Je, Zitto Kabwe anatumiwa na Standard Chartered Bank?

Salim Khatri

Member
Mar 6, 2015
69
21
BLSlHmZCcAEKuQL.jpg

Zitto Kabwe akiwa na Balozi wa Uingereza Bi. Dianne Melrose mnamo Mei 2013.

Katika makala yangu ya “Uongo wa Taarifa ya Kamati ya PAC Kuhusu Sakata la Escrow” nimeonyesha udanganyifu mkubwa uliofanywa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya uenyekiti wa Mh. Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini. Uongo, udanganyifu na ulaghai uliokuwemo kwenye Ripoti ya PAC ni wa kiwango cha juu kabisa. Unaweza kuisoma makala hiyo pamoja na viambatanisho vyote vinavyojadiliwa kwenye makala hiyo kwa kuipakua hapa: Index of /escrow/viambatanisho

Leo napenda tujadili mkono wa Standard Chartered Bank (kwenye makala hii tutaifupisha kama“SCB”) kwenye sakata la Tegeta Escrow na uwezekano wa Zitto Kabwe kutumika na hii benki ya kimataifa kufikia malengo yake.

Awali ya yote ni muhimu tufahamu nafasi ya SCB kwenye sakata hili. SCB inadai kuwa tarehe 4 Agosti 2005 ilinunua ‘mkopo mbovu' kutoka kwa benki ya Danaharta ya Bumiputra nchini Malaysia. Mkopo huo wa benki ya Danaharta ndiyo mkopo waliochukua IPTL kujenga mtambo wa IPTL uliokuwa Salasala, Tegeta. SCB inadai kuwa ilinunua mkopo wenye thamani ya dola za Kimarekani millioni 125 kwa gharama ya dola za Kimarekani millioni 74. Yaani benki ya Danaharta iliamua kula hasara ya dola za Kimarekani 51 ili kuachana na deni hilo la IPTL lililowashinda.

SCB inadai kuwa masharti ya mkopo huo ni kuwa iwapo mdaiwa (IPTL) atashindwa kulipa mkopo basi benki inayodai itamilikishwa kampuni yote ikiwemo mtambo wa kufua umeme ulioko Tegeta pamoja na fedha za IPTL zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta. Sasa hivi SCB inahangaika kwenye mahakama mbalimbali duniani kujaribu kuthibitisha kuwa umiliki wa kampuni ya IPTL ni wa kwao wao SCB. Lakini kabla ya kuthibitisha umiliki wa IPTL, wanatakiwa waweze kuthibitisha uhalali wa deni wanalolidai, kitu ambacho kote wanapoenda wanagonga mwamba.

Katika harakati zao za kutakawalipwe fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kugonga mwamba mahakamani, SCB walikuja na mpango maalum waliouita “mpango uliokubaliwa” (waliouita Agreed Plan) wa kutatua hilo tatizo na kumuandikia barua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dr. Idris Rashid. Katika barua yao ya tarehe 22 Septemba 2009 waliishauri TANESCO itaifishe IPTL haraka iwezekanavyo. Na kama shauri la kutaifisha litakubalika na kutekelezwa basi:

(a) Mchakato mzima ufanyike kupitia Bunge la Tanzania. Kutakuwa hakuna haja ya kuzihusisha mahakama kwenye hili [la kutaifisha].

(b) Upande utakaostahiki kulipwa fidia kutokana na utaifishaji huu chini ya “Makubaliano ya Hull” itakuwa wao benki [yaani SCB].

(c) Benki [SCB] itakubali masharti ya “Agreed Plan” kama ni fidia kamili (final compensation). Benki [SCB] haitajaribu kulazimisha fidia nyingine za utaifishaji ambazo zimo kwenye vipengele vya mkataba wa utekelezaji uliosaniwa Juni 8, 1995 kati ya Serikali ya Tanzania na IPTL.

(d) Benki [SCB] inakubali kutokudai, katika ngazi yoyote, kuchukua hatua yoyote katika kesi yoyote ya ICSID dhidi ya TANESCO au Serikali ya Tanzani (aidha kwa jina lake ama kwa jina la IPTL ama vinginevyo) kwenye masuala yanayolalamikiwa sasa.

