John Heche: Wananchi wa Tarime Vijijini tumechoka Kunyang'anywa Ardhi na Unyanyasaji wa DC

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,689
55,662
IMG_20170412_115753.jpg
IMG_20170412_115803.jpg

Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ana mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Hoteli ya Defrance, iliyoko maeneo ya Sinza White Inn au Sinza Darajani karibu na Uwanja wa Tiptop.

=========

=> Kikubwa anamlalamikia Mkuu wa Wilaya ya Tarime kwa Kutumia nguvu Kuwanyang'anya Ardhi watu wa Tarime eti wanataka kumpa Muwekezaji wa Kiwanda.

=> Sisi watu wa Tarime hatutakubali, sisi watu wa Tarime hatutakubali. Pale Tarime ni Ukanda wa dhahabu. Wanakuja kupima na vifaa vyao. Miwa inapandwa huko chini? Tunahofia wameona kuna dhahabu pale wanasingizia wamepata muwekezaji wa Kiwanda cha Miwa.

Wale Wawekezaji wa dhahabu ukikatiza eneo lake unapigwa risasi eti ni mtu wa nje. Mwananchi wa Tarime na Muwekezaji nani mgeni wa eneo lile?

=> Mkuu wa Wilaya hawezi kuwazungumzia wananchi bila kuwepo Mbunge.
=> Tunachotaka mkuu wa Wilaya alete huo mkataba wa Uwekezaji tuujadili baraza la Madiwani na tukubaliane ni ardhi kiasi gani tutoe.

=> Wasipofanya hivyo, tutapambana nao na mimi ntaongoza. DC hana gereza la kutuweka watu wote wa Tarime. Tuna Wanajeshi Wastaafu karibia kila nyumba, nakuhakikishia wasipofuata Sheria tutapambana na huyo Muwekezaji. Ataweka Bendera tunaichoma moto. Sisi Tarime hatutishwi wote mnajua.

=>Hii nchi inapoenda ni kubaya. Kuna nesi alisoma kwa jina la mtu mwingine sasa hivi kafungwa, lakini kuna mtu anajiita bashite, kila mtu anamuogopa. Lema alisema kuna watu wanaandamana moyoni, juzi ulimuona Bashe anavyolia, ile ndo Lema alikuwa anaiita kuandamana moyoni.

=>Watu wanatumiwa meseji za vitisho Serikali ipo kimya.

=>Nawaunga Wabunge wengine kwamba Nchi yetu ni zaidi ya CCM, CHADEMA, CUF au chama kingine.

=>Sasa hivi Afrika kusini Serikali imegawanyika. Makamu rais anampinga rais huko Afrika kusini. Nchi yetu inaelekea huko. Haijawahi mutokea wabunge wa CCM kuilalamikia Serikali hivi.

=> Sasa hivi Mbwembwe za Mawaziri kufanya Ziara za kushitukiza zimeisha. Wameanza kunyooka.

=>Tunaenda kujadili Wizara ya Tamisemi. Tutambana rais, hela inatangazwa lakini hatuioni Majimboni.



OFISI YA MBUNGE JIMBO LA TARIME VIJIJINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA KUHUSU WANANCHI WA TARIME KUNYANG'ANYWA ARDHI

Ndugu wanahabari

Nimeomba kukutana na ninyi hapa kama hatua ya awali na haraka kuzungumzia suala muhimu na nyeti linaloendelea kuhusu uporaji wa ardhi ya wananchi wa Jimbo la Tarime Vijijini ambalo kama mnavyojua mimi ni mwakilishi wao.

Nimelazimika kuwaita na kuzungumza nanyi nikiwa Dar es Salaam kwa sababu jambo ambalo nitalizungumzia limewaumiza wananchi wangu na kuibua hofu kubwa miongoni mwao hasa baada ya kuona kupitia vyombo vya habari kuwa ardhi yao 'imeporwa na kugawiwa' kwa anayeitwa mwekezaji, kinyume na utaratibu kama nitakavyoeleza.

Eneo la Bonde la Mto Mara hasa katika vijiji vilivyoko katika kata za Matongo, Kemambo, Kibasuka na Manga; lina historia kubwa tangu enzi za mababu, kwa sababu tangu kuwepo kwake ni sehemu ya uhai na maisha ya watu wa Tarime, likitumika kwa ajili ya kilimo, ufugaji, samaki (chakula na kipato) na maji.

Wananchi wa maeneo hayo ambao upo ushahidi usiopingika kuwa ni wakaazi na wamiliki wa ardhi hiyo, wako katika sintofahamu na hofu kubwa ya kupoteza ardhi yao kwa sababu tu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na baadhi ya watu wanaojificha nyuma ya mtu anayedaiwa kuwa ni mwekezaji, wanataka kutumia mabavu, vitisho na kukandamiza watu, ili wajipatie eneo la kuweka mradi wa ujenzi wa kiwanda cha miwa.

