Kijue kitabu cha Zaburi

Kijue kitabu cha Zaburi

hamis77

JF-Expert Member
Joined
Aug 20, 2013
Posts
18,253
Reaction score
26,641
Neno “Zaburi” linatokana na lugha ya Kiebrania ya kale, ambapo huitwa "Tehillim", likiwa na maana ya “sifa” au “nyimbo za sifa kwa Mungu.” Katika tafsiri ya Kigiriki, Zaburi huitwa "Psalmos", neno linalomaanisha “wimbo unaopigwa kwa ala ya muziki” — kama vile kinubi, zeze, au kinanda cha zamani (lyre).

Kwa hiyo, kabla hujaifikiria Zaburi kama tu sura kwenye Biblia, tambua kuwa kiasili ni nyimbo zilizojaa hisia, dua, maungamo, na utukufu kwa Mungu, zikipigwa na kuimbwa hadharani mbele za watu.

Kwa muktadha wa Biblia, Zaburi ni kitabu cha Biblia chenye sura 150, kikiwa miongoni mwa vitabu vya kale zaidi vyenye maombi ya ndani kabisa ya moyo wa mwanadamu kwa Muumba wake. Kimejaa nyimbo, sala, manung’uniko, sifa, na hata maswali magumu kwa Mungu — kikiwakilisha hali halisi ya maisha ya kiroho na kimwili ya waandishi wake.


WAISLAMU NA NENO “ZABURI”

Ukitaka kumtibua kwa upole ndugu yako Mwislamu, muulize hivi:
“Unaposema kwamba Mungu aliteremsha Zaburi kwa Daudi, unaweza kueleza Zaburi ni nini hasa?”
Ni wengi wasiojua kuwa si tu jina la kitabu, bali ni mkusanyiko wa nyimbo halisi, nyimbo zilizojaa hisia na zilipigwa kwa ala za muziki. Na Biblia yetu inazo zote — nyimbo 150!

Uislamu unakiri kuwepo kwa Zaburi kama “kitabu cha mbinguni” lakini haukuhifadhi nyimbo hizo. Lakini kwa sisi Wakristo, tuna Zaburi zote kwa maandishi, neno kwa neno, na tunazisoma kila siku — ni hazina ya ajabu!

JE, NI DAUDI PEKEE ALIYEANDIKA ZABURI?

Mara nyingi jina la Daudi hujitokeza haraka unaposema “Zaburi.” Ni kweli, Daudi alikuwa mtunga zaburi mkuu, lakini hakuwa pekee. Katika sura 150, yeye ameandika takribani 73 — karibu nusu. Lakini kuna waandishi wengine waliochangia pia, kutoka vizazi mbalimbali, walioguswa na Roho wa Mungu kwa nyakati tofauti.

Hawa ndio waandishi wakuu waliothibitika katika kitabu cha Zaburi:

1. Daudi – Mfalme, mpiganaji, mwanamuziki, na mtu aliyeitwa “mtu wa moyo wa Mungu.” Aliandika Zaburi nyingi zaidi (angalia: Zaburi 3, 23, 51, 103 n.k). Maisha yake ya milima na mabonde yalikuwa chanzo cha maombi yenye nguvu:

"Mimi ni maskini na mnyonge; Bwana hunifikiria; Wewe u msaada wangu..." (Zaburi 40:17)


2. Asafu – Mwanamuziki wa Walawi, aliyeongoza ibada za muziki hekaluni. Aliandika Zaburi 12, miongoni mwao:

"Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, kwao waliwafuatao moyo safi." (Zaburi 73:1)


3. Wana wa Kora – Kikundi cha Walawi waliowekwa kwa kazi ya uimbaji. Walihusika kuandika Zaburi kama:

"Kama vile ayala anavyopenda vijito vya maji, vivyo hivyo nafsi yangu yakutamani, Ee Mungu." (Zaburi 42:1)


4. Mose – Mtumishi wa Mungu aliyeandika Zaburi ya zamani zaidi:

"Bwana, wewe umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi." (Zaburi 90:1)


5. Sulemani – Mwana wa Daudi na mfalme mwenye hekima. Aliandika Zaburi 72 na 127, kama hii:

"Isipokuwa Bwana aijenge nyumba, waijengao wafanya kazi bure..." (Zaburi 127:1)


6. Ethan Mwezrahi – Mwanamuziki na mwalimu wa hekalu, aliyeandika Zaburi 89.



ZABURI ZILIZOANDIKWA BAADAYE (ENZI ZA UHAMISHO NA BAADA YAKE)

Baadhi ya Zaburi zinaonyesha wazi ziliandikwa wakati wa huzuni kuu, hasa kipindi cha uhamisho Babeli (586–538 KK). Kwa mfano:

Zaburi 137:

"Kando ya mito ya Babeli, huko tuliketi, tukalia..."


Na nyingine zilitungwa baada ya Wayahudi kurejea toka Babeli, kama:

Zaburi 126:

"Bwana alipowarudisha mateka wa Sayuni, tulikuwa kama waotao ndoto."


Zaburi si jina la kiitikadi, bali ni urithi wa kihistoria, kiroho, na kisanaa ulioshikwa kwa mkono wa watu wa Mungu. Si kila atajaye jina Zaburi anaelewa kina chake.

Kwa hiyo, ukikutana na mtu anayetaja Zaburi kwa mdomo tu, lakini hajawahi kusoma hata Zaburi ya 23 au 51 — muulize kwa upole:
“Je, umewahi kuisikia Zaburi inayosema ‘Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu?’”

Labda hapo ndipo safari ya kweli ya kiroho itaanza kwake...

Binafsi Nina Zaburi ambazo nazitumia kwa maombi ya kila aina ya shida au changamoto inayonikabili, nitaleta Uzi wa Siri ya Zaburi ambayo wengi hawaijui ....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom