Jinsi watawala wanavyosigina mamlaka ya wananchi

Ntile II

Member
Nov 19, 2015
22
12
Yupo mwanafalsafa mmoja kutoka Ufaransa anaitwa Baron De Montesquieu mtalamu wa Sheria pamoja na masuala ya utawala katika Ulaya mnamo karne ya kumi na nane aliwahi kuainisha aina tatu za tawala katika Mataifa, Aina ya kwanza kwa mujibu wa De Montesquieu ni tawala za Kifalme (Monarch) zinazoongozwa na Wafalme au Malikia, tawala za pili ni zile tawala za Kijamhuri (Republic) ambazo huongozwa na kiongozi mkuu wa nchi ambaye huchaguliwa na wananchi na aina ya tatu ni zile tawala za Kiimla au kidikteta (Depotism).

Hata hivyo, kama alivyoamini mwanafalasa huyo karne kadhaa zilizopita kwamba tawala za Kijamhuri zinazotokana na kuchaguliwa na watu yaani za Kidemokrasia ndizo zafaa katika taifa vivyo hivyo bado mpaka hii leo tunaamini ndivyo. Lakini mafanikio yoyote ya Utawala wa kidemokrasia yanategemea nguvu na mamlaka ya wananchi waliyonayo juu ya utawala wao na jinsi gani mgawanyo wa madaraka (separation of powers) unavyoheshimiwa baina ya mihimili mitatu ya dola yaani Serikali, Bunge na Mahakama.

Katika taifa la kidemokrasia ukiachilia mbali mihimili mingine ya dola, Bunge ndio chombo pekee cha wananchi ambacho huendesha mkutano wa kitaifa juu ya mijadala mbalimbali inayohusu wananchi wenyewe na taifa lao kwa ujumla juu ya namna ya kujipangia na kujiamlia mambo yao wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Hapo ndipo dhana ya Uwakilishi na Ushirikishaji wa wananchi inapoanzia, kwani katika zama za sasa wananchi wote hawawezi wakakusanyika kwa pamoja kufanya mkutano wa Kitaifa, ndio maana wanawachagua wawakilishi wao kupitia uchaguzi lakini bado haitoshi wananchi wana haki ya kushirikishwa katika mijadala hiyo kwa kujua kinachoendelea katika mkutano wao wa kitaifa ambapo wanawakilishwa na Wabunge wao walio wachagua.

Nchini Tanzania, hivi karibuni imezuka mijadala mbalimbali juu ya uhuru na haki za wananchi katika kupata taarifa mbalimbali kutoka katika chombo chao cha Bunge,hii imetokana na hatua ambazo Serikari ilizichukua ikiwemo ile ya kuzuia kurushwa kwa matangazo ya Bunge moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa pamoja na zile za watu binafsi kwa sababu mbalimbali ikiwemo mpango wa Serikali kubana matumizi ya fedha za umma. Hizi ni hoja ambazo hazina nafasi katika ulimwengu huu wa sasa wa Kidemokrasia na Maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mantiki ya kuzima matangazo ya moja kwa moja ya Bunge kupitia televisheni ya Taifa na zile binafsi inaleta tafsiri ya uporaji wa haki na mamlaka ya Wananchi katika Bunge lao. Kwa kuwa Bunge ndio chombo pekee chenye madaraka kwa niaba ya Wananchi kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 63 (2) ambayo inasema ‘…Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya Wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake yote…’, hivyo basi, kwa mantiki hiyo wananchi wananyo haki ya kufuatilia juu ya kile kinachoendelea katika mijadala ya Bunge lao pasipo shaka lolote.

Katika minajili ya kuisimamia serikali, Katika vikao vya Bunge ndiko inakoendeshwa mijadala mipana ya kuchambua utekelezaji wa mipango na sera za serikali kwa wananchi. Katika mijadala hiyo, ndipo mwananchi anapata mwanga na picha ya serikali yake aliyoichagua.

