Karibu Jagina karibu

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,284
KARIBU JAGINA KARIBU.
1
Karibu ndugu karibu, jisikie u nyumbani,
Keti upate kababu, toa shaka mtimani,
Umepewa taratibu, soma ziweke kitwani.
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.
2
Jina la baba na babu, tutajie hadharani,
Sisaahu na lakabu, unotumia dimbani,
Ukipenda na muhibu, aliye mwako kichwani.
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.
3
Naomba nipe sababu, zakupenda hino fani,
Unambie taratibu, nielewe kwa undani,
Sinione nina gubu, kukujua natamani,
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.
4
Lipi halikupi tabu, kutunga ama kughani?
Jua sita staajabu, kijua yote mwandani,
Jibu niseme twaibu, miye nipate amani,
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.
5
Fani yataka adabu, imethibiti nadhani,
Kuwaheshimu mababu, hivi kuna mana gani?
Kama twakosa labibu, na kuibananga fani,
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.
6
Sasa nafunga kitabu, nisije zama gizani,
Naungaunga irabu, penye kosa samahani,
Kuandika najaribu, sijafuzu darasani,
Jagina karibu ndani, karibu ufanye yako.

Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
mzalendo.njano5@gmail.com
0762845394/0784845394
kwa mashairi mengine kama hayo waweza kujisomea katika blogu yangu, kwenye icon ya mashairi utabofya hapo kisha utayaona mashairi mengi nilitotunga
SASA HAMSINI RASI, HAMSINI MAJINUNI. | Kisima Cha Jangwani.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom