Hofu ya Ugaidi (1)

maggid

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2006
Posts
1,084
Reaction score
1,251
Na Maggid Mjengwa,


MOJA ya sababu kadhaa za vita vya Iraq ilikuwa ni kupambana na ugaidi. Juzi hapa nchi yetu imekumbwa na shambulizi la pili la kigaidi. Naam, ugaidi ungalipo na unabaki kuwa ni tishio kubwa duniani.

Hakika, hapa duniani matukio ya kigaidi yameongezeka. Ajabu ya matukio ya ugaidi, kihistoria, mengi ya matukio makubwa ya ugaidi humu duniani yamefanyika katika mwezi Septemba.

Ni ukweli wa kihistoria, kuwa mwezi Septemba ni mwezi wenye kuambatana sana na matukio ya kigaidi.

Mfululizo wa makala hizi zitazungumzia juu ya suala hili la ugaidi na hofu yenye kuambatana nayo. Mahusiano ya mwezi Septemba na ugaidi yataonekana pia.

Kwa faida ya wasomaji, nitaanza kwa kuangalia chimbuko la ugaidi kihistoria na kutoa mifano mbalimbali.

Ni rahisi kusema kwamba ulimwengu umebadilika baada ya ugaidi wa Septemba 11 mwaka 2001 kule Marekani. Kwamba ugaidi umesogea karibu zaidi katika fikra zetu. Watanzania bado tunakumbuka tukio la shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Dar Es Salaam Agosti 7, 1998.

Sura ya ugaidi imeonekana vema zaidi miongoni mwa walimwengu. Bila shaka, picha ya filamu ya televisheni yenye kuonesha majengo mawili ya World Trade Centre kule Marekani yakitunguliwa na kuanguka, zimeonwa na takribani asilimia 75 ya watu wa ulimwengu huu. Katika hili la kuchambua ugaidi, hebu basi tuanze na kujiuliza;

Ugaidi ni nini?

Itakumbukwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano walipokutana Dodoma mwaka 2002 walipitisha Muswaada wa Ugaidi. Wabunge wetu walitumia muda mwingi sana kujadili tafsiri ya neno "ugaidi".

Kwa kifupi, ugaidi ukitafsiri kutoka neno la Kiingereza "Terrorism" tunapata maana ya "hofu". Neno la Kiingereza "Terror" lina maana ya hali ya "kutisha".

Vitendo vya kigaidi hutumiwa na mtu au makundi ya watu ili kuwaingizia watu hofu ndani ya mioyo yao na pengine hata kuchukua madaraka ya kisiasa. Ugaidi ni njia ya mnyonge na hata mwenye nguvu kutimiza malengo yake. Hili litafafanulika zaidi kadri utakapofuatilia maandiko haya.

Kihistoria tunaona kuwa, vitendo vingi vya kigaidi humu duniani vimefanywa pia na dola zilizo madarakani kwa minajili ya kuendelea kushika hatamu za dola. Mathalan, msemo wa " Utawala dhalimu" kwa tafsiri ya Kiingereza "Terror regime" hutumika tunapoielezea dola yenye kutumia mabavu na nguvu nyingi kupita kiasi. Dola au mtawala asiyezingatia sheria wala haki za kibinadamu.

Msamiati huu wa utawala dhalimu unatokana na lugha ya Kifaransa na una chimbuko la Mapinduzi ya Wananchi kule Ufaransa kati ya mwaka 1789 hadi 1799. Utawala dhalimu wenye kutisha" la terreur" ulikuwepo kule Ufaransa kunako miaka ya kati ya 1792 hadi 1794. Katika kipindi hicho watu takribani 40,000, wengi wao wakiwa wakulima na wahunzi waliuawa.

Mifano ya tawala dhalimu na za kutisha katika sehemu nyingine za dunia ni kama Urusi ya zamani chini ya dikteta Stalin, utawala wa Kinazi wa Ujerumani kati ya 1933-1945 chini ya Fashisti Hittler.

Katika Afrika, tuna pia mifano kadhaa ya tawala dhalimu na za kutisha ambazo kimsingi ni tawala za kigaidi. Uganda ya Idd Amin, Afrika ya Kati ya Bokassa, Zaire ya Mobutu, na nchi nyingine nyingi. Hizi zilikuwa tawala dhalimu.

Ugaidi kimsingi ni ile hali ya mtu, kikundi au dola, kwa maana ya taifa, kutumia nguvu nje ya wigo wa sheria ili kufikia malengo yao. Mwenye kuendesha vitendo vya kigaidi huchagua watu wake watakaoathirika na vitendo hivyo. Si lazima mtu au watu hao watakaoathirika wawe ni wahusika wa moja kwa moja wa mgogoro husika, isipokuwa, waathirika mara nyingi huchaguliwa na huonekana kama wawakilishi wa malengo ambayo magaidi wanataka kuyafikia. Malengo au sababu za ugaidi zaweza kuwa ni za kidini, kijamii na kisiasa.

