Jipu la moyo

Nicodemas Tambo Mwikozi

JF-Expert Member
Joined
Aug 13, 2016
Posts
663
Reaction score
1,047
Nimepanga kwenye chumba kimoja maeneo ya kigamboni. Na ninaishi kisela, maisha ya kigumu. Sina mke wala demu, na sitaki demu. Sitaki kabisa kusikia huo utumbo. Hapa nilipo nina hasira hadi natamani niache kuandika!!

Namlaumu sana Nasra, kwani ndiye kasababisha yote haya. Yani kwa jinsi navyomuheshimu... Namlaumu kishenzi, na sitaacha kumlaumu!

Kwenye nyumba hii tupo wapangaji karibu saba. Lakini ukitoa mimi na Nasra waliobaki wote ni wanafunzi wa vyuo. Sina muda wa kuwafuatilia. Lakini nasikia wengine wanasoma hapo Mwalimu Nyerere Memorial Academy na wengine IFM. Sina time nao. Wananisaidia nini?

Nafanya kazi kwenye kampuni moja kubwa ya mafuta huko vijibweni. Nikutajie jina la kampuni yangu ili iweje? Naomba na wewe usinichanganye!

Kikubwa tambua kuwa mimi ni kibarua pale, na sikosi vishilingi mbili tatu kutokana na dili za wizi wa hapa na pale. Mshahara huwa tunausubiri kama fasheni. Kwa hiyo ukisikia sehemu panauzwa mafuta pasi ujue wizi haukosekani. Habari ndiyo hiyo!

Ibra na Pazi ni washkaji zangu wakubwa. Tulipata kazi pamoja, na kabla ya hapo tulisota sana mtaani kipindi kile tunaishi wote buza.

Tunachopishana na hawa jamaa ni kuwa washikaji ni walevi wakubwa. Tena bora wangeishia kwenye pombe peke yake. Ulevi wao umefungua matawi kwenye ngono na sigara. Wanapenda ngono kuliko chakula. Wanavuta sigara kama oksijeni. Wanahusudu club za usiku kuliko Trump anavyohusudu mabifu!

Kuna baa gani hapa mjini wasiyoijua? Kuanzia huko sijui forty forty tabata hadi liquid ya kigamboni, kote ni wenyeji wakubwa. Na kila waendako kuna malaya gani wasiyemfahamu? Wanawajua makahaba wote kwa majina na 'viwango' vyao!

Wakati fulani niliwahi kwenda kutazama nao soka kwenye club moja ya usiku maeneo ya Sinza, nilikoma. Na kuanzia hapo nikaapa kuwa uswahiba wetu utakuwa unaishia saa kumi na mbili jioni, baada ya hapo tusijuane asilani.

Kazi zenyewe hizi za kujishikiza kama mtarimbo wa kuzuia mgomba unaotaka kuanguka; unatoa wapi mfupa wa kuanza kutapanya pesa kwenye pombe na wanawake? Pesa zenyewe za magumashi! Watajua wenyewe aisee!

Achana na hao mbwiga, sikiliza kisa chenyewe kilichotunga jipu kwenye moyo wangu hadi naongea kwa jazba hivi!

Jumamosi iliyopita Pazi alikuja kunisalimia nyumbani. Wala hii haikuwa mara yake ya kwanza. Mara nyingi tu huwa wanakuja kunisalimu, ila sikumbuki ilikuwaje leo akaja peke yake.

(Mtanisamehe msiotumia) Mchana huo tumekaa hapa tunakula kitimoto ndipo mambo yalipoharibika.

Kwanza mwanzo nikasema labda ni hizo bia mbili nilizomnunulia, maana huwa sina hiyana wakija kunisalimia, huwa nawanunulia kipenda roho chao, japo kwa masharti ya chupa zisizozidi mbili mbili. Lakini toka lini komba hawa wakalewa kwa bia mbili?