(e) Kutegemea muda itakapofikishwa Bungeni, “Agreed Plan” [ya kuitaifisha IPTL] unaweza kutekelezwa haraka bila ya haya ya Msimamizi ama mchakato wowote wa Mahakama.

(unaweza kuipakua na kuisoma barua hiyo hapa: http://www.orcis.com/escrow/Letter_SCB_to_TANESCO_CEO.pdf)

Baada ya kuelewa mkono wa SCB kwenye hili suala la Akaunti ya Escrow ya Tegeta na mpango wao waliokuwa nao ili kuweza kufanikiwa kupata fedha zilizokuwa kwenye hiyo akaunti, sasa tuangalie kidogo mamba yafuatayo:

(a) Kwanza kama walivyotaka SCB kwenye “Agreed Plan”, hili suala hatimaye lifikishwa Bungeni kupitia kwa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulilla na Zitto Kabwe wakitaka “Kamati Teule” iundwe kuchunguza hili suala na kulitolea hukumu.

(b) Serikali ikasisitiza hili suala lichunguzwe na PCCB pamoja na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG). Waakina Kafulila na Zitto walipinga sana hili suala kuchunguzwa na PCCB/CAG. Soma barua ya Kafulila kwa Mkurugenzi Mkuu wa PCCB wakitoa sababu kwanini hawataki hili suala lichunguzwe na PCCB/CAG. Barua hiyo inaweza kupakuliwa hapa: http://www.orcis.com/escrow/Letter_From_Kafulila_To_Hosea.pdf

(c) Baada ya CAG kuwasilisha ripoti yake Bungeni, alichotakiwa kufanya Zitto kama Mwenyekiti wa PAC ni kuwasilisha Ripoti ya CAG lakini badala ya kufanya hivyo wakaandika ripoti mpya kabisa na kuiweka Ripoti ya CAG pembeni. Waliwasilisha hii ripoti yao (Ripoti ya PAC) na kujengwa taswira kuwa walikuwa wanawasilisha Ripoti ya CAG. Yaani kazi iliyofanywa na CAG ikawekwa pembeni, wao PAC wakiongozwa na Zitto wakaja na ripoti ya uchunguzi wao waliofanya.

(d) Katika moja ya azimio lililopendekezwa kwa ajili ya kupitishwa na Bunge, lilikuwa lile la kuitaifisha IPTL, yaani vile vile walivyotaka SCB kwenye ile barua yao kwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO waliouita “Agreed Plan”.

Ni wazi kuwa SCB waliwatumia baadhi ya wanasiasa wa Tanzania kufikia malengo yao ya “Agreed Plan” na hatimaye mgogoro wa IPTL ulifikishwa Bungeni na vile vile kufanikisha kupata azimio la Bunge linalotaka kile kilichokuwemo kwenye “Agreed Plan” yaani “mtambo wa IPTL utaifishwe”. Ni wazi wale waliokuwa wanajulikana kama vinara wa sakata la Escrow Account ndiyo waliotumika katika kufanikisha azma hii ya SCB. Sasa tujaribu kuunganisha nukta (connect dots) kati ya SCB na Mh. Zitto Kabwe.

Mambo muhimu nayotaka kuyajadili ni haya yafuatayo:

(a) Madai ya SCB yanatetewa na Makala za Zitto
(b) Ripoti ya PAC imepindisha ukweli ili kuhalalisha madai ya SCB
(c) Alichoandika Zitto kwenye ukurasa wake wa Facebook (FB) kabla CAG hajakamilisha uchunguzi wake.
(d) Kukiri kwa Zitto kuwa alifuatwa na Balozi wa Uingereza akiwa na ujumbe wa SCB.

Tuyaangalie haya moja baada ya lingine.

