Hutuba ya rais Wa ukawa

Hutuba ya rais Wa ukawa

A2theb

Member
Joined
Feb 15, 2014
Posts
16
Reaction score
3
HOTUBA YA MGOMBEA URAIS
KUPITIA CHAMA CHA CHADEMA
NA UKAWA MH. EDWARD
NGOYAI LOWASSA YA KUZINDUA
ILANI NA KAMPENI YA
UCHAGUZI MKUU
Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOSTI 2015
Ndugu Wana Dar es salaam na Watanzania
wenzangu
Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya miaka ishirini
na tano tangu mfumo wa vyama vingi
urejeshwe, vyama vya upinzani wa CHADEMA,
CUF, NCCR na NLD umeungana chini ya Umoja
wa Katiba ya Wananchi kupigania uchaguzi
mkuu wa mwaka huu na kuwa na mgombea
mmoja katika ngazi zote.
Miaka zaidi ya hamsini ya utawala wa serikali
za CCM na waasisi wake, umekuwa utawala wa
wachache walio hodhi madaraka na mali za
nchi.
Leo tunaanza safari ya uhakika ya kuleta
mabadiliko ya kweli nchini.
Mabadiliko yaletayo neema na kujenga upya
mfumo wa uchumi, haki na sheria nchini.
Mabadiliko ya kuimarisha huduma za jamii kama
elimu, afya, maji na makazi.
Mabadiliko ya kuondoa umaskini.
Mabadiliko tunayatoahidi ni mabadiliko ya
kurejesha matumaini kwa Watanzania kwa
kubadili hali zao za maisha.
Kila mwaka hali na ubora wa maisha ya
Watanzania imeshuka wakati tunaambiwa kuwa
pato laTaifa linakuwa.
Lakini Watanzania wanachotaka siyo takwimu
bali kuona kipato chao kinakua, shule, hospitali
na barabara bora zinajengwa.
Wanataka kupata maji safi na salama ya
kunywa. Wanataka makazi bora.
CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira ya kuleta
mabadiliko ya kweli ili kuona azma ya
Watanzania tangu uhuru ya kuondoa umaskini,
maradhi,na ujinga inahitimishwa.
Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye mabadiliko ya
fikra, uongozi, sera na utendaji.
Leo Tanzania inakabiliwa na changamoto nyingi
za ki-uchumi, kisiasa na kijamii. Changamoto
hizi ni matokeo ya sera za utawala wa Chama
kimoja wa miaka hamsini. Sote ni wahanga wa
siasa na sera hizi.
Miaka Hamsini ya CCM imetosha. Tunataka
mabadiliko na siyo ahadi zile zile kila mwaka
Tusidanganyike, CCM hawana jipya
Chagueni UKAWA wenye dira ya kubadili maisha
ya wananchi.
Mimi ninauchukia umaskini na mimesimamia
maendeleo kwa vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu
nilijaribu kubadili hali hii. Nilisimamia ujenzi wa
shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Nilihakikisha mikataba mibovu ya maji inavunjwa
na sasa wananchi wa kanda ya ziwa wanapata
maji safi.
Ndugu watanzania
CCM wanauliza tuna mpango gani wa kumaliza
umaskini. Sisi hatuahidi tu. Tutatenda.
Ilani yetu ni dira ya kuondoa umaskini kwa
mikakati sahihi na siyo nadharia.
Mkakati wa kuondoa umaskini si wa sekta kwa
sekta bali wa sekta zote kwa pamoja. Ni ujumla
wa utendaji na utekelezaji wa sera za kila sekta
utakao leta maendeleo.
Mkakati wangu na UKAWA wa kuondoa umaskini
utakuwa na nguzo tano:-
Kupunguza matumizi ya serikali na mashirika
yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji.
Kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na
misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi
inawekeza katika sekta muhimu na inapata
gawio halisia kutoka wawekezaji
Kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu
ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na
uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo,
viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa
wanyonge.
Kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya,
maji na makazi, na mazingira
Kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na
sheria chini ya Katiba ya Wananchi.
Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa
kuondoa umaskini, serikali yangu itafanya
yafuatayo:-
ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA
Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema tena leo.
Elimu kwanza, Elimu kwanza, Elimu kwanza.
Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi utakuwa
kutoa Elimu itatayogharamiwa na serikali kwa
kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi Chuo
Kikuu na pia:-
Kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi
inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani
katika soko la ajira.
Ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu
ikiwa ni pamoja na shule za Kata.
Kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote
nchini.
Kuimarisha taaluma na mitaala katika mashule.
Kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za
wanafunzi.
Kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu
ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya
kufundishia, usafiri na zana za teknolojia.
Kufuta michango ya maabara ya shule za kata
AFYA
Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa
kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya
hifadhi ya jamii
Tutaimarisha afya ya msingi pamoja na kinga
kupunguza gharama za tiba.
Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji
wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili
kuleta tija na huduma stahiki.
Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na
kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma
za afya karibu na jamii na pia kuepukana na tiba
za nje ya nchi.
Tutarejea kwa lengo la kuboresha maslahi na
vitendea kazi katika sekta ya Afya ikiwa ni
pamoja na nyumba na usafiri.
Tutathibiti ongezeko la gharama za huduma za
afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji huduma
za afya kama vile serikali na hospitali za sekta
binafsi.
ARDHI, MAJI NA KILIMO
Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa
Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi hasa
kati ya wakulima na wafugaji.
Tutapima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha
vijiji na wakulima kwa hati za serikali ili kuipa
thamani.
Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa kuimarisha
elimu, ufundi na teknolojia ya kisasa na
kumkomboa mkulima kutoka jembe la mkono.
Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa
na kuunganisha sekta hizo na ya viwanda.
Kuhakikisha kuwa wananchi wanatunza na
kulinda vyanzo vya maji.
Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa
wakulima elimu na mikopo ya riba nafuu ya
kuvuna maji na kujenga miundombinu husika.
Tutaweka mazingira rafiki yatakayomhakikishia
kwa kila Mtanzania kupata maji safi na salama.
Kumaliza kero za maji nchini kutamkomboa
mwanamke kutokana na adha ya kuchota maji
kwa kichwa
Nitafuta kodi zote za mazao na mifugo kwa
wakulima na wafugaji.
Tutasimamia kilimo cha biashara
kinachozingatia maslahi ya nchi na ya
Watanzania.
Tutaanzisha programu maalum ya kufufua
mazao asilia ya Tanzania hususan mkonge.
Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya Ufugaji na
Uvuvi.
MIUNDOMBINU
Tutaboresha bandari zilizopo na kujenga mpya
kama vitega uchumi vya Taifa ili kurejesha
biashara tulizopoteza kwa bandari za nchi jirani.
Tutajenga barabara nchini kwa kuzingatia ubora
hasa zile za vijijini.
Tutajenga reli ya kati kwa viwango vya kisasa
Tutajenga shirika la Ndege la Taifa
linalojiendesha kwa misingi ya faida.
Tutajenga miundombinu ya kisasa na kuondosha
misongamano ya magari hasa katika majiji ya
Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Arusha
Tutaimarisha uzalishaji na usambazaji wa
umeme vijijini ili kufikia zaidi ya asili mia sabini
na tano ya Watanzania
VIWANDA
Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa mhimili wa
uchumi kwa uzalishaji wa bidhaa na ajira
endelevu
Tutajenga viwanda vipya vya kusindika mazao
ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka mitano mali
ghafi zote za Tanzania zinasindikwa kabla ya
kusafirishwa nje ili kuongeza mapato na ajira ya
mamilioni ya vijana.
Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa Viwanda
UCHUMI
Tutabadili mfumo wa Uchumi wa nchi ili
kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi wa
Tanzania unakuwa ni wa soko-kijamii ambapo
nguvu za soko zitatumikia jamii kwa serikali
kuweka uwiano wa mapato unaohakikisha
huduma za kijamii zinapatikana kwa ufanisi.
Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za ndani kwa
kuwapa Watanzania upendeleo wa maksudi kwa
kipindi cha mpito ili waimarike na waweze
kuhimili ushindani. Tutawapa wafanyabiashara
wetu upendeleo katika manunuzi ya serikali na
kuwajengea mazingira mazuri ya biashara na
kodi endelevu.
Tutawawezesha Watanzania kupata mitaji ya
biashara kwa masharti nafuu kabisa.
Tutavutia uwekezaji na wawekezaji wenye tija.
Kuweka udhibiti wa wahamiaji wasioleta tija
wala maslahi kwa Taifa.
Tutaimarisha sera ya ubia baina ya Serikali na
Sekta binafsi kwenye maeneo muhimu ya
kiuchumi na kibiashara. Pia, kuwawezesha
Watanzania kuwekeza kwa njia ya ubia na
wawekezaji wenye mitaji mikubwa bila kujali
wanapotoka.
Tutaimarisha usimamizi kwa kubadilisha mfumo
wa Vyama vya Ushirika nchini ili utokane na
uendeshwe na wakulima wenyewe ikiwa na
pamoja na kuwawezesha kuboresha makazi kwa
mpango wa kushirikiana kujenga nyumba bora
Tutaanzisha na kuwezesha uanzishaji wa
viwanda vidogovidogo vinavyotoa ajira kwa wingi
kwa kuvihusisha na vyuo vya ufundi na benki
maalum kwa lengo hilo.
