Haki bila wajibu ni sawa na jembe bila mpini

Nov 28, 2016
34
23
Na. F.M.Philip

Haki ni neno maarufu sana midomoni pamoja na masikioni mwa watanzania.Siku hizi haipiti siku haujasikia haki zikidaiwa mahali, si watoto, vijana, wanawake, wanaume, wazee, kina mama ,kina baba, wakristo kwa waislamu, wafanyakazi hata pia waajiri nao wamekuwa mstari wa mbele kudai haki zao.Kinachoshangaza umma wa Tanzania ni kwamba, wengi kama sio wote wa wale wanaodai haki kila uchwao hawataji suala la wajibu walionao katika kudai na kutekeleza haki zao.Suala hili ndilo linalofanya uwepo mjadala wa nafasi ya haki na wajibu kwenye jamii yetu. Hebu tujiulize sasa, Je haki ni nini na wajibu ni nini? Kwa nini ni haki, haki haki, na sio wajibu wajibu wajibu? Je kati ya haki na wajibu kipi huanza na kipi hufuata?

Neno wajibu maana yake rahisi ni ile hali ya kuwa na jukumu la kushughulikia jambo fulani au udhibiti wa jambo au mtu flani kisheria. Wajibu hutokea katika kila haki inapohusishwa au kutajwa, haki haipati maana iliyokamilika bila kutaja au kuihusiha na wajibu.

Neno haki kwa ujumla wake limebeba dhana pana sana na ni suala linaluhisisha mamlaka mtambuka. Ni jambo rahisi kutamka na kulidai, ila ni gumu kulielewa na kukubali pale unapopewa haki yako.Mfano mtu akishitakiwa Mahakamani kwa kutenda kosa la jinai, shauri likasikilizwa pande zote, kisha mshitakiwa huyo akatiwa hatiani, na kuadhibiwa kutumikia kifungo gerezani. Hapo malalamikaji ataona haki imetendeka kwake, ila mfungwa atalalamika kutotendewa haki, anasahau kuwa ni haki yake kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria pale kosa lake linapothibitika kupita shaka, lakini pia amepewa haki yake ya kusikilizwa kupitia utetezi wake . Wataalamu wa sheria wanatuambia kwamba…”Haki haitakiwi itendeke tu, bali ionekane kwamba imetendeka na kwamba, haki inaonekana imetendeka endapo watu wenye akili timamu wataondoka mahakamani wakisema ama kukubali kwamba hapa kweli imetendeka”.

Kwa kawaida, wanadamu huelewa haki kuwa utekelezaji wa sheria bila upendeleo. Kitabu Right and Reason—Ethics in Theory and Practice chasema kwamba ‘haki inahusiana na sheria, wajibu, haki za watu, na madaraka, nayo hutekelezwa bila kupendelea na kwa yule anayestahili.

Mwanazuoni maarufu ajulikanaye kwa jina la “Tabarsiy” anasema: “Neno Haki huwa lina maana ya kila kitu kukaa katika sehemu yake ipaswayo kukaa, hivyo basi wakati wowote ule mtu atapokuwa na itikadi ya kitu fulani kwa kupitia dalili imara katika kuisimamisha itikadi hiyo, hapo basi itikadi hiyo itasadikika kuwa ni itikadi ya haki, kwani kuthibitika itikadi fulani kwa kupitia misingi imara na dalili madhubuti ni haki, na kinyume chake huwa ni Batili”. Mwanazuoni huyu anachosisitiza hapa ni kwamba, haki yoyote huwa imejengwa katika misingi ya upatikanani wa haki hiyo, misingi inayozungumziwa hapa ni utaratibu wa upatikani wa haki hiyo, na mtu ataipata haki yake kihalali pale atakapoisimamia misingi hiyo, na kinyume cha hapo haki yake hiyo huwa ni batili, yaani kama mtu atataka kupata haki bila kufuata misingi iliyowekwa katika kupata haki hiyo.