Mwananchi hawezi kupata picha kamili ya serikali kupitia mijadala ya kwenye vijiwe vya kahawa au vinginevyo bali ni katika mijadala ya Bunge. Ndio maana nasema Serikali lazima ihakikishe inaweka utaratibu wa kuhakikisha wananchi wanakuwa na taarifa juu ya kile kinachoendelea Bungeni bila ya kuwa na shaka yoyote juu ya taarifa hizo.Kwa mantiki hiyo serikali yetu ya Tanzania haina budi kurudisha urushaji wa moja kwa moja wa matangazo ya Bunge ambayo yamekuwa na hamasa kubwa katika taifa letu hadi kupelekea wananchi hususani vijana kutambua wajibu-jamii wao kwa taifa.

Hapo kale kati ya karne ya nne mpaka tano kabla ya kuja Kristo miji katika dola la Uyunani, iliweza kuizisimamia serikali zao kupitia mikutano iliyojuisha wananchi wote wa mji, katika kipindi hiko dola hiyo ya Uyunani na miji yake ilipata kushuhudia ustawi wa watu wake pamoja na maendeleo makubwa ya hekima (wisdom) kwa kuwa raia wake walikuwa watu wa kudadisi na kujenga hoja juu ya dola lao na maisha ya mwanadamu kwa ujumla. Katika mikutano hiyo ambayo wao waliita Ekklesia (The assembly) wananchi waliendesha mijadala mbalimbali kama vile kujadili vita na mahusiano na dola jirani, kupitisha kiwango cha kodi, kupitisha sheria na adhabu kwa wakosaji.

Nimetolea mfano wa miji ya Uyunani ya kale kwanza, kuonesha ni kwa jinsi gani taasisi za kidemokrasia zimeanza kipindi kirefu sana katika maisha ya binadamu lakini pili, nataka kuonesha ni kwa jinsi gani upo umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika mijadala inayohusu taifa lao hususani ile mijadala ya Bunge ambayo kimsingi ni yao ili kuweza kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo makubwa ya hekima kupitia uwezo wa kudadisi pamoja na ujenzi wa hoja zenye maslai mapana kwa taifa na maendeleo endelevu ya mwanandamu.

Kama nilivyosema awali, Mfumo wa demokrasia ya Uwakilishi hushuruti wengi wawachague wachache kwa niaba yao, hivyo basi wachache hao hawaachiwi hivi hivi tu hayo madaraka waliyopewa na wengi bali ni sheriti pia wengi hao (umma) lazima wafuatilie kinachoendelea kwenye mijadala hiyo ya wachache kwa manufaa ya wote.

Vivo hivyo kwa Bunge letu wananchi wanao wajibu wa kufuatilia mijadala ya Bunge lao ambapo kuna wawakilishi wao pasipo na shaka ya upataji wa taarifa juu ya Bunge hilo, ati kwa kigezo cha gharama urushaji wa matangazo labda iwe kwa makusudi ya kuwapora wananchi mamlaka yao ambayo ni kinyume na misingi demokrasia.

Pia ikumbukwe kwamba Tanzania ni moja kati ya mataifa yanayofuata utamaduni wa Mabunge wa Jumuiya ya madola ( Western minster ) ambapo Ushirikishwaji wa wananchi ni moja ya msingi na utamaduni wa Mabunge hayo.

Hivyo basi wito wangu kwa Serikali ni kwamba lazima ieshimu mgawanyo wa madaraka kwa kuacha kila mhimili kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba.Kwa Wananchi kwa ujumla, wahamasike kusimama na kutetea mamlaka yao kwa chombo chao cha Uwakilishi yaani Bunge ambacho ndicho chenye mamlaka ya kutunga sheria, kupitisha sheria na kuisimamia serikali katika utekelezaji wa majukmu yake katika taifa.

Wananchi wasisubiri mpaka vyama vya siasa hususani vya upinzani kuwasemea bali ni wajibu wao maana wasipokuwa thabiti kutimiza wajibu-jamii wao wataporwa mamlaka yao na kikundi cha watawala ambao kimsingi wanaona mamlaka kamili ya wananchi kwao ni kizingiti cha uendeshaji wa shughuli zao za kiutawala.

Chanzo: Rai
 
Back
Top Bottom