Pazi alimuona 'shemeji' yake akiingia kwenye chumba cha Da Nasra, acha macho yamtoke! Wakware utawajua tu, na ndiyo maana sikuwahi kuwatambulisha. Wahuni sio watu!

Rose hakuwa mwanamke wa kumtambulisha kwa watu sampuli ya Ibra au Pazi. Ni sawa na kumuonesha fundi wako gari unalotaka kununua kwa mtu, lazima alitesti!

Hawa ni jamaa zangu na tumetoka mbali, lakini linapokuja suala la mwanamke nilishajiapia ntakuja kuwatambulisha shemeji yao siku ya kufunga ndoa. Hawaaminiki hata kidogo. Niwatambulishe mke wangu mtarajiwa hawa chovya chovya sijipendi? Wakafie mbele pimbi wakubwa hawa!

Ungemuona huyo Rose mwenyewe ungedhani ana umri mkubwa kunizidi, kumbe ndiyo kwanza alikuwa na miaka ishirini na mbili.
Toto limeenda hewani, miguu iliyoshiba, upana wa kutosha, rangi safi kabisa ya chocolate isiyojua makali ya vipodozi. Rose alikuwa na weusi wa asili uliomvutia kila aliyemtazama, na kumkosesha raha kila mwanamke aliyejichubua.

Maana alikuwa kama kioo kilichowasuta wapenda mkorogo, "kumbe hata weusi ni mzuri hivi?" Ni kama walikuwa wakijilaani kimoyomoyo kila walipomuona, na kuishia kusema ati anafanana na Anti Ezekiel, pumbavu kabisa washindwe na walegee. Maana siku si nyingi na mimi wataniambia nafanana na Mose Iyobo nguchiro taipu hawa! Kwani mimi ndio niliwatuma wajichubue?

Siku nimemuona mara ya kwanza nilichanganyikiwa. Alikuwa amekuja kwenye chumba hicho cha mpangaji mwenzangu ambaye tumezoea kumwita Da Nasra ambaye ana saluni yake maeneo ya ferry, ushoga wao ulipoanzia.

Siku hiyo sikuweza kabisa kuudhibit moyo wangu. Waswahili wanasemaga hakuna mkate mgumu mbele ya chai. Siku hiyo yalinishinda, na baada ya kumuona anamsindikiza nilitoka nje na kumsubiri Da Nasra mlangoni pake ili nianzishe chokochoko.

Alivyorudi tu nikamchokoza, Nasra akaachia cheko lake kabla sijamuonya. "Da Nas, tafadhali....cheko hilo vepe? Unafikiri tuko saluni kwako hapa?"

"Utamuweza?" Ndilo swali alilopiga nalo breki ya kufungia hilo cheko la kikuda.

"Nisimuweze kwa mpango gani? Hivi unanichukuliaje Da Nasra...?"

"Akha....manake wasichana wa mjini hawa kaka'ngu..." Alinikatiza dada wa kizigua. Kuona bado namkazia macho akashusha zaidi sauti yake.

"Usijali kakangu....maadam umeonesha nia, we niachie mimi!" Alihitimisha kwa kauli hiyo ambayo iliniachia bubujiko la furaha moyoni.

"Fanya hima sister, nimeoza sifai..." Nikagonga msumari wa mwisho. Da Nasra akacheka tena lile cheko lake na kuingia zake ndani.

Baada ya hapo ikawa kimuhemuhe. Kazini namuwaza Rose. Nimepanda bodaboda namuwaza Rose. Wakati wa kulala ndiyo usiseme. Kweli kupenda ugonjwa.

Kila siku nikawa namvizia Da Nasra nikitegemea breaking newz yoyote. Na yeye akawa kama ananikomesha, hanitafuti wala hanisemeshi.

Ndipo ikaja siku ya unyakuo. Unyakuo wa penzi la toto lile la kibantu. Nikiwa sijui hili wala lile, Da Nasra aliniita aliponiona nafunga kufuli la mlango wangu. Hata sikumbuki nilikuwa nataka kwenda wapi.

"Njoo umsalimie mdogo wangu...!" Aliniita.