Madai ya SCB Yanatetewa na Makala ya Zitto

Kabla hata CAG hajamaliza uchunguzi wake, Zitto alipata kuandika ‘Briefing Paper’ iliyoitwa “How Pan Africa Power Ltd acquired Independent Power Tanzania Ltd for almost Nothing and looted US$124m from the Bank of Tanzania”. Unaweza kuipakua hii paper hapa: http://www.orcis.com/escrow/Makala_Zitto_HowPAPAcquiredIPTL.pdf)

Katika paper hii, Zitto anadai kuwa yaliyomo ni mawazo yake na siyo ya PAC na mnamo tarehe 29 Julai 2014 aliiwasilisha ‘paper’ hiyo pamoja na ushahidi mwengine ukiwemo barua, hukumu, risiti za TRA na mengine kwa timu ya uchunguzi wa CAG. Pia akadai kuwa uchunguzi huo wa CAG uliamriwa na Kamati ya PAC mnamo tarehe 20 March 2014.

Ni muhimu kufahamu kuwa Uchunguzi uliofanywa na CAG chimbuko lake ni ombi kutoka kwa Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na ombi la Katibu wa Bunge baada ya mjadala mkali bungeni na kuamuliwa hivyo. Siyo kwa ombi/amri ya Kamati ya PAC kama anvyodai Zitto kwenye ‘paper’ yake. Anyway huo ni mjadala wa siku nyingine.

Katika ‘paper’ hiyo, Zitto anajaribu kuonyesha kuwa Bw. Harbinder Singh Sethi siyo mmiliki halali wa IPTL. Cha ajabu anashindwa kueleza kinagaubaga ni nani hasa mmiliki wa IPTL. Amejaribu kuonyesha kuwa SCB ni mdai halali wa IPTL na hata kujaribu kushawishi wasomaji wake kwa kuwafafanulia ni vipi deni la thamani ya dola za Kimarekani millioni 125 linaweza kununuliwa kwa dola za Kimarekani millioni 84 na kupata punguzo la dola za Kimarekani millioni 51. Pia anawaonea huruma SCB kuwa “To date, SCB-HK have not recovered a cent from IPTL” yaani “mpaka leo, SCB-HK hawajaweza kulipwa hata senti moja kutoka IPTL”.

Unajiuliza, hii huruma kwa SCB inatokea wapi?


Ripoti ya PAC imepindisha ukweli ili kuhalalisha madai ya SCB

Ripoti ya Kamati ya PAC (siyo Ripoti ya CAG) imejaribu kila njia kuonyesha kuwa SCB ina madai halali. Mojawapo ni hii hapa:

“Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba kumekuwa na mvutano juu ya uhalali wa madai ya SCB-HK ikielezwa kuwa matakwa ya kifungu Na. 79 (1) na Kifungu Na. 172 vya Sheria ya Makampuni CAP 212 (iliyorekebishwa mwaka 2002) hayakutimizwa kwa IPTL kutowasilisha makubaliano yaliyoingiwa kuhusu deni hili na dhamana zake 26, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amethibitisha uhalali wa madai ya SCB-HK kwa kuzingatia yafuatayo:

(a) Uamuzi wa Shauri Na. ARB/10/20 lililofunguliwa ICSID ulioeleza kuwa kutosajiliwa kwa makubaliano yenye maslahi ya dhamana “Security Interest” haiondoi uhalali wa deni dhidi ya Kampuni husika.
(b) IPTL ilikuwa ikifanya marejesho hata baada ya deni hilo kununuliwa na SCB-HK, ambapo hadi kufikia mwaka 2007 ilikuwa imelipa jumla ya USD 58.69 milioni na kati ya hizo USD 20 milioni zililipwa kwa SCB-HK.
(c) Hukumu ya tarehe 5 Septemba, 2013 ya Mahakama Kuu ya Tanzania ilirejesha IPTL kuwa Kampuni hai.”

