Hoja si udikteta au upole bali ni matokeo ya kazi

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
FEBRUARI 4, mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alizindua mwaka mpya wa Mahakama, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Sheria Duniani, tukio lililofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu kadhaa mashuhuri, akiwamo Jaji Mkuu wa Kenya, Dk. Willy Mutunga.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Magufuli ambaye Februari 12, wiki hii – Ijumaa, atatimiza siku 100 tangu achaguliwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mambo mengine, alizungumzia namna ambavyo nchi hii imekuwa ikifanyiwa mambo aliyoyaita “ya ajabu” na baadhi ya watendaji serikalini.

Rais Magufuli alisema ameamua nchi iende mbele na anayepanga kukwamisha atakwama yeye, na kubwa zaidi, alisema nchi hii inapaswa kuwa katika kundi la nchi wafadhili na si kuwapo kwenye kundi la nchi zinazoomba kufadhiliwa, tena wakati mwingine kwa lugha za kejeli sambamba na masharti ya udhalilishaji kutoka kwa nchi wafadhili, zikiwamo baadhi ya nchi za Ulaya na kwingineko duniani.

Rais alionyesha kuchukizwa na uzembe uliotamalaki ndani ya serikali za taasisi nyingine za umma nchini. Aliweka bayana kwamba, uamuzi katika masuala ya kuendesha nchi ili kukidhi matarajio ya Watanzania unapaswa kufanywa wakati wowote na mahali popote.

Katika kusisitiza hilo, alisema kwamba yeye kwa nafasi yake kila anapofanya uamuzi mgumu kwa maslahi ya nchi haina maana kuwa ni mtu wa ajabu, bali ni mpole na si dikteta lakini hana namna zaidi ya kufanya uamuzi husika bila kigugumizi.

Kwa upande wetu, tunaamini kwamba kipaumbele cha Watanzania kwa sasa ni matokeo ya kazi inayofanywa na Rais, wizara na taasisi nyingine serikalini na hata katika sekta binafsi.

Tunaamini mjadala muhimu na wa kwanza kwa Watanzania walio wengi na ambao wamekuwa wakitaabika kutokana na hali ya mkwamo wa masuala muhimu kwenye uendeshaji nchi ni matokeo ya kazi tu, si upole, ukali au udikteta wa Rais.

Rais awe dikteta, mpole au mkali ni mambo ambayo yanaweza kujadiliwa lakini si kwa kuyapa kipaumbele. Kwa kuzingatia hali halisi nchini huo si mjadala wa kipaumbele ikilinganishwa na kiu ya matokeo ya kazi ya kusogeza mbele nchi kwa kasi inayohitajika. Zipo nchi duniani zenye viongozi wapole, lakini hazikuwa na matokeo mazuri kimaendeleo.

Zipo nchi duniani zilizokuwa na viongozi madikteta au viongozi wakali, lakini hazikuwa na matokeo mazuri katika kazi ya kusaka maendeleo na ndiyo maana tunasema, jambo la muhimu ni matokeo ya kazi, mengine baadaye.
 
Back
Top Bottom