Ugaidi huwa wa kimataifa pale tukio la kigaidi linapofanywa nje ya mipaka ya yule anayatenda tendo la kigaidi, au raia wa nchi moja wanapokuwa walengwa na kauthirika na tendo la kigaidi katika nchi ya tatu, mathalan, magaidi kutoka Colombia wanapofanya tendo la kigaidi dhidi ya raia wa Uingereza katika nchi ya Zambia.

Makundi ya ugaidi

Ugaidi kihistoria tunaweza kuugawa katika makundi manne:

1. Vikundi vya kigaidi vyenye kujitenga na vyenye mitazamo ya kitaifa ama kizalendo. Hapa tunaweza kuona mifano ya vikundi vya kigaidi kama vile IRA, Red Brigade ( Italia) na vikundi kadhaa vya kigaidi katika Palestina, mathalan, Islamiska Jihad, Al –hasqa Brigade na vinginevyo.

Hapa pia tuna mfano wa kikundi cha kigaidi cha ETA kule Hispania na vikundi kadhaa vya kigaidi katika Tjechnia. Mifano ya vitendo
vya kigaidi vilivyofanywa na vikundi hivi ni kama vile vya utekwaji nyara wa raia kule Mosko Urusi mwaka 2002, Mauaji ya wahanga kule Israel na mabomu yaliyokuwa yakitegeshwa kwenye magari kule Hispania.

2. Vikundi vya kigaidi katika Marekani ya Kusini. Vikundi hivi kwa kiasi kikubwa ndio vimekuwa chachu ya ugaidi. Vikundi vingi vya kigaidi duniani vimehamasishwa na ugaidi wa mijini unaofanywa na vikundi vya kigaidi katika Marekani ya Kusini. Mifano ya vikundi vya ugaidi hapa ni Tupamaros kule Argentina, ambacho, kikundi cha ugaidi cha RFA cha kule Ujerumani kiliiga mbinu za kikundi hiki.

3. Aina nyingine ya ugaidi ambayo inalingana sana na huo uliotangulia hapo juu ni ugaidi uliokua kwa haraka katika Marekani ya Kaskazini, Ulaya Magharibi na hata Japan. Baada ya kushindwa kwa kampeni za kisiasa, vikundi vya ugaidi katika mataifa hayo vilihamasishwa na mbinu za ugaidi wa mijini kama za wenzao wa Marekani ya Kusini.

4. Ugaidi unaotokana na waumini wa kidini wenye "Imani kali" . Mara nyingi hawa hutoka kwenye makundi yaliyojitenga yenye misimamo ya kitaifa. Makundi haya yanapatikana katika dini zote mbili zilizo kubwa humu duniani, Ukiristo na Uislamu. Kwa upande wa vikundi vyenye kutoka mataifa ya Kiislamu, mara yingi malengo ya vitendo vya kigaidi kwa vikundi hivyo ni kuundwa kwa mataifa ya Kiislamu yenye kufuata "sharia".

Katika hili la kugawa aina za ugaidi na makundi yake, tunaweza pia kuona mifano ya vikundi vya kigaidi ambavyo havistahili kuwepo katika makundi hayo manne niliyotaja hapo juu: Hawa tunaweza kuwaita "magaidi wa kujitegemea".

Mara nyingi hawawakilishi kikundi maalum au chama fulani chenye kufuata itikadi fulani ya siasa. Hata hivyo, kundi hili nalo huendesha vitendo vya kigaidi, malengo hasa ya ugaidi wao wakati mwingine huwa hayaeleweki.

Mifano ya magaidi wa kujitegemea ni mtu kama Abu Nidal ambaye inasadikiwa aliuawa mjini Baghdad mwaka 2002. Vile vile tuna mtu kama Carlos ambaye alijulikana kama Schakalen.

Magaidi wa kujitegemea, Abu Nidal na Carlos walijulikana sana kutokana na kuendesha kwao kwa mashambulizi ya kigaidi katika miaka ya 70. Yawezekana mmoja wa watu hawa wawili ndiye aliyeshiriki kwenye kupanga shambulizi la kigaidi dhidi ya ndege ya Shirka la ndege la Marekani la Pan-Am iliyolipuka katika anga za Scottland mwaka 1988, watu 270 walipoteza roho zao.

Gaidi nambari wani au labda tuseme gaidi "kidedea" katika ulimwengu wa leo bila shaka yeyote atabaki kuwa Osama Bin Laden. Huyu aliuawa na makomandoo wa Marekani. Osama alikuwa ni mwislamu mwenye itikadi kali.

Osama bin Laden na kundi lake la Al-Qaida ilikuwa ni vigumu kuwaingiza pia katika mgawanyo makundi manne niliyoyaainisha hapo juu.
 
Wale waliohusika kumteka kibanda nao ni magaidi? naomba jibu,kwani nasikia kuna watu wamehojiwa nk!
 
Kumbe umejikopi na kujipesti mwenyewe.....without even editing the paragraph styles..... naona thread title na content havishibiani kabisa....goodluck for the second part
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…