Influenza said:
Kifungua kinywa kinachozungumziwa hapa ni kile ambacho kitaweza kukupa nishati lishe (kalori ) yenye theluthi moja ya nishati lishe inayotakiwa kwa siku ile.
Anza kunywa uji wa dona asubuhi au kunywa uji wa mtama au ngano ambayo haikukobolewa sana, kula magimbi, Muhogo uliochemshwa, au kama kuna viazi vitamu vile vyenye rangi ya njano hapo mambo ndipo yatakapo noga.
Ukipata kipande cha tunda la msimu kama embe, nanasi, tikiti maji, chungwa. Kwa wale wanaoishi ukanda wa pwani, uji kwa mafenesi ni chakula kizuri sana kwa mtoto aendae shuleni asubuhi au baba au mama aendae shambani au kwenye ajira yoyote ile.
Ukipata karanga kiasi kidogo tu, mlo wa asubuhi wenye mkusanyiko huo ndio mlo unakubalika kiafya. Achana na maandazi, chapati au vitumbua asubuhi vilivyojaa mafuta, vyakula kama hivyo hunenepesha mwili na sio vyakula asilia.
Vyakula asilia nilivyovianisha ndivyo vyenye mlomakapi (fibre) Vyakula vyenye mlomakapi haviyeyushwi na kusharabiwa na mwili, bali vinasaidia kusafisha mabaki ya sumu mbali mbali (free radicals) na pia husaidia anayekula vyakula vyenye mlo makapi, mtu huyo asilani katika uhai wake akiendelea kwa hatua hizo hataongezeka uzito kiholela, na pia atajiepusha na kupata saratani ya utumbo mpana (colon cancer) na ataweza kujikinga asipate ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu litapungua au kutoweka.
Tuwe na saa maalum za kula chakula cha jioni ili tuweze kupata mlo wa asubuhi wa kufungua kinywa wenye theluthi mbili za kalori zote zinazo hitajika kwa siku moja.
Watoto walale mapema wapigishwe mswaki kabla ya kulala. Asubuhi kunywa maji kama glasi mbili kuna saidia kusafisha tumbo. Fanya zoezi kidogo pata mlo wa asubuhi wenye moto kama uji na viazi vya kuchemsha magimbi na muhogo kama ipo matunda kidogo na karanga kama zipo.
Mlo huo pia ni mzuri kwa mtoto anayekwenda shule. Nishati yetu inatokana na chakula. Seli zako katika ubongo hazina sukari ya kutosha wakati wa asubuhi na huna hifadhi ya nishati lishe. Watu wengi huchoka kwa sababu hawali kifungua kinywa asubuhi. Wanakacha kifungua kinywa.