Hujuma hizi Uchaguzi Zanzibar zikomeshwe

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
JANA katika vyombo mbalimbali vya habari likiwemo gazeti hili kulikuwa na habari za kusikitisha kuhusu hatua ya watu wasiojulikana kuchoma nyumba tano za wakazi wa Kangagani katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Watu hao hawakuishia kuchoma nyumba za wananchi wenzao pekee, bali pia walichoma ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoko Kiuyu, Minungwini na Kituo cha Afya cha Tibirinzi, huko huko Kaskazini Pemba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nasiri Ali, uchomaji moto huo una dalili za hujuma katika kipindi hiki ambacho Zanzibar inaelekea kwenye uchaguzi wa marudio.

Si Polisi tu waliohisi kwamba matukio hayo yanaweza kuwa hujuma, bali hata Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema matukio hayo yamelenga kuhujumu na kutisha wananchi ili wasijitokeze kupiga kura katika uchaguzi wa marudio.

Kwa mujibu Vuai, matukio hayo yamelenga wafuasi wa CCM kwa sababu hakuna mwanachama wa CUF ambaye nyumba yake imeharibiwa na moto. Hata sisi tunapata hisia kwamba hizi zinaweza kuwa hujuma kwa sababu wiki chache zilizopita kulikuwa na madai ya wagombea wa vyama vya upinzani vilivyoamua kushiriki uchaguzi huo wa marudio utakaofanyika Jumapili ijayo kutishwa ili wasishiriki.

Tunapenda kutoa rai kwa wale walioamua kususia uchaguzi kama wanadhani hatua yao ina maana yoyote basi wakae pembeni na kuwaacha wale wanaoamini kwamba ni kwa njia ya uchaguzi mgogoro wa Zanzibar unaweza kutatuliwa.

Wawaache watumie uhuru wao wa kikatiba kupiga kura ili kupata viongozi kwa njia ya kidemokrasia. Hatua ya kumchomea binadamu mwenzako nyumba ambayo anaitumia yeye na familia yake kwa sababu za kisiasa ni kitendo cha kinyama ambacho hakipaswi kuungwa mkono na yeyote mwenye akili timamu.

Inasikitisha zaidi kusikia kwamba watu hao walifikia hata kuchoma kituo cha afya ambacho kinahudumia wananchi bila kujali itikadi zao. Tunatoa rai kwa yeyote aliyepanga kufanya hujuma kujifikiria mara mbilimbili kuwa anafanya kosa la jinai na ukatili kwa binadamu wenzake.

Ni kwa muktadha huo huo, tunalihimiza Jeshi la Polisi kuhakikisha wote waliofanya hujuma hizi na wengine wanaofikiria kuzifanya wakati siku za uchaguzi zinaposogea wasakwe kwa udi na uvumba na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. La kuzingatia ni kuhakikisha hakuna mtu atakayeonewa.

Halikadhalika, Jeshi la Polisi lizidishe mikakati yake ya kiintelijensia ili kuhakikisha hujuma kama hizi hazitokei tena. Uchaguzi wa marudio ni njia sahihi ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar kwani anayedhani kwamba alishinda katika uchaguzi uliofutwa hana sababu ya kuogopa kushiriki kwani ataendelea kushinda na anayeamini kwamba uchaguzi uliofutwa ulikuwa na kasoro, basi huu wa maridio utaondoa kasoro hizo.

Tunachukua pia fursa hii kuhimiza wananchi wajitokeze kwa wingi bila woga kushiriki katika uchaguzi wa marudio kwani ndio njia sahihi ya kupata viongozi watakawaongoza katika kipindi kingine cha miaka mitano.
 
Back
Top Bottom