duniani. Rais Kagame aliwatafuta kote walipokuwa duniani na kuwashawishi kurejea nyumbani kumsaidia kujenga nchi yao.
Habari za kuaminika zinasema kwamba, Rais Kagame, au tuseme Serikali ya Rwanda, huwa inafuatilia kwa karibu wananchi wake wote waliopo Ughaibuni wanaofanya kazi nyeti za kitaaluma huko.
Nimetaarifiwa kwamba wanayo data base inayoonyesha wataalamu hao ni wangapi, wako nchi gani na wanafanya nini, na kwamba kila inapobainika kwamba mmojawao anahitajika kurejea Rwanda ‘kuokoa jahazi', Rais Kagame anamshawishi kurudi, na kwa uzalendo wao, mara nyingi huwa wanarudi.
Hapa kwetu Tanzania, kitu kama hicho hakipo kabisa. Licha ya kwamba sote tunafahamu kuwa tuna Watanzania wenye bongo zinazochemka kweli kweli ambao wanafanya kazi nyeti za kitaaluma huko Ughaibuni (na hapa nazungumzia nje ya bara la Afrika, na si Botswana au Namibia ambako wamejaa), bado serikali yetu haijaandaadata base yao.
Na si tu kwamba hatuna data base inaohusu wenzetu hao walioko Ughaibuni, lakini pia hatuna hata fikra za namna tunavyoweza kuwatumia kuiendeleza nchi yetu kiviwanda (nilisema bila viwanda hakuna maendeleo); hasa katika sekta nyeti ambazo tu dhaifu kitaalamu.
Labda nitoe mfano. Hivi karibuni Serikali imewapa Wachina mradi wa chuma wa Liganga. Nijuavyo, Tanzania hatuna wataalamu wa kiwango cha juu na wa kutosha wa fani ya vyuma (metallurgy), na hivyo uwezekano wa "kulizwa" na Wachina katika mradi huo ni mkubwa.
Ingekuwa kama ni Rwanda, nina hakika Kagame angewatafuta wananchi wake wenye utaalamu huo popote pale walipo duniani, na kuwashawishi warejee nyumbani kufanya kazi bega kwa bega na Wachina hao ili kuepusha uwezekano wa "kulizwa" na wawekezaji hao wa kigeni.
Katika fani hiyo ya vyuma, ambayo kimsingi ndiyo chachu ya mapinduzi ya viwanda popote pale duniani; angalau namfahamu mtaalamu mmoja Mtanzania ambaye anafanya kazi katika sekta hiyo nchini Sweden kwa zaidi ya miaka 18 sasa.
Huyu bwana, Dk. Mselly Nzotta, ambaye ni bingwa katika fani ya upembuzi wa chuma, alisomeshwa na Serikali ya Nyerere ili baadaye yeye na wenzake waisimamie sekta hiyo hapa nchini. Alipofuzu na kurejea nchini, watawala waliofuatia hawakuona umuhimu wake, na hivyo akarejea Ulaya ambako aliajiriwa mara moja, na baadaye akazidi kujiendeleza katika fani hiyo.
Nina hakika katika suala hilo la chuma cha Liganga, hata kuombwa tu ushauri na Serikali ya Tanzania wakati wa majadiliano na wawekezaji hao wa Kichina, hakuombwa, na siamini kama NDC yenyewe ina wataalamu waliobobea katika fani hiyo.
Kwa hiyo, inashangaza kwamba mtaalamu wa Kitanzania ambaye Sweden inamthamini na kumuajiri katika nafasi nyeti, nyumbani kwake Tanzania hathaminiwi; hata katika kuombwa ushauri tu (tena wa bure)!
Na hii ndugu zangu, ni moja ya tofauti kubwa kati yetu na Rwanda! Ingekuwa ni Rwanda, huyu bwana angesharejeshwa nyumbani kuisaidia nchi ili "isilizwe" na Wachina.
Na kusema kweli, sina hakika kama hata Serikali yenyewe inajua kwamba inaye Mtanzania aliyebobea katika fani hiyo ya vyuma huko Sweden; maana, kama nilivyosema mwanzo, hatuna hata data base ya bongo hizo za Kitanzania zilizopo Ughaibuni.
Ndugu zangu, katika zama hizi ambapo mataifa mengi duniani sasa huwatumia wananchi wake walioko nje ya nchi kufanya ushushushu wa kuiba teknolojia za kisasa na kuzipeleka nyumbani, nadiriki kusema kwamba kushindwa kuzitumia bongo hizi za Watanzania wenzetu waliopo Ughaibuni, ni udhaifu mkubwa wa kiuongozi.
Rais wetu, Jakaya Kikwete, amekuwa akisafiri sana Ughaibuni kushinda rais yeyote katika historia ya Tanzania. Kila akiwa huko amekuwa akijitahidi kuwahimiza Watanzania kuwekeza nyumbani, lakini hakuna hata mara moja ambapo
amepata kusaka Ughaibuni vipaji vya Kitanzania vilivyoko huko na kuwashawishi warejee nyumbani kumsaidia kazi!
Mara nyingi amekuwa akizungumza nao huko Ughaibuni juu ya mambo ambayo sio ya msingi sana katika suala zima la kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
Safari yake ya mwisho ya Marekani, kwa mfano, alikutana na Watanzania wanaoishi huko; lakini aliishia kuwapasha juu ya mikopo ya nyumba inayotolewa na NSSF, na kuwahimiza wajenge nyumba za kisasa za kuishi nyumbani (Tanzania)!
Hivi kweli Mtanzania aliyeishi Marekani miaka 20 akifanya kazi kama mtaalamu wa teknolojia ya kisasa ya mawasiliano kule Silicon Valley, "mchango" pekee anaoweza kutoa kwa nchi yake ya asili (Tanzania), ni kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi nyumbani Tanzania? Lakini huo ndio uliokuwa wito wa Rais Kikwete kwa Watanzania wale katika safari yake ya mwisho nchini Marekani!
Ndugu zangu, nihitimishe hivi: Tuna Watanzania wengi wenye bongo zinazochemka kweli kweli walioajiriwa huko Ughaibuni kwa miaka mingi tu wakifanya kazi katika nafasi nyeti, lakini bado hatuna data base yao, na hivyo hatujawahi kuwatumia.
Tunapaswa kurekebisha hilo. Kama kweli watawala wetu wana nia ya kweli ya kuiendeleza nchi yetu kwa kasi, basi, wakati umefika wa kufuata nyayo za Rwanda kwa kuwashawishi wenzetu hao walioko Ughaibuni, kurejea nyumbani na kutusaidia katika zile sekta ambazo kitaalamu bado tu duni mno.
Vinginevyo, tutaishia tu "kulizwa" na Wachina kama itakavyokuwa kwenye mradi huo tuliowakabidhi wa chuma cha Liganga.
Source: Raia mwema