Chanzo: Uk. 33 Ripoti ya PAC (http://www.orcis.com/escrow/Ripoti_Ya_PAC_(NakalaYaBunge).pdf)​

Ukisoma Ripoti ya CAG hakuna sehemu yoyote ambapo CAG amethibitisha uhalali wa madai ya SCB kama inavyodaiwa na kunukuliwa na hiyo Ripoti ya PAC hapo juu. Ripoti ya CAG inataja walichobaini (a) na (b) na hawakufikia hitimisho lolote la uhalali wa madai ya SCB. Kilichonukuliwa kama (c) hapo juu ni jaribio la kuminya kile kilichobainishwa na Ripoti ya CAG. Pamoja na hayo, hakunapopote kwenye Ripoti ya CAG inapodai kuwa hicho kilichobainishwa ni uthibitisho wa uhalali wa madeni ya SCB. Huu ni UONGO uliotungwa katika harakati za kutoa uhalali wa madai ya SCB. Soma Section 2.7.1 ya Ripoti ya CAG “Madai ya Standard Chartered Bank Hong Kong (SCBHK)” utaona kile walichoandika CAG na namna PAC walivyopindisha maneno ya CAG kuhalalisha madai ya SCB.

Unajiuliza ni kwanini Kamati ya PAC ilidiriki kupindisha taarifa za CAG kuipa uhalali SCB? Kwa manufaa ya nani zaidi ya SCB? Kwani Kamati ya PAC na Mwenyekiti wake walipindisha ukweli na kuandika uongo huu?


Alichoandika Zitto kwenye FB kabla CAG hajakamilisha uchunguzi wake.

Katika ukurasa wake wa Facebook (Zitto Kabwe - Mapya IPTL: $250m zimetokaje BoT ? Nimesoma... | Facebook), Zitto Kabwe aliandika hivi:

“Mwaka 2006 Rais Jakaya Kikwete aliagiza kwamba, ili kumaliza kabisa suala la mkataba wa kuuziana Umeme wa IPTL, mitambo ya kampuni hiyo ichukuliwe na Serikali. Mwaka 2006, 2007 na 2008 Kamati ya BUNGE ya Nishati na Madini imekuwa ikitoa maagizo hayo hayo kuhusu suala la IPTL. Mwaka 2009, Aprili 30 Kamati ya Bunge ya POAC ilipeleka mapendekezo bungeni kwamba IPTL ichukuliwe na serikali na fedha zilizopo katika escrow account zitumike pia kubadili mtambo ule kutoka mafuta mazito kwenda kutumia Gesi Asilia. Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge na POAC ikatoa maelekezo maalumu kwa Gavana wa Benki Kuu kuwa fedha zilizopo escrow account zisitumike kwa namna yeyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa ili itumie Gesi Asilia.”​

Yaani paragraph hiyo nzima inajaribu kuonyesha ni vipi Rais, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, na Kamati ya POAC zimekuwa zikijaribu KUAGIZA mtambo utaifishwe kama wanavyotaka SCB kwenye barua yao tuliyoijadili hapo juu.

Unajiuliza kwanini azma ya SCB kwenye “Agreed Plan” ndiyo hicho hicho kinatiliwa mkazo na maandishi ya Zitto?


Kukiri kwa Zitto kuwa alifuatwa na Balozi wa Uingereza akiwa na ujumbe wa SCB.

Katika hotuba yake ya majumuisho, Zitto Kabwe alisema haya:

“Leo kuna baadhi ya wabunge wanahoji kuwa labda tunatumwa na Uingereza. Huyu Chikawe ni shahidi. Balozi wa Uingereza alikuja na delegation yake ya watu wa Standard Chartered kuniona kama Mwenyekiti wa POAC ku-lobby kwamba tuwaachie Standard Chartered wachukue hela za Escrow. Nikatoka nje ya kikao nikampigia simu Chikawe, wakati huo ni Waziri wa Justice, nikamwambia Chikawe hawa wanavunja diplomatic protocol, hawawezi kuja kwa Mwenyekiti wa Kamati hawana kibali cha Wizara ya Mambo ya Nje, wanakuja ku-lobby. Chikawe ni shahidi yangu akatae hapa, anikane. Hamna kingine kilichonituma kufanya hivyo, ni uzalendo kwa nchi yangu. Kwa hiyo, siwezi kuwajibu watu ambao kwa njia moja ama nyingine wameniparuraparura, siwezi kuwajibu; siwezi kuwajibu hata kidogo kwa sababu hawajui nini nilichokifanya kwa nchi hii.”

