Jenerali Ulimwengu akiwa kwenye kongamano la kigoda cha mwalimu Nyerere chuo kikuu cha Dar es Salaam, amesema pamoja na hatua nzuri anazochukua Rais wa sasa, Mheshimiwa John Magufuli ambazo zimepongezwa lakini ukiangalia picha kubwa ni kwamba tumerudi nyuma kama miaka 50 kwenye demokrasia.
Ulimwengu amesema ni kutokana na kufinya uhuru wa kujieleza na hususan kwa kufinya uhuru wa wawakilishi wa wananchi ndani ya bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Ulimwengu ameendelea kwa kusema katika hili hamna kifimbo cha uchawi cha kujinasua isipokuwa mchakato wa katiba ambao ulichukua fedha nyingi kisha ukaachwa njiani na Mheshimiwa Kikwete.
Mwandishi huyo wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa ametaka Raisi mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuisababishia serikali hasara baada ya kutokuufanikisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.
Jenerali Ulimwengu alisema katika kipindi cha mchakato wa katiba mpya, fedha nyingi ambazo zilitokana na kodi za wananchi zilitumika katika shughuli mbalimbali lakini katiba mpya haikupatikana.
“Katika kipindi hiki tumeona viongozi mbalimbali waliopita wakichukuliwa hatua kwa kuisababishia serikali hasara… Kikwete anapaswa kufikishwa mahakamani kuelezea zile pesa za mchakato wa katiba zitarudi vipi,” alisisitiza.
Akijibu hoja hiyo, mwenyekiti wa mdahalo huo, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amesema wakati wa mchakato huo yeye hakuwa mshauri wa rais hivyo hawezi kulijibia suala hilo.
“Mimi sikuwahi kuwa mshauri wa raisi wala mshauri wa chama juu ya mchakato huo, ila niliombwa kutoa maoni kama wananchi wengine,” alisema Mkapa na kuongeza kuwa wasomi wanapaswa kufanya uchambuzi makini kabla ya kutoa hoja kwani kuna baadhi ya hoja hutolewa lakini sio muhimu kwa maendeleo ya taifa.