Hii ya bodi ya mikopo ni ujasiri wa kifisadi

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
JUZI Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza matokeo ya uchunguzi, baada ya kufanyika kwa ukaguzi maalumu katika mfumo wa utoaji wa mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini (HESLB).

Uchunguzi huo umebaini madhaifu makubwa katika maeneo manne ndani ya HESLB ambayo ni udhaifu katika mfumo wa utunzaji wa taarifa za marejesho ya mikopo, udhaifu katika ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo na upungufu katika malipo ya mikataba ya utambuaji wa ukusanyaji wa madeni.

Kwa mujibu wa taarifa ya waziri uchunguzi huo umebaini kuwa wanafunzi 262 walinufaika na mikopo ya Sh bilioni 10.8, lakini kumbukumbu zinaonesha kwamba wadaiwa hao wanatakiwa kurejesha Sh bilioni 5.5 tu.

Kutokana na kiasi hicho ambacho wanafunzi hao wanatakiwa kurejesha ni wazi kuwa Sh bilioni 5.3 hazitarejeshwa na wadaiwa hao; licha ya kumbukumbu kuonesha kuwa walipewa mkopo huo ambao ni fedha za walipa kodi Watanzania.

Kwa kuwa kumbukumbu zinaonesha kuwa fedha hizo zilitoka serikalini na zikaingizwa kwenye akaunti za wanafunzi hao, ni wazi kuwa kulikuwa na mchezo mchafu unachezwa kati ya maofisa watendaji wakuu wa bodi ya mikopo pamoja na baadhi ya wanafunzi wenyewe.

Taarifa nyingine inaonesha jumla ya wanafunzi 247 ambao walifanya marejesho ya mikopo yao ya awali kwa kiwango cha asilimia 25 ambao walilipa Sh milioni 270.9 bado hawajaingizwa kwenye orodha ya wanafunzi waliorejesha mikopo yao.

Kama hawajaingizwa kwenye orodha hiyo, fedha walizolipa zimepelekwa wapi? Na pia ikabainika kuwa mfumo wa urejeshaji mikopo bado haujaunganishwa na mfumo wa utoaji mikopo hali inayosababisha kutokuwepo kwa taarifa sahihi za marejesho.

Kwa mifano hiyo ni wazi kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wa utunzaji taarifa za marejesho ya mikopo hali ambayo inatoa mianya ya watu kuweza kutumia marejesho hayo kuzikwapua. Kuhusu udhaifu katika ufuatiliaji wa urejeshaji wa mikopo, inaonesha kuwa wanafunzi 105,202 wenye mikopo iliyoiva ya Sh bilioni 712.9 hawajaanza kurejesha mikopo.

Wanafunzi hao ni wale ambao walipata mikopo kuanzia mwaka 1994 hadi 2013. Yaani mtu amepata mkopo tangu mwaka 1994 hadi leo hajarejesha, huyo mtu yawezekana anakaribia pia kustaafu kazi, hivyo inaweza kuwa ngumu mtu huyo kurejesha mkopo aliofaidika nao katika kupata elimu yake.

Huu ni uzembe wa hali ya juu ndani ya bodi hiyo. Katika eneo hilo, ukaguzi pia unaonesha wanafunzi 2,619 wenye mikopo iliyoiva ya kiasi cha Sh bilioni 14.5 wanadaiwa kwa kukopeshwa mikopo wakiwa katika vyuo tofauti; lakini wanatumia namba moja ya kidato cha nne.

Wanafunzi hao walikopeshwa Sh bilioni 7.1 katika chuo cha kwanza na Sh bilioni 7.3 katika chuo cha pili. Kwa taarifa hizo cha uchunguzi ni wazi kuna uwezekano mkubwa wa fedha za umma ambazo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi, zilitumika kinyume na malengo yake na kuingia kwenye mifuko ya watumishi wasio waaminifu.

Yawezekana ndiyo maana migomo ya mara kwa mara ilikuwa inafanywa na wanafunzi mbalimbali wa vyuo vya elimu ya juu kwa kuwa utoaji wa mikopo haukuwa kwenye mfumo unaoeleweka.

Hii ilisababisha fedha zinazotolewa na Serikali kutowafikia walengwa na hivyo baadhi ya watu kunufaika. Naunga mkono hatua hii ya Serikali ya kuwaamuru wanafunzi ambao walifaidika na mikopo hiyo kwa kupata fedha zaidi ya mara moja, warejeshe fedha hizo ili zikawasomeshe wengine.

Huu ni ujasiri wa kifisadi ambao naipongeza Serikali ya Rais John Magufuli kwa kuamua kufanya uchunguzi wa namna hii na kubaini madudu haya. Hili lisifumbiwe macho ni vyema wahusika wafikishwe mbele ya Mahakama wakaeleze zilikoenda fedha hizo.

Chanzo: Habari leo
 
Back
Top Bottom