Chanzo:


Kuna vitu kadhaa vya kuzingatiwa kwenye haya madai ya Zitto.

(a) Protokali za kikiplomasia zinavunjwa, kwanini aliamua kuripoti kwa waziri wa sheria na siyo waziri wa mambo ya nchi za nje anayeshughulika na masuala ya kidiplomasia?

(b) Je malalamiko yake kwa Waziri wa Sheria yalichukuliwa hatua gani?

(c) Kwa sababu alitoka nje ya kikao (ina maana tayari walikuwa kwenye kikao) kwa hasira na uzalendo, je yeye alichukua hatua gani zaidi kuhakikisha Balozi wa Uingereza na ujumbe wa SCB wasiweze kufanikisha azma yao ya “kuziiba” zile pesa kama anavyodai?

(d) Katika utetezi wake dhidi ya tuhuma za kutumiwa na SCB ambazo aliziweka kwenye Blogg yake, Zitto hakutaja hili kulizungumzia hili la kufuatwa na Balozi wa Uingereza akiwa na ujumbe wa SCB. Kwanini hakufanya hivyo wakati huu ni utetezi mzuri zaidi? Unaweza kusoma utetezi wa Zitto Kabwe hapa: Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema “Hatutetereki”

(e) Katika Ukurasa wa 31 wa makala ya Zitto “How Pan Africa Power Ltd acquired Independent Power Tanzania Ltd for almost Nothing and looted US$124m from the Bank of Tanzania” anaelezea kuwa aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini alimtuhumu balozi wa Uingereza Diana Melrose kuipigia debe SCB kwenye hili sakata. Kwanini Zitto kwenye hiyo makala yake hakutaja popote kuhusiana na kufuatwa na balozi wa Uingereza akiwa na ujumbe wa SCB? Kwanini kwenye Ripoti ya PAC, hili la kufuatwa na balozi wa Uingereza halikutajwa popote?

(f) Alipowasilisha makala yake na vielelezo vya ushahidi kwa kamati maalum ya CAG, kwanini hili la kufuatwa na Balozi wa Uingereza hakuliripoti?

(g) Kama alitoka kwenye kikao hicho cha Balozi wa Uingereza na ujumbe wa SCB, kwanini anaendelea kuitetea SCB kwenye sakata hili na hata kutaka kile kilichokuwa kwenye mpango maalum wa SCB ulioitwa “Agreed Plan”?

Unajiuliza kwanini hii ya kufuatwa na balozi wa Uingereza aliifanya siri na akaendelea kuifanya siri hata baada ya kuitoboa kwenye Bunge? Je ulimi usiokuwa na mfupa uliteleza siku ile Bungeni?
 
Sina uhakika kama hutumiwi na Ruge maana kuna uzi humu unao onyesha alivyo nunua kila anaye nunulika akiwemo mkurugenzi wa Takukuru
Kitu ambacho umekwepa kufafanua ni lini na wapi Singasinga alinunua IPTL na alimlipa nani
Kama SCB haihusiki je wale waliobeba fedha kwa viroba Stanbic wanahusikanaje?
Kwa taarifa yako kazi ya balozi ni kufutilia maslahi halali ya taifa lake na wananchi wa kwao
 
Sijawahi kumuamini Zitto.. Huyu jamaa kapiga sana hera wakati akiwa mwenyekiti wa PAC
 
Kwa akili yako unataka kusema kitilya, sioi na yule miss wanaonewa?. Kweli hii Ndio bongo.
 
Maelezo mengi sana ila sisi wananchi wa kawaida ugomvi wetu na Escrow ni kwamba ilithibitika baadhi ya viongozi wa serikali wamepata mgawo wa pesa... tena ni mabilioni na mamiliomi ya shilingi....

Inawezekana uyo Zitto anatumika na iyo benki ya Uingereza ila ingekua vizuri zaidi ukafafanua ni vipi zile pesa walizochota akina Mh.Chenge na Tibaijuka zilihusika na hili sakata la Escrow....

Hii ni siasa kila jambo lina sura mbili mbili... hatuwezi kumhukumu Zitto kwa "unafiki" au sijui upotoshwaji wa taarifa ya kamati yake kipindi iko Halafu tukaacha kujiuliza hivi ilikuaje wale viongozi wakaingiziwa zile pesa katika akaunti zao???
 
Ulicho kiandika hakina chembe yoyote ya Uongo!! Zitto ni mwanasiasa mpiga Smart sana. Zitto ni mtu wa maslai sana refer NSSF saga
 
Khatri, Khatri kama una ugomvi na Zitto pambana nae kwa njia nyingine, njia hii umeshindwa. Katika maelezo yako yote haya umeshindwa kabisa kueleza ni jinsi gani SCB ingelipwa fidia endapo mitambo ya IPTL ingetaifishwa. Hoja ya Zitto na ni kuwa kihalali hakuna mmiliki wa IPTL kwani imegundulika wamiliki wake "hawa exist, hawapo", hivyo serikali ichukue mitambo ya matapeli waliojificha. Hoja ya SCB ni kuwa ilinunua deni la kampuni mufilisi ambapo wakapata nafasi ya kumiliki madeni na mali ikiwemo akaunti ya ESCROW. Anachopigania Zitto na wanachopigania SBC ni vitu viwili tofauti. Zitto anapigania matapeli wanaojifanya wamiliki wa IPTL ambao 'hawapo' wasiendelee kulipwa mabilioni ya pesa kila mwezi na pia taifa litaifishe mitambo ya matapeli hawa wakati SCB wao wanahangaika kwenye mahakama za kimataifa kutafuta umiliki wa IPTL. Wewe unasemaje SCB wanataka kupata umiliki wa IPTL kwa maana ya 'fidia' kupitia bunge? Kwa nini kila siku unataka ripoti ya uchunguzi wa PAC ifanane na ripoti ya CAG? Kama hivyo ndio lilikuwa lengo wewe unafikiri kulikuwa kuna haja gani ya kuipa PAC mamlaka ya kwenda kuchunguza nakuongezewa nguvu na wabunge kadhaa? Unamtetea nani Harbinder Singh? Una ugomvi na Zitto? Lengo lako hasa ni nini? Kwa malengo yawayo yote, nenda kafanye 'summary' ya unachotaka kusema ili upate mawazo zaidi kwani si kila mtu atakuwa na muda wakusomahaya maelezo yako yasioumana yenye kulazimishakuelekea sehemu fulani japo pia kwa kufanya hivyo umejikanganya vibaya mno. Ingekuwa mahakamani ushahidi wako ungeonekana ni wa uongo na ungetumika dhidi yako kwa kuiongopea mahakama.
 
Khatri, Khatri kama una ugomvi na Zitto pambana nae kwa njia nyingine, njia hii umeshindwa. Katika maelezo yako yote haya umeshindwa kabisa kueleza ni jinsi gani SCB ingelipwa fidia endapo mitambo ya IPTL ingetaifishwa. Hoja ya Zitto na ni kuwa kihalali hakuna mmiliki wa IPTL kwani imegundulika wamiliki wake "hawa exist, hawapo", hivyo serikali ichukue mitambo ya matapeli waliojificha. Hoja ya SCB ni kuwa ilinunua deni la kampuni mufilisi ambapo wakapata nafasi ya kumiliki madeni na mali ikiwemo akaunti ya ESCROW. Anachopigania Zitto na wanachopigania SBC ni vitu viwili tofauti. Zitto anapigania matapeli wanaojifanya wamiliki wa IPTL ambao 'hawapo' wasiendelee kulipwa mabilioni ya pesa kila mwezi na pia taifa litaifishe mitambo ya matapeli hawa wakati SCB wao wanahangaika kwenye mahakama za kimataifa kutafuta umiliki wa IPTL. Wewe unasemaje SCB wanataka kupata umiliki wa IPTL kwa maana ya 'fidia' kupitia bunge? Kwa nini kila siku unataka ripoti ya uchunguzi wa PAC ifanane na ripoti ya CAG? Kama hivyo ndio lilikuwa lengo wewe unafikiri kulikuwa kuna haja gani ya kuipa PAC mamlaka ya kwenda kuchunguza nakuongezewa nguvu na wabunge kadhaa? Unamtetea nani Harbinder Singh? Una ugomvi na Zitto? Lengo lako hasa ni nini? Kwa malengo yawayo yote, nenda kafanye 'summary' ya unachotaka kusema ili upate mawazo zaidi kwani si kila mtu atakuwa na muda wakusomahaya maelezo yako yasioumana yenye kulazimishakuelekea sehemu fulani japo pia kwa kufanya hivyo umejikanganya vibaya mno. Ingekuwa mahakamani ushahidi wako ungeonekana ni wa uongo na ungetumika dhidi yako kwa kuiongopea mahakama.
Umeandika Vyema sana,

