Kassim Majaliwa baki hapohapo, usibadilike

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MICHEZO ya nchi nzima imekwama. Hakuna mchezo ambao nchi inaweza kusimama mbele ya hadhira na kujitamba nao. Si mpira wa miguu, si ngumi, si riadha, si judo, si bao, kila mchezo tumekwama.

Ni janga la kitaifa kuona michezo imekwama kwenye kipindi ambacho michezo imekuwa ajira na sio sehemu ya burudani kama zamani.

Raha iliyoje tumekusanya kundi kubwa la vijana mitaani wenye vipaji, lakini kutokana na kutokuifanya michezo yetu kuwa ajira ndio kunakofanya vijana wapotelee huko waliko.

Jikumbushe tu mtaani kwako kuna vijana wangapi wenye vipaji ambao unaona kabisa kama juhudi zikifanyika wanaweza kufika mbali kujinufaisha wao na kulitangaza taifa? Jiulize tu. Najua wako wengi, lakini unafanyaje sasa zaidi ya kuishia kuwatazama na kuwapa moyo.

Ukimuulizia kila kijana mmoja atakupa majibu yake ya kusikitisha. Mwisho wa vipaji hivyo ni kuingia kwenye makundi mabaya ya utumiaji madawa ya kulevya. Huwezi kuwalaumu wamekwenda huko ni kutokana na kutokuwepo kwa mrejesho sahihi ulio ndani ya michezo ambao ungemvutia hata mzazi kumpelekea mwanae kwenye shule husika ya kipaji cha mtoto wake.

Ni ngumu kwa mzazi wa Kitanzania kutoa fedha kumnunulia mtoto wake kiatu cha mpira au ‘glovu’ za kupigana na akaacha kumnunulia mahitaji yake mengine. Ni ngumu hii.

Ndio maana wazazi wengi wanaamini maisha mazuri kwa watoto ni kusoma amalize mpaka vyuo, kitu ambacho wakati mwingine si sahihi.

Michezo kwetu ni burudani ndio maana vijana wengi wanaenda sehemu za michezo wanapomaliza kila kitu.

Nchi za Afrika Magharibi, zimegeuza michezo ajira na inayoweza kubadirisha kila kitu ndani ya familia ndio maana ni rahisi mzazi kuuza hata nyumba yake mwanae aende sehemu za majaribio.

Mzazi gani wa Kitanzania anaweza kuuza hata baiskeli yake ili kupata fedha ya kumnunulia mwanae vifaa vya michezo? Tusidanganyane. Hakuna!

Kama nchi ndio tumefikia hapa. Tumebaki kubangaiza na kufanya kila mchezo tunaokwenda kushiriki kugeuka wasindikizaji badala ya washindani.

Siwalaumu wachezaji wetu wanapokuwa kwenye michezo yao. Nafahamu mazingira wanayokutana nayo. Hawakuandaliwa kushinda na wanacheza kama sehemu ya kujifurahisha na kufahamiana na watu wa mataifa mengine.

Ndio maana kama nchi inachukua muda mrefu kushuhudia tena mchezaji anayeweza kuitangaza nchi kupitia michezo. Imechukua miaka 44 Tanzania kupata mcheza soka aliyeingia katika wachezaji 11 wa Afrika. Alikuwa Maulid Dilunga, miaka hiyo, nchi ikasota sana na sasa amekuja Mbwana Samatta. Ni aibu.

Tazama riadha, tangu Filbert Bayi, aliposhinda medali ya dhahabu mwaka 1974, nchi imesimama tena na mpaka sasa haina mkimbiaji mwingine ambaye amefanya vizuri kama Bayi.

Ngumi ni kama zimezaliwa kwenye ukoo wa Matumla. Tangu Rashid Matumla ‘Snake Man’ alipofanya vizuri katikati ya miaka 1990, hakuna bondia mwingine aliyeweza kuvaa vyema viatu vyake na kuipeperusha bendera ya nchi.

Kila bondia anayeondoka nchini hivi sasa kwenda nje kunakuwa na asilimia kubwa ya kushindwa kuliko kushinda.

Michezo yetu imefikia katika mtiririko wa aina hii. Haishangazi kuona michezo inazungumzika zaidi kwenye historia na sio wakati uliopo.

Huwezi kuzungumzia raidha bila kulitaja jina la Bayi, ni kama kwenye ngumi bila kuacha kumtaja Matumla, bado hujazungumza ngumi.