Ndugu wanahabari, jambo hili, kwa namna ambavyo limeendeshwa na ghafla kuonekana kupitia vyombo vya habari, limemshtua karibu kila mtu. Kuanzia sisi wawakilishi wa wananchi kwa maana ya mbunge, madiwani na wananchi wenyewe.

Kwa hakika kabisa, suala hili ambalo tayari limeibua mgogoro wa chini chini na sasa malalamiko ya watu wangu huko jimboni ni kama volcano inayoweza kulipuka wakati wowote, linawakumbusha watu wa Tarime kwenye historia ya athari za uwekezaji unaoletwa kwa njia zisizozingatia taratibu na maslahi ya wananchi.

Ndugu wanahabari

Hadi leo watu wa Tarime bado hawajapona majeraha na makovu ya uwekezaji unaoletwa kwa namna hiyo ya kubebwa na kulazimishwa na watawala.

Wanajua na wanakumbuka vyema kuwa uwekezaji wa uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa North Mara ulioko katika Kata ya Matongo, Kibasuka, Nyamwaga na Nyarukoba umewaacha katika shida kubwa ya ardhi, huku wakilazimika kupambana dhidi ya risasi na mauaji ili kunufaika na rasilimali ambazo zinavunwa kutoka katika maeneo yao.

Ni vyema nikaweka kumbukumbu sawa kupitia taarifa hii kuwa, tahadhari tunayoitoa na kukataa uporaji wa ardhi unaotaka kufanywa na DC kwa mgongo wa uwekezaji wa kiwanda, ni kwa sababu watu wa Tarime walishaumwa na nyoka kupitia uwekezaji wa Nyamongo, sasa wakiguswa na nyasi huko Matongo, Kemambo, Kibasuka na Manga LAZIMA tushtuke.

Kuonesha kuwa mradi huu hauna uhalali, Serikali ya Wilaya kupitia kwa mkuu huyo wa wilaya, baada ya kukiuka taratibu zote zinazotakiwa kuweza kutwaa ardhi ya wananchi, wameanza kukamata, kutisha, kubambikia watu kesi na hata kulaghai ili kulazimisha uwekezaji huo, mfano;

(i) Mwalimu Eliud Choggo, S/M Bisarwi amehamishwa ndani ya masaa 24 kwenda S/M Magoma na kushushwa cheo kutoka mwalimu mkuu na kuwa mwalimu wa kawaida, kinyume na taratibu za utumishi wa umma kwa sababu ya kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakihoji ujio wa mradi huo na hatima ya ardhi yao.

(ii) Mzee Marwa Gesamore Chacha (67) na Mwinyi Marwa, wamekamatwa na kubambikiwa kesi kwamba wanapinga maendeleo baada ya kuhoji maeneo yao kupimwa na kutaka kuchukuliwa bila ridhaa ya wananchi, kinyume cha Sheria za Nchi.

(iii) Wenyeviti wa Vijiji kulazimishwa kutoa mihtasari ya vikao vya nyuma pamoja na orodha ya wananchi ili itumike kama ushahidi kwamba mikutano mikuu ya vijiji imekaa na kuridhia. Hii ni kinyume cha kifungu cha 12 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5, 1999 ambacho kinaeleza utaratibu mzima wa namna ya kutoa ardhi ya kijiji kwa mtu yeyote anaeomba ardhi kwenye kijiji husika.

Ndugu waandishi wa habari, ni vyema ikaeleweka kwamba, hatupingi kuwepo kwa mradi wa ujenzi wa kiwanda.Kinachotakiwa hapa ni utaratibu uzingatiwe, kama ifuatavyo;

Kwanza, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 (The Village Land Act no. 5 of 1999) kifungu cha 3 kinachosema wazi kuwa eneo la mwananchi/wananchi likitwaliwa lazima fidia ilipwe kwanza"Fair prompt and adequate compensation should be paid before acquisition of anypiece of land".


Sheria hiyo pia inaelekeza kuwa vijiji havina mamlaka kisheria ya kugawa zaidi ya ekari 50 za ardhi.

Pili, lazima uwepo uwazi katika mradi huo pamoja na ushirikishwaji wa wananchi ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu manufaa kwa jamii nzima kutokana na uwekezaji huo.

Tatu, mbunge kama mwakilishi wa wananchi pamoja na madiwani kupitia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kushirikishwa kikamilifu.