Neno haki katika sheria , hasa Mahakamani, huwa lina maana ya stahiki ambayo mtu anastahihili kuipata kwa mujibu a sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa katika upatikanaji wa kitu au jambo hilo. Kwa kitaalamu (kisheria) tunaweza kusema kwamba ni muowano unaoweza kupatikana baina hali dhahiri ya mambo fulani na ukweli halisi wa mambo hayo yalivyo, hivyo basi neno haki kimahakama huwa lina maana ya ambatano la ukweli wa jambo fulani linaloshikamana na udhahiri wa shuhuda zilizotolewa au kupatikana na Mahakama fulani katika kumsimamishia mtu shauri au kumhukumu mtu huyo kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo zisemavyo. Kwa mantiki hii, neno haki kimahakama au kisheria linaendana na mchakato (process) ya upatikananji wa haki husika kwa kulinganisha masuala mbali mbali, mfano, ushahidi wa wahusika katika shauri, nafasi ya kisheria (position of the law applicable) na pia kutazama maslahi mapana ya umma kwenye jambo linaloshindaniwa (Public Interest).

Wanazuoni wa dini wanatuambia kwamba utendaji wa mambo kihekima ndiko kunakoweza kuifanya haki ithibiti katika kila kitu, mara nyingi iwapo mtu atakuwa ni mwenye kushikamana na sifa fulani, mwisho wake sifa hiyo hugeuka kuwa ndiyo umaarufu wa mtu huyo. Kwa kutokana na kuwa Muumba Mkamilifu Ndiye Mbora wa kutenda haki, hivyo basi neno haki limegeuka kuwa ndiyo sifa maarufu ya Mola wetu, na sifa hii hakupewa na mtu, bali Yeye mwenyewe ndiye aliyejipa sifa hiyo, Mwenye Ezi Mungu katika Qurani anasema: {Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki, Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu.}Hekima wanayozungumzia wanazuoni wa dini hapa ni suala la kufanya kila jambo kwa ufasaha , wakati sahihi na kwa mtu sahihi.Hapa pia wajibu unajitokeza, kwamba unawajibika kuwa sahihi muda wote ndio haki inapopatikana kwako na kwa wengine.

Kwa ujumla,neno haki lina maana nyingi sana, kila mtu au kikundi cha watu wanaweza kuielezea haki katika mazingira tofauti, lakini kwa maana ya jumla haki ni uhakika au usahihi wa jambo fulani lilivyo, au kuthibika kwa kitu fulani katika picha halisi ya kitu hicho kilivyo. Wakati mwengine neno haki huwa lina maana ya stahiki halali upasayo kupewa , na mara nyingi watu hulitumia neno hilo katika maana hiyo hasa kwa kuwa jambo lolote linalohusishwa na haki huwa ni jambo linalohusiana na sheria, hivyo haki huusishwa na mchakato au utaratibu, kwa mfano pale anapoambiwa mmoja wetu, ni haki yake kupata kitu fulani, yaani ni stahiki yake kupata kitu hicho, na hilo linamaanisha kuwa kupata kwake huko kwa kitu hicho ni lazima afuate taratibu zilizowekwa ili kukipata kitu hicho.

Kwa muda mrefu watu wamekuwa wakidai haki sana bila kutimiza wajibu wao, hapa kinachofanyika ni sawa na kushinikiza matakwa yao yatimizwe bila kujali wengine wanaumizwa vipi na madai yao hayo ya haki zao. Makala hii imelenga kuangalia masuala haya mawili kwa pamoja, na maswali ya msingi yanayoulizwa katika hili ni kwamba; inawezekana kupata haki bila kutimiza wajibu?, kama jibu ni ndiyo, je haki hizi ni kwa ajili ya nani?, jamii, kikundi cha watu fulani wanaodai rehema ama ni mtu binafsi? Kwa nini jamii inahubiri sana haki kuliko wajibu walionao katika katika kupata haki zake? Inakuwaje kama tukiamua kutotimiza wajibu, je kutotimiza kwetu wajibu sio kuvunja haki za watu?

