Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,286
Mwenzangu nikueleze, naomba sikio tega,
Fanya nenda ukacheze, pale unapo chezaga,
Tena muda sipoteze, ondoka pasi kuaga,
Chungu hutaki kupwaga, vipi moto uchokoze?
Nakuona uko bize, kama wataka kutaga,
Viapo uniapize, ni bure nimejikaga,
Ati uniangamize, jua kwetu nimeaga,
Chungu hutaki kupwaga, vipi moto uchokoze?
Lengo unitokomeze, fataki unazopiga,
Wataka unileleze, nikose pa kukanyaga,
Vidonge sasa umeze, una hiyari kumwaga,
Chungu hutaki kupwaga, vipi moto uchokoze?
Umetumwa unichokoze, mtumaji ana woga,
Aliko na achomoze, akome kwake kuzuga,
Nangoja ajikooze, sima 'tasema ubaga,
Chungu hutaki kupwaga, vipi moto uchokoze?
Kaditama sipuuze, inyeshayo si mawaga,
Si masika nikujuze, hiki kimbunga chapiga,
Singoje kikufukuze, dunia ukaiaga,
Chungu hutaki kupwaga, vipi moto uchokoze?
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whats 0622845394 Morogoro.