AJIRA
Tutasimamia swala la ajira hasa kwa vijana kwa
kukuza elimu ya ufundi ili waweze kujiajiri
Tutazipa kipaumbele sekta zinazozalisha ajira
kwa wingi hasa za viwanda, kilimo, ufugaji,
uvuvi na utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili zikue
kwa haraka.
Tutawapa wawekezaji wakubwa katika sekta hizi
upendeleo maalum na viwango vya kodi nafuu.
NISHATI NA MADINI
Serikali itashiriki kikamilifu katika uzalishaji wa
nishati
Itatengeneza mazingara mazuri ya kisera
yatakayovutia na kuwezesha ushiriki wa
Watanzania na ubia kati yao na wageni.
Serikali yangu itaupa uzalishaji mkubwa wa
umeme wa maji kipaumbele namba moja,
umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba
mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba
tatu na umeme wa urana kipaumbele namba
nne.
Serikali itatoa vipaumbele muhimu kwenye
usambazaji wa huduma kubwa ya umeme
sehemu za uzalishaji uliyolenga masoko ya
ndani, ya nchi jirani na ya nchi za kigeni.
Itapitia upya mikataba yote mikubwa ya nishati
na madini ili kubaini iliyo mibovu na kuifanyia
maboresho.
Serikali yangu itatumia sehemu ya hisa zake
kwenye raslimali kubwa ya gesi asilia
iliyopatikana hapa nchini kama rehani kwenye
kujichukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa
miundo mbinu ya mabomba ya gesi.
Serikali itatoza kodi na ada ndogo zaidi kwa
wazawa wenye ubia kati yao na wageni kuliko
zitakazotozwa kwa wageni wasiowekeza kwa
kushirikisha wazawa.
Serikali itasitisha utoaji wa misamaha ya kodi
isiyo lazima kwenye sekta ya madini, na badala
yake itawekeza kwenye kuongeza thamani ya
raslimali zake za madini.
Tutakuza nishati mbadala kutamkomboa
mwanamke kutokana na adha ya kukata kuni
MALIASILI NA UTALII
Tutasimamia uvunaji na matumizi ya rasilimali
za Taifa kwa manufaa ya kila Mtanzania wa
kizazi hiki na kijacho
Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha utunzanji
wa hifadhi za taifa na mazingira
Tutachochea ujenzi wa miundombinu ya utalii
nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mahoteli na
kuimarisha mafunzo
Tutaongeza idadi ya watalii kufikia milion mbili
ifikapo 2020.
UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA
USALAMA WA RAIA
Tutasimamia Katiba mpya inayolinda haki za
msingi za wananchi na kuweka bayana mipaka
ya madaraka ya serikali na viongozi, Bunge na
Mahakama.
Tutasimamia haki za raia na kuangalia upya
sheria kandamizi ili wananchi kama Masheik wa
Zanzibar hawasoti jela kwa sababu za kisiasa.
Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya Polisi hasa
wapelelezi na waongoza mashtaka ili wapate
uwezo wa kusimamia utoaji wa haki.
Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na usalama
nyenzo na kuboresha mazingira yao ya kazi na
maslahi
UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI
Tutajenga uzalendo ili kila Mtanzania aweze
kutathmini mchango wake kwa taifa kila siku
Tutaimarisha nidhamu, utendaji na uwajibikaji
katika Sekta ya Umma
Tutaimarisha mchango wa Wataalam wetu,
wanawake na vijana katika kusimamia uchumi
na kuwajengea mazingira stahiki ya kazi pamoja
na mafao.
Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu katika sekta
ya Umma na binafsi
Tutadhibiti na kupunguza matumizi ya serikali
ikiwa ni pamoja na kufuta safari za watumishi
serikalini zisizokuwa muhimu pamoja na zile za
Rais na kupiga marufuku matumizi ya
mashangingi serikalini.
Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza na ukaguzi
wa madeni ya serikali ili kuhakiki jinsi
yalivyotumika
Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri katika
shughuli za serikali na kuweka bayana mikataba
yote ya nchi ikiwa ni pamoja na ile ya mafuta,
madini na gesi asilia
KUKUZA PATO LA SERIKALI
Tutadhibiti mapato kutokana na raslimali kwa
kupitia upya viwango vya mirabaha kutokana na
madini na gesi asilia ili kuhakikisha kuwa
Tanzania inapata gawio stahiki.
Serikali itaanzisha Wizara maalum
itakayosimamia nishati ya gesi na mafuta.
Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa Hazina ili
kusimamia vema uwekezaji wa Serikali katika
mashirika na mapato yake.
Tutahakikisha kuwa mashirika ya umma
yanaendeshwa kwa misingi ya faida na uadilifu.
Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru wa forodha
na kupiga marufuku misamaha ya kodi holela ili
kuokoa mabilioni ya fedha yanayopotea kila wiki.