Nilienda kwa papara ndipo nikakutana na Rose akiwa kwenye kiwango kingine cha ubora. Alikuwa kapendeza mno japo kuna kasoro chache ambazo niliziona na kuzifumbia macho.

Kasoro ya kwanza ilikuwa ni lile wigi alilovaa. Sikulipenda hata kidogo. Lilikuwa kubwa mno tena likiwa limesheheni mirangirangi ya kila aina utadhani upinde wa mvua. Uzoefu wangu ni kwamba mawigi ya kishankupe kama haya huwa yana vinasaba vya ushangingi na mvaaji.

Pili, machoni alikuwa amebandika zile kope za bandia, na kuyafanya macho yake yawe kama ya mdoli kila alivyoyapepesa. Sipendagi kabisa hizo mambo!

Tatu na mwisho ni hicho kimini alichovaa. Ukweli ni kuwa hapo kochini alipokaa licha ya kukivutavuta na kujibana, kilianika nje robo tatu ya mapaja yake laini yaliyokula mafuta ya kutosha. Ukweli alivutia mno lakini nilijiuliza hali ilikuwaje huko barabarani alikopita?

Anyway, akishaingia kwenye kumi na nane zangu, nitamfunza jinsi kujienzi. Nilijisemea moyoni hata kabla sijajua kama ntapata hifadhi au lah.

"Shikamoo..." Eti akaniamkia huku macho yake makubwa meupe na mazuri yakinitazama kiwiziwizi.
"Asante..." Nikapotezea.
"He....makubwa! Jamani Foro mdogo wangu si kakuamkia hapa? Mbona huitiki?" Hizo zilikuwa fujo za maksudi za Nasra. Namjua sana huyu dada alivyo mtu wa makuzi.

"Mbona nimeitika? Nimesema marahaba asante....!" Vikafuata vicheko, huku mwenyewe Rose akicheka kwa aibu akijiziba mdomo.

Moyo wangu ulikuwa ukirukaruka kwa furaha. Ni dhahiri kazi ilikuwa imeshamalizwa siku nyingi na Dada yangu Nasra. Mimi nilikuwa nakuja tu kusaini mkataba wa maridhiano.

** **
Mpaka sasa tulikuwa na miezi kama mitano ya mapenzi motomoto. Penzi lilikuwa limeota mizizi utadhani tumefahamiana miaka saba iliyopita. Wanaonifahamu walisema nimenawiri sana tangu nilipoanzisha mahusiano na huyo mwanamke. Nami sikuacha kurudisha sifa na shukrani kwa Dada yangu Nasra.

Nilimpenda sana Rose. Nilimpenda kwa vitu vingi. Kwanza kabisa ni ule ukimya wake. Alikuwa hana maneno mengi. Kila tulipokuwa naye alikuwa mkimya akinitazama tu usoni. Kucheka ndiyo kikubwa alichokiweza. Kila nilichomwambia alisema sawa. Hakuwa mbishi wala hakuwahi kukasirika.

Zamani sana sikuwahi kutamani kuwa na mwanamke wa namna hii, anayenikubalia kila kitu na kukosa kunipa changamoto?

Wanasaikolojia wanadai wanawake wa namna hiyo licha ya kuwa na mapenzi ya dhati, na hodari wakubwa kitandani, huwa hawana msimamo linapokuja suala la kutongozwa na wanaume wa nje. Lakini kwani wanasaikolojia ni miungu? Si kila wasemalo lazima liwe kweli.

Pili, Rose alikuwa anafundishika. Kwa hiyo miezi minne alikuwa amebadilika sana kitabia na kuachana na tabia karibu zote zilizonikereka siku za awali, ikiwa ni pamoja na uvaaji wa mawigi, kuvaa nguo fupi au zilizoshikamana na mwili wake kiasi cha kusababisha 'vikohozi' kila tulikopita. Mwanamke wa kuoa ana sifa zipi zaidi ya hiyo?
Hata yale makope ya bandia alikuwa hajipachiki tena. Unaachaje kumfungia moyoni mwanamke kama huyo?