Hoja Ya Zitto na Ambyo Kimsingi Inaegemea katika utata wa Umiliki wa IPTL,Bdo imesimama kwani kimsingi kutaifishwa ndio Suluhisho.

Mtoa mada tokea Mwanzoni mwa sakata hili alichukua upande na Pengine anasukumwa na Maslahi Binafsi.
 
zito sio mtu wa kuaminika kabisa
JF nayo imejaa kweli. Zitto anakuwa sio mtu wa kuaminika anapoiumbua serikali katika wizi.
Ila akikosana na wapinzani wenzie kwa kupishana kauli anaitwa Mwanasiasa mahiri na mpinzani wa kweli. Na kauli hizo tofauti zinatoka kwa watu walewale tena unaweza kukuta ni ndani ya siku moja ila thread tofauti
 
nimejaribu kusoma mstari baada ya mstari lakini sioni matiki yako ya kumuhusisha Zitto na SCB.
Maana sababu zilizotolewa za kuitaifisha mitambo ya IPTL ni tofauti kabisa na sababu unazotaka kutuaminisha.

Kama tukataifisha Hizo mitambo kwa makosa mengine(kama tulivyoelezwa bungeni) sio hayo unatyotaka kutuaminisha (agreed plan), Ikagundulika kuwa pia SCB wanawadai kihalali IPTL hizo dolari, Itabidi IPTL wao ndio watafute pesa za kwalipa maana hizo mitambo hazitakuwa zao tena.

Hueleweki kabisa mkuu labda ufupishe na uende kwenye point kabisa. Maana naona bado dots zako zinaungana at infinity.

Simuungi mkono zitto kama kweli anahusika tutamtumbua tu lakn kwa hoja hizi hakuna substance kabisa.

Mtazamo wangu.
 
  • Thanks
Reactions: BAK
Mimi simtetei zitto,lakini mbona na wewe husemi unatumiwa na IPTL? Mbona hujacopy kuonyesha ripoti ya CAG ilisemaje?Nani hajui kuwa IPTL imeibia nchi hii fedha nyingi sana kwa kupitia mkataba tata walioingia na Tanzania?Acha kutufanya wajinga kuja kutaka huruma yetu mfanikishe mambo yenu..
 
Sina uhakika kama hutumiwi na Ruge maana kuna uzi humu unao onyesha alivyo nunua kila anaye nunulika akiwemo mkurugenzi wa Takukuru
Kitu ambacho umekwepa kufafanua ni lini na wapi Singasinga alinunua IPTL na alimlipa nani
Kama SCB haihusiki je wale waliobeba fedha kwa viroba Stanbic wanahusikanaje?
Kwa taarifa yako kazi ya balozi ni kufutilia maslahi halali ya taifa lake na wananchi wa kwao

Hao waliobeba fedha kwenye magunia na mifuko ya Rambo kutoka benki ya Stanbic mimi siwajui kwani hawajatajwa kwenye Ripoti ya CAG wala ile Ripoti ya kisanii ya PAC. Wewe kama unawajua kwanini usiwataje?
 
Back
Top Bottom