Sambamba na hilo tutarahisisha utaratibu wa
kulipa kodi ili kuondoa kero na mazingira ya
rushwa. Kwa kudhibiti makusanyo ya kodi
tutakusanya fedha za kugharimia huduma za
msingi kama afya na elimu kikamilifu.
KUIMARISHA MUUNGANO
Tutaimarisha umoja, usalama na udugu wa
Watanzania na Muungano kwa misingi ya haki
na usawa
WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE
Wanawake watapewa fursa na haki sawa katika
elimu na uchumi ili waweze bila kuwezeshwa.
Tutahakikisha wazazi wanapata fursa ya kuwa
walezi na wafanyakazi kwa kuongeza urefu wa
likizo ya uzazi
Tutaimarisha elimu ya watoto hasa wasichana
na kukuza fursa zao na kukomesha ndoa za
watoto wadogo.
Tutaongeza uwakilishi wa akina mama katika
ngazi zote serikalini na mashirika yake kufikia
asili mia hamsini ifikapo 2020.
Wazee na wasiojiweza watapewa posho ya
kujikimu inayokidhi mahitaji ya msingi
itakayowawezesha kuishi kwa heshima na
kulinda utu wao ndani ya familia na jamii zao.
SANAA, UTAMADUNI NA MICHEZO
Tutaendeleza na kuwezesha vipaji vya sanaa na
michezo
Tutarudisha viwanja vya michezo vilivyovamiwa
Tutafuta kodi zote za vifaa vya michezo.
Tutadhibiti viwango na maadili ya bidhaa za nje
zinazoingizwa nchini na kuzitoza kodi halisia
Tutajenga taasisi na vyuo vya kukuza michezo
ili kuhakikisha kuwa ndani ya miaka mitano
Tanzania inashiriki kwa ushindi katika
mashindano ya kimataifa ya soka na riadha
Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini
Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii chipukizi ili
kuwapa muda kwa kujijenga.
SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA KWA
TAIFA
Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na
Ujirani mwema.
Tutatetea haki za binadamu, usawa wa nchi na
kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika
diplomasia ya kimataifa.
Tutakuza umoja na ushirikiano wa Umoja wa
Afrika, Jumuia ya Afrika Mashariki, SADC na
Umoja wa Mataifa.
Tutaimarisha Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja
na kudai mabadiliko ya mfumo ili kuleta usawa
wa nchi shiriki.
Ndugu Watanzania
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo
Natambua kuwa uongozi ni dhamana.
Mkinichagua nitaienzi dhamana hiyo kwa
utendaji uliotukuka.
Nawaahidi Watanzania kuwa kwa uwezo, akili,
uzoefu na nguvu zangu zote nitawatumikia.
Nawaomba nanyi mniahidi jasho lenu na uwezo
wenu wote ili kwa pamoja tuvuke. Tutajikomboa
toka utawala wa CCM unaodumaza uchumi na
maendeleo. Tutaanza safari ya uhakika kuondoa
umaskini.
Mabadiliko pia ni kuthamini utu na kukataa
hadaa ya hongo ili kuuza haki yako ya
kuchagua. Msikubali rubuni za uchaguzi kwa
kupewa pesa au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo
sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza pia haki na
sauti yako ya kuwalalamikia walio madarakani.
Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na haki zetu.
Tuchague mabadiliko.
Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na kutenda tofauti.
Hatuwezi kuendelea kufikiri na kutenda kama
kwamba hatuna dharura ya maendeleo. Kwanza
tuanze kwa kufanya mabadiliko na tujiamini
kuwa sisi kama Taifa tunaweza. Tunaweza
kujitegemea na kuleta maendeleo yetu wenyewe
bila kutegemea wafadhili. Hii si ndoto. Nchi
nyingi zimefanikiwa kuondoa umaskini katika
kizazi kimoja. Tujifunze kutoka kwao.
Tuwe taifa linalotumia raslimali zake
kujiendeleza na siyo kuwanufaisha wageni na
kuwafanya Watanzania watwana katika nchi yao.
Inabidi tuache kuwa taifa ombaomba. Tuache
kuukubali na kuvaa umaskini kama joho la
fahari.
Mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na CCM.
Tusitegemee kuwa leo wana jipya. Ndiyo maana
ahadi walizotoa miaka thelathini iliyopita ndizo
wametoa juzi. Tukatae hadaa. Miaka hamsini ya
CCM imetosha.
Tunaamani kwamba tutashinda kwa sababu
Watanzania mpo nyuma yetu. Watanzania
mmeamua kuleta mabadiliko. Kura yako ndiyo
itakayokuwa mkombozi wako. Hakikisha unapiga
na kuilinda kura yako. Wakati wa mabadiliko ni
sasa.
Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana
 
Good if implemented but meaningless if no implementation much had have been promised by previous politicians but less or no have been put into action.
 
Back
Top Bottom