Msumari wa chuma ulipigiliwa kwenye kichwa cha Tanganyika kufuatia kutungwa kwa Sheria Namba 27 ya 1967 na Bunge la kawaida, iliyompa Rais uwezo wa kuweka neno Tanzania badala ya Tanganyika katika Sheria zote, na mahali popote Tanganyika lilipoonekana, lakini bila kugusa wala kubadili jina hilo katika Hati ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, ambazo hata hivyo, Rais hakuwa na mamlaka ya kuzibadili.
Hii ni kwa sababu, kwanza, Mkataba wa Muungano una hadhi ya kimataifa isiyoweza kuguswa na sheria za nchi; na pili, Sheria ya Muungano ni tunda la Mkataba huo wa Kimataifa ambapo kazi pekee ya mabunge ya nchi hizo mbili huru, ilikuwa ni kuridhia tu yaliyomo katika mkataba ili yapate nguvu ya kisheria kwa utekelezaji wa mambo yale 11 ya Muungano; na yasiyo ya Muungano yaendelee kushughulikiwa na Serikali za nchi husika.
Mabadiliko yote haya, kuanzia na Rais kuahirisha kuteua Tume ya kupendekeza Katiba na kutoitisha Bunge la kupitisha Katiba ifikapo Machi 26, 1965; kutungwa kwa Katiba ya muda ya 1965, na Sheria Na 24 ya 1967 iliyofuta kwa nguvu jina la Tanganyika; ndiyo yaliyoridhiwa na kurithishwa bila utafiti makini wa kisheria, kwa kuingizwa katika Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano ya 1977; ambayo nayo hata hivyo, misingi na uhalali wa kutungwa kwake umezua utata miongoni mwa wanasheria wa mambo ya Katiba.