Dar es Salaam. Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam imemuomba Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene kuingilia kati mgogoro wa madai juu ya jengo la Machinga Complex.
Mgogoro huo ni kati ya Halmashauri ya Jiji dhidi ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) waliolijenga kwa mkopo wa Sh. 12.4 bilioni. Akizungumza leo, Agosti 25,Meya wa Jiji, Isaya Mwita amesema tangu jengo hilo likamilike deni limezidi kukua kwa kasi hali inayowafanya kushindwa kulipa.
Amesema, NSSF ilijenga jengo hilo kwa gharama ya Sh. 12.4 bilioni lakini deni limekua hadi kufikia Sh. 42 bilioni na kufanya NSSF kutengeneza faida ya Sh. 30 bilioni kutokana na riba. Amesema, jengo hilo lina mapungufu mengi ikiwamo kuwa na vizimba 4,000 na si 10,000 kama mkataba ulivyoelekeza.
Pia, Jengo hilo lilikabidhiwa mwaka 2012 likiwa na ghorofa nne pekee na si tano kama walivyokubaliana hali inayosababisha kukusanya kodi isiyozidi Sh 500 milioni kwa mwaka.
"NSSF watuambie kama wanaweza kukaaa na tutafute suluhu, kama hawawezi walichukue lile jengo waliendeshe kwa faida na wajilipe hilo deni, "amesema.
Amewataka wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao hadi watakapofikia makubaliano.
mwananchi