Jinsi ya kuishi na moyo mkubwa

Kurzweil

JF-Expert Member
May 25, 2011
6,622
8,411
MOYO.jpg


Kwa ufupi
kupumua kwa shida ni moja ya dalili za moyo kupanuka. Wakati nikiwa nazungumza na mmoja wa wasomaji wa gazeti hili mwenye tatizo la moyo mkubwa aliuliza iwapo kuna vipimo vikubwa zaidi na dawa za kutibu tatizo la moyo kupanuka, limemsumbua kwa muda mrefu.

Anadai mwanzo alikuwa anapumua kwa shida akaenda hospitali, wakampiga picha ya x-ray na kumwambia moyo wake umepanuka na mapigo hayaendi vizuri. Alipewa dawa za mwezi mzima, katumia ila bado anapumua kwa shida. Aliniambia sasa anakata tamaa.

Mimi nilimhakikishia kuwa matibabu yapo na anaweza kulimaliza kulingana na aina ya tatizo na kuna uwezekano pia wa kulidhibiti pale tiba inaposhindikana. Hiyo ikoje, tafadhali fuatilia makala haya. Ili kuwaweka wasomaji kwenye nafasi nzuri, ni vyema nikaanza kwa kuelezea tatizo jinsi lilivyo.

Moyo Kupanuka ni Nini?

Moyo ni ogani yenye misuli, vyumba na kuunganishwa na mishipa kadhaa. Ogani hii ipo kwenye mwili wa mwanadamu na wanyama. Kazi yake kubwa ni kusambaza damu sehemu mbalimbali za mwili. Damu inayosambazwa huupa mwili oksijeni, virutubisho na kuondoa takamwili. Moyo hupanuka ili kukabiliana na tatizo la misuli ya moyo kuharibika.

Moyo kupanuka unaweza kusababishwa na vitu vingi, ila sababu kuu zinazopelekea moyo kupanuka ni kupanda kwa shinikizo la damu (hypertension) na ugonjwa wa mishipa ya moyo kuziba (coronary artery disease).

Sababu zingine zinatia ndani, maambukizi ya virusi katika moyo, valvu za moyo zisizo za kawaida, ujauzito hasa karibia na kujifungua, upungufu wa damu mwilini, ugonjwa/matatizo ya tezi, ugonjwa wa figo, matumizi mabaya ya pombe na madawa ya kulevya, maambukizi ya VVU, matatizo ya moyo ya kurithi. Hata hivyo, kuna sababu zingine za kupanuka moyo zisizojulikana moja kwa moja.

Moyo uliopanuka unaweza kushindwa kusukuma damu vizuri na kusababisha kupungua kwa nguvu ya moyo. Kukiwa na matibabu mazuri tatizo la moyo kupanuka linaweza kupungua na mgonjwa kujisikia vizuri ingawa linahitaji matibabu kipindi chote cha maisha ya mtu husika.

Ugonjwa wa misuli ya moyo (Cardiomyopathy) husababisha misuli ya moyo kukakamaa na kufanya moyo kujaribu kusukuma damu kwa nguvu zaidi kitu kinachoweza kusababisha moyo kupanuka. Ugonjwa huu umegawanyika katika aina kuu mbili, ugonjwa wa misuli ya moyo kupanuka (dilated cardiomyopathy) na ugonjwa wa misuli ya moyo kuwa minene (hypertrophic cardiomyopathy).

Ugonjwa wa misuli ya moyo kupanuka (dilated cardiomyopathy) hutokea pale kuta zote za moyo yaani ventrikali za kushoto na kulia zinapokuwa nyembamba na kuvutika kusababisha moyo kuongezeka. Wakati ugonjwa wa misuli ya moyo kuwa minene (hypertrophic cardiomyopathy) hutokea pale ukuta wa kushoto wa moyo yaani ventrikali ya kushoto inapoonenepa isivyokawaida na kufanya moyo kupanuka.

Kupanda kwa shinikizo la damu husababisha kupanuka kwa ventrikali ya kushoto.

Dalili za moyo kupanuka

Dalili za moyo kupanuka zinatofautiana kati ya mtu na mtu. Baadhi ya watu wanaweza kuwa bila dalili zozote, wengine dalili chache na wengine dalili nyingi hasa kushindwa kupumua vizuri.

Dalili za moyo kupanuka zinasababisha kupumua kwa shida, miguu kuvimba, tumbo kuwa kubwa, kuongezeka uzito, uchovu na moyo kwenda mbio. Baada ya kuzungumza na daktari jinsi unavyojisikia, daktari anaweza kubaini kupanuka kwa moyo wako kwa kukufanyia uchunguzi wa mwili wako.

Hata hivyo vipimo vingi vinaweza kufanyika kuweza kuthibitisha bainisho hilo. Vipimo hivyo ni kama echocardiography (ultrasound of the heart), kipimo kinachopima ukubwa wa moyo, unene wa misuli ya moyo na uwezo wa moyo kusukuma damu.

Vipimo vingine ni x-ray ya kifua, CT Scan, MRI na vipimo vya damu kama kuangalia VVU, ugonjwa wa tezi na wingi wa damu. Matibabu ya moyo kupanuka hukazia sana chanzo chake. Mfano ugonjwa wa mishipa ya moyo kuziba (coronary artery disease), kupanda kwa shinikizo la damu, matumizi ya pombe na dawa ya kulevya.

Mgonjwa atapewa dawa zitakazo tibu dalili kama kuvimba miguu na kutibu chanzo cha tatizo la moyo kupanuka. Moyo kupanuka ni hali ambayo inaweza kutibiwa kwa urahisi ikiwa itagundulika mapema, hivyo ni vyema kutafuta msaada wa kitabibu ikiwa unapata dalili yoyote kati ya hizo hapo juu.

Matibabu ya moyo mkubwa yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa, kubadili mfumo wa maisha na wakati mwingine upasuaji wa moyo.

Kuna njia zinazoweza kuiboresha hali yako ingawa haiwezi kutibika kabisa. Daktari wako anaweza kupendekeza aina ya maisha unayopaswa kuishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuvuta sigara na kupunguza uzito.

Utataikiwa kupunguza uzito iwapo uzito wako hauendani na kimo chako maarufu kama BMI, kupunguza matumizi ya chumvi kwenye vyakula, kudhibiti kisukari, kudhibiti kupanda kwa shinikizo la damu, kufanya mazoezi yanayopendekezwa na kutotumia pombe au kahawa.

Vilevile utatakiwa kupumzika vya kutosha mfano kulala masaa nane usiku.

Jambo jingine ni kuhakikisha unajiandikisha kliniki kwa ajili ya uchunguzi wa mara kwa mara na kutibu matatizo yanayoandamana na hali hiyo.
 
Back
Top Bottom