Msimamo wa Mbunge

Naomba kusisitiza hapa kuwa sipingi wala sikatai mradi huo wa uwekezaji wa kiwanda. Hakuna mtu yeyote anaweza kupinga uwekezaji wowote makini kwenye eneo lake. Ninahitaji ushirikiswaji wa wazi wa wananchi, wawakilishi wao ili kuondoa misuguano na misigano itakayoibua mgogoro mkubwa wa ardhi na kusababisha madhira na madhara kama ya Nyamongo, ambayo nisingependa turejeshwe huko.

Ili mkataba usainiwe lazima utaratibu urudi na uanzie kwa wananchi kwa namna ile ile ambayo nimeeleza hapo juu. Na ningependa mwekezaji huyo mtarajiwa aelewe kuwa tunataka haya yafanyike ili kuondoa mapungufu yoyote yanayoweza kuibua upya machungu na maumivu ya watu wa Tarime ambao wamemwaga machozi, jasho na damu wakipigania maslahi yao na kuhoji matumizi ya rasilimali zilizoko katika eneo lao dhidi ya wawekezaji.

Ardhi kwa watu wa Tarime ni jambo nyeti sana na ndiyo urithi pekee walionao watu wanyonge na maskini. Kwa sababu idadi ya watu inaongezeka na ardhi haiongezeki. Kuchukua sehemu kubwa kama hiyo kutoka kwa watu wengi maelfu ya watu na kumkabidhi mwekezaji ni suala linalohitaji kufikiriwa na kuangaliwa kwa umakini sana kabla halijaleta madhara makubwa.

Napenda kumkumbusha DC, kama niliposema hapo juu, kuwa maeneo ya kata hizo yamekuwa yakitumiwa kwa shughuli za kijamii kwa ajili ya uhai, maisha, maendeleo na ustawi wa jamii nzima (yapo hadi makaburi ya miaka ya 70). Aache mara moja kutumia propaganda za kuwasingizia watu hao kuwa ni wakulima wa bangi kama mpango wake wa kupotosha, kuwachafua na kuwatisha watu wa Tarime aili afanikishe jambo analolijua yeye. Hapa tunazungumzia maelfu ya hekta yanataka kuporwa na wajanja wachache kwa mgongo wa uwekezaji.

Ninasimamia msimamo wa wananchi wangu wanaotaka mkataba huu usomwe, ujadiliwe na kuridhiwa na wakazi wa eneo husika. Hapa nilipo mimi mwenyewe mbunge wao sijausoma, ofisi yangu haina taarifa. Sijui nini kimo ndani yake.

Kama jambo hilo kweli lina manufaa kwa jamii, lifuate taratibu za kisheria na lipate uhalali wa kukubalika kwa watu wenyewe.

John Heche (MB)

Aprili 12, 2017
 
Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ana mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Hoteli ya Defrance, iliyoko maeneo ya Sinza White Inn au Sinza Darajani karibu na Uwanja wa Tiptop.
d26183628167ff02e2827cde895de1dd.jpg
2b5c0a9e72d102be70bab5817f5d1544.jpg
WAACHE KUVAMIA MACHIMBO KUIBA MCHANGA WA DHAHABU !
 
Naomba kuuliza hivi wawekezaji WA HAP[O NYAMONGO huwa wanafata wakazi wa nyamongo majumbani kwao na kuwa piga risasi au Wakazi wa nyamongo wanavamia migodi kuiba????na walinzi wa wawekezaji wana tumia silaha za moto kujihami????
MAANA SITAKI AMINI KWA UTAWALA HUU WAWEKEZAJI WANA WEZA FANYA HUU UJINGA WA KUONEA WATANZANIA.........ilah naamini kabsa hawa vijana wa hapo NYAMONGO wanavamia migodi na kutaka kuiba wakiwa na matarajio ya kuwa mtetezi wao yupo HUYU HECHE.......
 
Angefanya vizuri kama angewahutubia wananchi wake na kuwaambia ardhi haitoki.

hata hivyo sijawahi kuona DC anaingia mkataba wa kutoa ardhi kwa mwekezaji, wenye mamlaka hayo ni baraza la madiwani kwa niaba ya wananchi.
 
Vituko vya media haviishi badala ya kupanga mikutano ya hadhara kuwambia wanachi mubashara wake kila kata au sehemu usika anakimbilia media vituto mwaka huu zitazidi
 
Angefanya vizuri kama angewahutubia wananchi wake na kuwaambia ardhi haitoki.

hata hivyo sijawahi kuona DC anaingia mkataba wa kutoa ardhi kwa mwekezaji, wenye mamlaka hayo ni baraza la madiwani kwa niaba ya wananchi.
Kwa ma-DC wa CCM inawezekana.
 
Back
Top Bottom