Kitu cha tatu nilichompendea unadhani ni zaidi ya hicho unachofikiria? Hakuna kingine zaidi ya hicho...

Nilimtambulisha kwa baadhi ya ndugu zangu wachache sana ninaowaheshimu. Na wote walinipa heko.

Nikamuonesha saiti yangu, nilikoanza kujenga nyumba yetu huko Mwembe mtemvu. Alifurahi sana. Na kama mara mbili au tatu nilishamtuma awapelekee hela mafundi ili wanunue vitu vilivyohitajika. Na hapo ndipo nilipogundua umakini wake. Hakuwakabidhi tu pesa, bali alisimamia kuhakikishia kila kitu kimenunuliwa ndipo akaondoka zake.

"Mafundi hawaaminiki mme wangu!" Aliwahi kuniambia.

Rose alikuwa akiishi na mama yake mdogo maeneo ya Magomeni. Sikuwahi kuonana naye lakini walau tumeshazungumza mara mbili au tatu kwa njia ya simu.

Kwa wiki Rose huja kwangu mara mbili au tatu, katika siku nazokuwa napumzika. Na kwa maadili yangu sikutaka katu kuanza kuishi naye kama mke bila kufuata taratibu. Nayajua madhara. Ukishaanza hivyo basi ujue habari ya kufunga ndoa utaisikia kwa jirani. Tena omba sana mimba isinase. Hivyo nilimruhusu aje na kuondoka. Mara chache sana alilala hadi asubuhi.

Jumamosi ya leo alikuwa na ratiba ya kuja kwangu. Kama kawaida yake, lazima aanzie kwa shogake Da Nasra, wakishamaliza kupiga umbeya ndipo anakuja kwangu. Nilishawazoea hivyo na wala sikuona shida.

Jicho la Pazi lilimuona Rose wakati anabisha hodi kuingia kwa Da Nasra. Mdomo wake ukabaki wazi kwa mshangao uliochangamana na tamaa. Umbo la Rose lilishamzuzua. Niliamini hivyo. Lakini kumbe sivyo ilivyokuwa!

"Umemuona yule demu?" Pazi alisaili akiwa amenitumbulia macho. Nikashtuka lakini nina uwezo mkubwa sana wa kuficha hisia zangu.

"Ndiyo...kwani vipi?" Nilimuuliza kwa utulivu huku nikimtazama jinsi alivyoyatoa macho.

"Anaishi hapa?" Akauliza tena kwa mihemko.

"Si umemsikia mwenyewe anabisha hodi, mtu atabisha hodi chumbani kwake mwenyewe? Huwa anakuja kumsalimu dada mwenye hicho chumba. Ni mashosti!" Nikamjibu kiupana.

"Aisee!" Pazi akashusha pumzi huku akiivuta simu yake mezani na kuifumbata kwenye kiganja cha mkono wake.

" Vipi? Umeshamtamani tayari?" Nikamkejeli.

" Sio Rose yule?" Pazi alisema huku akianza kusakanya nambari fulani kwenye simu yake.

"Unasema? Rose? Unamjua Rose?" Nilibweka huku nikiwa nimemtumbulia macho.

"Kwanini nisimjue? Sisi mapopo tunakutana na kila aina ya milupo....wewe si unajifungua ndani bhana? Utawaonea wapi hawa?"

Sikuamini nilichosikia kutoka kinywani mwa Pazi. Mlupo?

" Hapa nataka kumpigia simu Ibra, kwasababu juzi tu hapa alienda kupakua huo mzigo. Sema walizinguana kinyama. Hili demu linapenda sana hela...Usawa wenyewe huu, kununua malaya kwa elfu hamsini! Sijui walimalizana vipi?" Pazi aliongea hayo huku akicheka.

" Ila linajua mambo! Asikwambie mtu....walugaluga wanapigwa hadi laki moja na wanatoa!"