Je, haki ni kutii sheria na taratibu zilizopo kwa lengo tu la kuepuka adhabu na je kwa kufanya hiyo huwa tunatimiza wajibu wetu? Je, haki ni kile kinachoweza kufanywa na watu wengine ili kutupa faida hata kama kufanya hivyo kunawaumiza wenzao? Je, wale wanaoumizwa na utekelezaji wa haki zetu bila kutimiza wajibu wetu, je wao hawana haki? Je, kutenda haki ni kuwa mtu mzuri unayekubalika kwenye jamii? Vipi kama nikiamua kutafuta haki zangu kwa namna ninayoijua mimi hata kama kwa kufanya hivyo ntaonekana kituko? Je, haki ni kutimiza matakwa ya sheria zilizopo hata kama zinaingilia uhuru wa watu? Je, haki ni kutetea matakwa ya wengine, hata kama kufanya hivyo kunakunyima vitu fulani. Je, haki ni matakwa ya kibinafsi yayosilazimika kushahibiana na sheria zinazoonekana ni halali katika jamii?

Katika hali ya kawaida ni kwamba, haiwezekani hata kidogo kupata haki bila kutimiza wajibu wako, haki inapatikana kwa kufuata utaratibu, yaani upatikanaji wa haki ni suala la mchakato. Hakuna haki amabayo inapitakana kwa mara moja.Haki zote zinapatikana kwa kufuata utaratibu, na ndani ya utaratibu huo ndio wajibu wetu unapopatikana.Haki na wajibu ni sawa na sura mbili za sarafu moja.

Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorejewa mara kwa mara, katika Sura ya III, Ibara ya 12- 29 inazungumzia haki na wajibu muhimu wa raia wa Tanzania. Ipo pia sheria ya utekelezaji wa wajibu na haki za msingi(The basic Rights and Duties Enforcement Act), Sura ya 3 ya mwaka 1995 amabayo nayo imerejewa mara kwa mara, katika kifungu cha 3 cha sheria hiyo , imesisitizwa kwamba, sheria hiyo itatumika katika kutekeleza matakwa ya kikatiba katika sehemu ya III ya katiba ya Tanzania, yaani kuanzia Ibara ya 12-29 ya katiba hiyo. Hii maana yake ni kwamba, mtu anayelalamika kuvunjiwa haki yake, anapojaribu kuiomba mamlaka husika kumtekelezea matakwa yake, mamlaka hiyo nayo itarejea katika kumuuliza wajibu wake kama ameutimiza.

Mfano,tunapodai haki ya maandamano, tukumbuke kwamaba sio wote tutakaoandamana, hivyo wapo watu wanaoathirika moja kwa moja au kwa namna moja au nyingine na maandamo tuyafanyao, mfano wafanya biashara kwenye njia ambayo waandamanaji watapita lazima biashara zao zinafanyika, watumiaji wa barabara ambayo waandamanji watapita nao wataadhirika wakati wa maandamano hayo, wanausalama nao itabidi waaache shughuli zingine waelekeze nguvu kaatika maandamano hayo hivyo wengine usalama wao kuwa mashakani kwa kukosa ulinzi. Haya ndio masuala tunayopaswa kuyatazama au kuyazingatia wakati tunadai haki kama hiyo ya kuandama.

