Ipi Historia ya Kweli ya Chama Cha TANU?

Ipi Historia ya Kweli ya Chama Cha TANU?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
22,455
Reaction score
32,981

View: https://youtu.be/Zv8eSKAM4cU?si=jpAWzFbsa1qG--wS

IPI HISTORIA YA KWELI YA CHAMA CHA TANU?

Nimeweka historia nne za kuasisiwa kwa chama cha TANU.

Kuna historia ya TANU inayoanza na Mwalimu Julius Nyerere akiunda TANU ndani ya Misheni ya Kanisa Katoliki Tosamaganga, Iringa.

Kuna historia ya TANU ya Mwalimu Nyerere kufuatwa Francis College Pugu alipokuwa akifundisha aje mjini Dar es Salaam kuunda TANU.

Kuna historia ya TANU ya Mwalimu Julius Nyerere kuunda TANU Mwananyamala nyumbani kwa Mzee Mwinjuma Mwinyikambi.

Kuna historia ya TANU inayoanza nyumbani kwa Hamza Mwapachu, Nansio Ukerewe mwaka wa 1953 kwa mazungumzo kati yake na Abdul Sykes na Ali Mwinyi Tambwe kujadiliana na kukubaliana kumwingiza Julius Nyerere katika nafasi ya juu kabisa katika TAA na baada ya kufanikiwa katika hilo TANU iundwe mwaka unaofuatia 1954 na Mwalimu Nyerere aongoze harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Historia hii inaelezwa kwa wakati tofauti na Juma Mwapachu mtoto wa Hamza Mwapachu (1913 - 1962) na Aisha ''Daisy'' Sykes mtoto wa Abdul Sykes (1924 - 1968).

Juma Mwapachu anaeleza:

''Bado nakumbuka kwa uyakinifu.

Nilikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu na pamoja na kaka yangu Bakari tulilala sebuleni kuwachia chumba chetu wageni wawili, Abdul Sykes na Ali Mwinyi Tambwe Katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika).

Abdulwahidi alikuwa Rais wa TAA na uongozi wa TAA pamoja na wanaharakati wa siasa wengi wao wakiwa waislam walitaka Abdul Sykes abaki kuwa Rais.

Abdulwahid alikuwa tayari kumuafiki Hamza katika suala hilo katika ukweli kuwa ni Hamza ndiye aliyemtambulisha Nyerere kwa uongozi wa TAA Dar es Salaam mwaka 1949 kabla Nyerere hajaondoka kwenda Chuo Kikuu Edinburgh, Uskochi.''

Aisha ‘’Daisy’’ Sykes anaeleza:

''...nyumbani kwetu milango ilikuwa wazi siku zote kwa wageni.

Hivi ndivyo tulivyokuwa na wageni kutoka kila kabila, uwezo na hali tofauti.

Wageni mashuhuri waliokuwa wakija nyumbani ni pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle, Machifu Abdiel Shangali, John Maruma kutoka Moshi, Adam Sapi Mkwawa kutoka Iringa, Kidaha Makwaia kutoka Usukuma, Abdallah Fundikira, Harun Lugusha kutoka Tabora, Humbi Ziota kutoka Nzega, Michael Lukumbuzya kutoka Ukerewe na Patrick Kunambi kutoka Morogoro na wengine wengi.

Hawa machifu kwa kawaida walikuwa wakija na wake zao, wanawake warembo ambao hawakuacha kunifanya mimi kuwashangalia. Nakumbuka katika machifu wale, alikuwapo chifu mmoja na wa pekee mwanamke - Mwami Theresa Ntare kutoka Kasulu Kibondo.

Katika hali kama hii iliyokuwa tabu kufahamika, tukiwa watoto tulipata kujua maisha ya jamii nyingine, lugha zao, utamaduni wa makabila mengi ya Tanganyika kabla ya watu wengi kutoka sehemu nyingine za pwani hawajajua chochote kuhusu watu hawa.

Lakini aliyeshika nafasi ya juu kabisa katika fikra zangu nikiwa mtoto alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni kupitia kwake ndipo tukapata kujua kwa mara ya kwanza kuwa kuna kabila linaitwa, ‘’Wazanaki.’’

Kila alipokuwa anakuja nyumbani kwetu kuja kwake kulikuwa jambo maalum kulikosababisha minong’ono watu wakizungumza kwa sauti za chini wakipeana taarifa kuwa, ‘’Nyerere anakuja au keshafika.”

Kwangu mimi hii ilikuwa ishara ya kutimiza kazi yangu kwani siku zote nilikuwa nikiambiwa kutengeneza kifungua kinywa cha chai na mayai kila alipokuja nyumbani akitokea Shule ya Mt. Francis,Pugu alipokuwa akisomesha.

Nakumbuka katika akili yangu ya kitoto kumuona Mwalimu Nyerere akiishi nyumbani kwetu kwa muda katika nyumba yetu ya Mtaa wa Stanley baada ya kuacha kazi wakati marafiki zake wa karibu baba na Dossa Aziz walikuwa wanamtafutia nyumba ya kuishi.

Nyumba yetu ya Stanley kwa kuwa ilikuwa kwenye makutano ya barabara mbili ilikuwa na mjengo wa kipekee kwa nyakati zile.

Nikiwa mtoto nakumbuka sana vipi baba akishughulishwa na kutaka kuona kuwa Mama Maria na watoto wake hawakosi chochote kuyafanya masiha yao kuwa mepesi, ya starehe na furaha akihakikisha chakula kinapelekwa dukani kwa Mama Maria kila siku katika duka lake dogo lilikuwapo Mtaa wa Livingstone kona na Mtaa wa Mchikichi, hiki kikiwa kielelezo chake kikubwa kabisa cha huruma na ukarimu wake.

Nimesikia mazungumzo mengi wakati baba na wenzake walipokuwa wakijadili majina na shughuli ambazo hawa akina mama walikuwa wahusishwe ili kuleta mvuto wa kisiasa katika mikutano yao ya TANU.

Hawa wanawake ndiyo waliomsaidia Mama Maria kufungua hilo duka lake dogo pale Mtaa wa Livingstone kona na Mchikichi, mahali ambako Mama Maria alishinda kutwa nzima akiuuza duka lake.

Nikiwa mtoto nakumbuka kwenda kwenye duka lile kila siku mchana kupeleka chakula kwa Mama Maria, ambako hapakuwa mbali kutoka nyumbani kwetu.

Kwa kuwa baba alikuwa anataka ratiba hii yake ya chakula ifuatwe sawasawa kwa wakati wake, wakati mwingine hii ilikuwa changamoto kubwa sana kwa mama yetu, Bi. Mwamvua bint Mrisho.''

Mama Maria yu hai anaweza kuulizwa ukweli wa historia hii ya Abdulwahid Sykes na Julius Nyerere kwani kadi ya TANU ya Abdul Sykes ni No. 3, kadi ya Ally Sykes ni No. 2 na ya Julius Kambarage Nyerere ni No. 1.

Kadi hizi zote ziliandikwa na Ally Sykes.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom