USIKUBALI HASIRA IKUANGAMIZE.
Katika maisha kuna nyakati mtu au kitu
kimekukasirisha kupita kiasi.Wote huwa
tunakasirika. Ni kitu cha
kawaida kukasirika. Akili na mwili ndivyo vilivyo. Lakini hasira
kupita kiasi hubomoa, huangamiza na huaribu
starehe zote za maisha.
Usiende kulala ukiwaka hasira, simama na ishinde Phyllis Diller aliwaasa wanawake katika kitabu chake kinachoitwa
Phyllis Dillers House Keeping Hints (Dokezo za Phyllis Diller za Utunzaji wa Nyumba) cha mwaka 1966 wakati
wameudhiwa na
waume au watoto wao.
Katika hasira lazima kuna
mabishano na chanzo chake siku zote si
jambo jema. Ni kama kutupa
jiwe kwenye mzinga wa nyuki.
Tawala hasira, ikiwezekana
zuia isitokee.Mara nyingi matokeo ya hasira huwa
mabaya kuliko hata kilichosababisha
hasira.
Kuna msemo wa
Watamili unasema
hasira kali inaangamiza kuliko
upanga. Tumeshuhudia
wazazi wakiwaua watoto wao kutokana na
hasira. Hakuna ambaye hajawahi
kujuta maishani kwa matokeo ya hasira zake.
Sekunde moja ya
kuchelea kukasirika humwepusha mtu
siku mia za majuto, ni msemo usiopingika.
Shakespeare alisema mwenye
hasira humjeruhi hata rafiki yake
mpenzi.
Wagiriki waliamini kuwa Miungu ikitaka
kukuangamiza ilikuwa
ikikukasirisha kwanza ili upoteze
hekima kasha
ujiue mwenyewe. Waliamini kuwa yeyote alieweza
kukukasirisha alikuwa na uwezo wa
kukushinda katika vita.
Kila unapokasirika unamwaga
sumu katika mishipa yako.
Hasira huondoa busara na huonyesha upande wako wa pili usioufahamu. Kuwa na hasira kupita kiasi ni kama
kuvua nguo hadharani. Kila unapojawa na hasira mwili wako
hutenda maovu. Mwili haufanyi maamuzi ya
hekima kwenye
hasira, hufuata silika tu. Wakati wa chuki, maudhi, wasiwasi, matendo yote
hasi hujaa katika moyo, akili na mwili. Usikubali hasira kupita kiasi
kukukosesha heri na afya njema.
Wengine hupata hasira haraka na kwa kiwango cha juu kupita wengine, wengine hawaonyeshi hasira kwa namna inayoonekana wazi, bali mara zote huwa na
chuki na watu wa
kulalamika. Waliokasirika si mara zote
watalaani na kupigana, wanaweza
kujitenga na jamii, wakawa wakiwa na wapweke
hata wakaugua mwili.
Watu wanaokasirika haraka kwa kawaida huwa hawawezi
kuvumilia matatizo, hujisikia kuwa hawatakiwi
kusumbuliwa au kuudhiwa.
Ni vitu vingi hufanya watu wakasirike. Moja inaweza ikawa
genitiki au
saikologia. Kuna ushahidi kuwa watoto wengine huwa na
hasira, utukutu,
wakali tangu wakiwa
wadogo kabisa. Sababu nyingine inaweza ikawa
kijamii, kimazingira na kiutamaduni.
Hasira mara nyingi huchukuliwa kama kitu kibaya katika jamii, tunafundishwa kuonyesha
chuki, mawazo mazito au namna nyingine ile ya mtazamo lakini si hasira. Matokeo yake ni kwamba tunashwindwa kujifunza namna ya
kukabiliana na hasira kwa njia
iliyo sahihi.
Maisha ya familia vilevile huchangia kutawala hasira. Mara nyingi wanaokasirika haraka hutoka katika familia sizizo na
mshikamano, zenye
matatizo na
magomvi ya mara kwa mara hivyo hawajifunzi namna ya
kuwasiliana vyema.
Lengo liwe namna ya kuizuia na kutawla zaidi hasira kwa namna inayofaa.
Hatari hapa ni kuwa hasira kupita kiasi inaweza kuchukua sura nyingine kama mtu akishindwa kuitawala na kusababisha shinikizo la damu, vidonda vya tumbo na hata magonjwa ya akili. Ukibakia katika hasira ni kama kushikilia
kaa la moto kwa nia ya kumtupia mtu mwingine;
NI WEWE NDIYE UTAKAYEUNGUA.