Haki sio kutimiziwa matakwa yako au ya kikundi chako peke yake. Haki ni suala la usawa, ni pale unapopata na wenzio pia wanapata,japokuwa wakati mwingine haki inamaanisha wewe kukosa au watu flani ni wakose haki zao ili wengine wapate, mfano upendeleo unaotolewa na watawawala katika kuwapatia kundi flani la watu haki zao, kama upendeleo wa kielimu kwa watoto wa kike kuliko kuweka usawa katika upatikanaji wa elimu kwa watotot wa kiume na wa kike.Lakini jambo la kuzingatia hapa wakati wote ni kwamba, haki inakuwa na mana zaidi na ndivyo ilivyo wakati wote pale unapofuata taratibu,ni suala la kutimiza wajibu wako kisheria, hata kama sheria hiyo ni kandamizi kwa namana moja au nyingine, unachopaswa kufanya ni kufuata utaratibu katika kudai marekebisho ya sheria hiyo. Haimaanishi kwamba, kama sheria iliyopo ikikunyima haki basi wewe uivunje ili upate haki yako. Hupaswi kujijukulia sheria mikononi eti kwa sababu umevunjiwa haki yako, unawajibu wa kumlinda hata yule anayevunja haki yako na kumfikisha salama katika mamlaka husika ili utendewe haki naye pia apewe haki zake kwa mujibu wa hali yake katika sheria (mkosaji).

Kwa ujumla huwezi kupata haki bila kutimiza wajibu, neno haki halina maana kama halitaambatana na wajibu. Huwezi kuieleza haki kwa namna yoyote pasipo kuihusisha na wajibu. Kwa namana yoyote ile haiwezekani kamwe haki kusimama peke yake bila wajibu.Wanazuoni wa masuala ya sheria na haki za binadamu wanatuambia kwamba , haki ya mtu huwa imebeba wajibu kwa mtu mwingine kuhakikisha mtu huyo anapata na kuitumia haki yake ipasavyo, na wakati huo huo mtu yule anapotekeleza au kuitumia haki yake, anawajibu pia wa kuhakikisha kwamba , utekelezaji wa haki yake haukiuki haki za wengine.

Kwa lugha rahisi hapa ni sawa na kusema kwamba, watu tunapaswa kukumbuka wakati wote kwamba, haki yako inapoanzia, ujue kuna haki ya mwingine imeishia hapo, na haki yako inapoishia ujue pia kuna haki ya mwingine imeanzia hapo, ili usiingilie haki ya mwenzio ilipoishia au kuanzia katika kutumia haki yako, unawajibu wa kusimama kwenye utekelezaji wa haki yako katika mipaka yake, hapo ndipo wajibu wako ulipo, wajibu wako ni kukaa kwenye mipaka ya haki yako na si vinginevyo. Lakini pia tunapodai haki yatupasa tuwe na kumbukumbu kwamba, haki haipatikani bila kufuata utaratibu uliowekwa katika kuifikia haki hiyo.Tunapodai haki tunawajibu wa kutenda haki, tunapodai haki tunapaswa kuwa na mikono safi.

Ndio maana ninasema kwamba haki bila wajibu ni awa na jembe bila mpini, jembe lisilo na mpini halina maana, haliwezi kulima kwani litakosa nguvu ya kuchimba ardhi kwa kuwa halina mshikio, ili haki iwe na maana , lazima mdai haki atimize wajibu, hivyo haki bila wajibu ni vurungu. Ni wakati sasa wakukumbushana wajibu wetu kama raia pale tunapodai haki zetu. Mstakabali wa amani tuliyonayo upo kwenye matumizi sahihi wa maneno haya, haki na wajibu, tusiegemee upande mmoja tu kwa maslahi yetu binafsi, au maslahi ya vikundi vyetu hasa vya kisiasa.Kuhubiri haki bila wajibu ni sawa na kusambaza chuki kwenye jamii pasipo sababu, maana watu watakuwa wanadai wapewe tu wanachotaka bila hata kufuata taratibu zilizopo. Na wale walio katika nafasi ya kutimiza wajibu wao ili wale wanaodai haki wapate haki zao, nao watimize wajibu wao ili kuleta usalama na mani katika jamii yetu.

Kuhimiza haki bila wajibu ni kuvunja katiba , maana katiba yeneyewe inahimiza haki na wajibu kwa pamoja, kwa nini sisi tunahimiza haki tu bila wajibu? Tukumbuke kila wakati kwamba, HAKI BILA WAJIBU NI SAWA NA JEMBE BILA MPINI.
 
Back
Top Bottom