Inachosha kijana wa miaka 20 leo hii, akianza kusimuliwa stori za zaidi ya miaka 20 iliyopita muda ambao hakuwa amezaliwa.

Ilihitaji kijana wa miaka hiyo anazaliwa na kupata akili yake anajionea mambo yakifanyika viwanjani na sio kupewa mambo ya historia tena. Inachosha hali hii.

Lakini mazungumzo ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, katikati ya wiki iliyopita yatakuwa na tija kama yatafanyiwa kazi vyema.

Majaliwa, alizungumza na viongozi wa michezo yote nchini kwa ajili ya kupata mwanga, ambao leo hii haupo na kufanya nchi ijikite kuzungumza historia zaidi.

Mazungumzo hayo yaliyofanyika ndani ya Ukumbi wa mikutano wa Uwanja Taifa, jijini Dar es Salaam, ulikutanisha wadau, viongozi hao pamoja nasi (Waandishi wa Habari).

Majaliwa, alizungumza vitu vingi ndani ya ukumbi, ilihitaji umakini wa hali ya juu kuweza kumsikiliza na kumuelewa. Aliuzungumzia kila mchezo kwa anavyoufahamu.

Moja ya mambo yaliyonishitua ni robo tatu ya viongozi wa michezo kusema hawana ofisi za kufanyia shughuli zao.

Hii ilinishitua sana na kujisemea kimoyo moyo tuna safari ndefu ambayo tuko nayo inayoweza kutufanya kila mwaka tutoe mchezaji mmoja ambaye atatutangaza kimataifa.

Kama kiongozi anasema hana ofisi, unadhani mchezaji husika anajisikiaje akiona kiongozi wake anakiri kuwa hawana ofisi? Tuna safari ndefu sana!

Lakini kupitia kwa Majaliwa, kila kitu kitakwenda vizuri na baada ya muda tutaanza kuzungumza lugha nyingine kwenye michezo.

Sera ya michezo tuliyonayo nchini ni ya mwaka 1995. Ni sera ambayo imeshindwa kutuvusha hapa tulipokwamia ndio maana Majaliwa, amekitaka kila chama kije na Katiba yake ndani ya muda mfupi na utekelezaji wa baadhi ya mambo uanze.

Majaliwa, ni bahati kwetu wanamichezo. Lakini peke yake hawezi bila nguvu zetu sisi tunayesimama nyuma yake.

Kama Majaliwa, akija na mlengo wa kuinua michezo nchini inahitaji kila mmoja ndani ya nafasi yake kwenye chama ajitoe kwa nguvu na sio kuingiza ubinfasi.

Ubinafsi ni kitu kibaya sana. Umezifanya taasizi nyingi ziweze kufa. Mipango ya Majaliwa na michezo nchini isiingizwe na ubinafsi ambao umetufanya tukwamie hapa.

Maana hata Baraza la Michezo nchini (BMT), limeshindwa kusimamia vyema michezo na kuitoa nchi katika wingu kubwa la aibu hii.

Tunahitaji nguvu ya BMT, kuhakikisha inapita kwenye kila chama chake kuhakikisha kama nchi inasimama vyema kwenye michezo.

Kama michezo itasimamiwa vyema kuna vijana wengi watapata ajira na nchi itaondokana na umasikini huu ulioko sasa.

Kama bondia mstahafu wa Marekani, Floyd Mayweather ‘Junior’, ameweza kuajiri zaidi ya 100, ambao wanaishi kwa ajili yake, kwanini vijana wa Kitanzania wana vipaji, lakini wanaishi maisha ya hali ya chini?

Mayweather, anaweza kumudu kuwalipa watu hao ni kutokana na michezo kwao ni ajira na sio burudani kama ilivyo kwetu.

Muda ulioko sasa ni kumkumbatia Majaliwa kuliko chochote kile, huku kila kiongozi wa chama akisimama ndani ya weledi.

Mpaka kipindi cha Majaliwa kitakapoisha, nasi wanamichezo tuwe na kitu chetu ambacho kitakuwa na muendelezo wa vizazi na vizazi kukuta na wao kuendeleza.

Itakuwa jambo la aibu kama muda wa Majaliwa utaisha bila hata ya mchezo mmoja kufanikiwa. Ni muda sasa wa kila mmoja kuamka katika usingizi huu mzito. -

Raia Mwema
 
Back
Top Bottom