Kipa chaguo la kwanza wa Simba ya Dar es Salaam, Juma Kaseja amesema kuwa yuko tayari kupokea maamuzi yoyote yatakayotolewa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu yake inayotarajiwa kukutana leo jioni, imefahamika.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kaseja alisema kuwa hana hofu na maamuzi yoyote yatakayochukuliwa na viongozi wake ambao amefanya nao kazi tangu mwaka 2002 akitokea Moro United.
Alisema kuwa katika mpira, mchezaji anapaswa kukubaliana na mazingira yaliyopo, lakini haamini kwamba uwezo wake umeshuka kiasi cha kufikia hatua ya kuona maamuzi ya kuongezwa kwake mkataba yakifikiwa kwa kupiga kura.
"Hivi kweli mimi (Kaseja) nimeshuka kiasi hicho, siamini! Niko tayari kwa lolote, huu ndio mpira wetu wa Tanzania," alisema Kaseja ambaye alikuwa kipa bora msimu wa 2009/ 2010 na kuisadiai Simba kuandika rekodi ya aina yake kwa kutwaa ubingwa huku ikiwa haijawahi kufungwa .
Kaseja aliongeza kuwa yeye bado ana mkataba na Simba ambao unamalizika Juni mwaka huu na kabla ya kufikiria kusaini mkataba mwingine, ni lazima afahamu maslahi yake.
Alisema kuwa kupanda na kushuka kwa mchezaji ni jambo la kawaida na wakati mwingine, hutokana na aina ya wachezaji wanaounda kikosi kinachoshuka uwanjani.
"Ni lazima kwamba uangalie vigezo vingine kabla ya kusema fulani ameshuka kiwango, uzuri wa kila mchezaji huchangiwa na wachezaji wenzake anaoshirikiana nao uwanjani," aliongeza Kaseja.
Hata hivyo, Kaseja aliongeza kwamba amepigiwa simu na mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, akielezwa kuwa anatakiwa asichanganwe na taarifa zinazoandikwa au kuzungumwa na watu mbalimbali.
Alisema kuwa kiongozi huyo (jina tunalo) alimueleza kwamba Simba bado inamuhitaji na inaamini kwamba mchango wake unatakiwa ili kufikia malengo waliyoyawekea.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili inazo ni kwamba viongozi wa Simba bado wanatofautiana kuhusiana na suala la kuachwa kipa huyo, baadhi wakisema kwamba anahitaji kupumzika na ili hilo lifanyike ni lazima wasajili kipa mwingine mwenye kiwango cha juu ili wacheze kwa zamu.
Hivi sasa, Simba pia ina makipa wengine wawili ambao ni Ally Mustapha, 'Barthez' na Kabali Faraji aliyepandishwa kutoka kikosi B cha Simba.