"Unamjua Rose?" Niliuliza tena kwa sauti dhaifu yenye kutetemeka! Tumbo lilishaanza kuunguruma. Jasho likanitoka kwa wingi.

" Babu kwani vipi? Unaogopa kusikia malaya? Mbona ndo zetu.... Mimi mwenyewe nimewahi kulichetua halafu mpira ukabasti... Aisee nilitoa macho siku hiyo? Ila bei zake ndo zilinishinda...nilipiga mara moja nikamuachia Ibra, yeye ndiyo huwa anajipigia...tena simu yake hii inaita..." Pazi aliongea kama vile ananikomoa. Maneno yake yalipenya kama upanga wa moto kifuani.

Rose ni kahaba?

" Oya we mzushi vipi?" Sauti ya Pazi ilichangamka baada ya kupokelewa na Ibra kabla hajaamua kuweka loud speaker...

" Fresh....ni aje babu?" Ibra alijibu kwa sauti inayoonesha alikuwa ameamshwa usingizini.

" Aisee niko kigamboni kwa mwana huku, huwezi amini nimemuona demu wako kaingia hapa..."

"Unazingua Pazi, demu wangu yupi?"
"Si Rose?"
"Rose yupi?"
"Cheusi dawa.."
Ibra alisikika akicheka kwa kujilazimisha. Ni dhahiri usiku uliopita alikesha kwenye pombe.

"Juzi kaniboa aisee... Nimemtandika kishenzi yule changu. Eti nimeenda zangu kuoga kachukua hela kwenye wallet yangu. Ujue huu mwezi wote anazingua eti ana mimba yangu anadai nimpe laki moja akaichoropoe. Mimi nikamwambia asinione boya...hiyo mimba asimpe bwana ake wa TTCL nije kumpa mimi?"

Mazungumzo yaliyoendelea kati ya Pazi na Ibra yalibakiza kidogo sana kunitoa fahamu. Nikawa sisikii kitu tena. Natetemeka tu huku nimejishika kifuani palipouma kama vile kitu chenye ncha kali kimesimikw kikatili.

Kuna asilimia chache nilizobakiza akilini. Asilimia za kujipa moyo kuwa huenda Rose wanayemuongelea sio huyu mchumba wangu. Rose wangu hawezi kahaba! Hata hivyo asilimia hizo zilikuwa chache kama zilivyo asilimia za kushinda milioni kumi ya tatu mzuka!

Kila walichokiongea kilisadifu wasifu wa Rose wangu.

Pazi alikata simu baada ya kumuona Rose anatoka chumbani kwa Nasra na kuja hapa tulipokuwemo. Pazi akanigeuzia macho yake makubwa kwa mshangao baada ya kumuona Rose anabisha hodi na kujikaribisha mwenyewe kwa kufunua pazia lile jepesi na kupokelewa na macho ya wanaume wawili wenye hisia tofauti juu yake!

** **
ANGALIZO

Ukimuona mwanamke mzuri wa sura na umbo ambaye anayaendesha maisha yake kwa kutegemea akili yake na kuweka kapuni uzuri wa shepu na sura yake; mpigie magoti, muamkie na kumpa heshima yake.

Wengi wanaofanana naye wameweka kapuni akili zao, na kuamua kuyaongoza maisha yao kwa kutumia uzuri wa sura na miili yao.

SITAKI TENA!

Poleni wanariverpool wezangi
 
Ifikie muda mjali afya zenu, umekutana na na mtu chocho unamvutia kwako unajipigia mambo yenyewe kama haya ya rose kahaba, pimeni kwanza mue huru kujiachia, subiri miezi mitatu ukapime
 
No body care anyway ndefu balaaaa soma mwenyewe.....
 
ANGALIZO

Ukimuona mwanamke mzuri wa sura na umbo ambaye anayaendesha maisha yake kwa kutegemea akili yake na kuweka kapuni uzuri wa shepu na sura yake; mpigie magoti, muamkie na kumpa heshima yake.


Nimependa ulichoandika hapa.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…