ILIPOISHIA;
Lakini ilikuwa ni tofauti na alivyodhania baada ya kula chakula ambacho alishiba vizuri na kunywa maji matamu, Balkis alimpulizia vitu kama unga vilipomgusa usoni, palepale aligeuka hali yake ya mwanzo ya nzi.
SASA ENDELEA ...
Alitamani kuomba msamaha lakini alichelewa, alichukuliwa na kurudishwa kwenye tawi la mti na kukumbana tena na harufu kali ya uchafu wa mzoga wa mbwa aliyekuwa akinuka.
Kwa harufu ile kama angekuwa katika umbile la kibinaadamu basi angetapika mpaka utumbo. Lakini bahati nzuri alikuwa kwenye umbile la nzi, aliendelea kuteseka na harufu na baridi kali.
Balkis baada ya kutoka kwa Tonny alikwenda moja kwa moja kwa Ashura aliyekuwa amelala pembeni ya nyumba mbovu.
Karibu yake kulikuwa na mtaro wa maji machafu lakini yeye aliichagua sehemu iliyokuwa kavu. Lakini ukali wa ubaridi ulikuwa ukimpata kisawasawa.
Alijuta kwa mambo yote aliyoyafanya kwa kuwatepeli wanaume kwa ajili ya Tonny ambaye ndiye aliyemuingiza kwenye kazi ile ya kuolewa na wanaume na mwishowe kuwadhulumu kwa kuvunja uhusiano.
Kitu kilichowafanya wanaume zaidi ya wawili kujiua baada ya kufilisika na wengine kupatwa na ukichaa.
Aliamini hali ile ingemtokea na Muddy lakini kwa bahati ya ajabu Balkis aliyaokoa maisha yake. Alitamani Balkis atokee mbele yake amuombe msamaha lakini hakuonekana.
Usingizi ulimpitia pale alipokuwa amejilaza huku akichonyotwa na njaa pamoja na kiu.
Alishtuliwa kutoka usingizini na kujiona akiwa mbele ya Balkis, kama Tonny alivyotaka kuomba msamaha, naye alikuwa kama anataka kumuuma Balkis aliyemchukua na kumpeleka sehemu iliyokuwa nzuri, alimtemea mate na muda uleule alibadilika kurudia katika umbile lake la kibinadamu.
Ashura baada ya kurudi katika hali yake ya kawaida alipiga magoti mbele ya Balkis na kuanza kuomba msamaha.
“Balkis nisamehe sana nimekosa, adhabu ya leo inatosha hali yangu ni mbaya,” alisema huku akibubujikwa na machozi.
“Hii si adhabu ya siku moja ni ya muda mrefu kama nilivyokueleza muombeni Mungu nijifungue salama, kama mwanangu akifa au mimba ikitoka mjue na nyinyi maisha haya yatakuwa ya milele kwenu.”
“Naomba unisamehe, sitarudia tena, niliyokutananayo leo yanatosha, ukiongeza zaidi nitakufa.”
“Ashura sikufuata kuombwa msamaha, nimekuletea chakula, kula haraka kabla hapajakucha, ukichelewa utalala na njaa, kuonana na mimi tena ni mpaka kesho muda kama huu, tapeli mwenzako kanichelewesha na wewe unataka kufanya hivyo.”
“Nani, Tonny?”
“Eeh.”
“Yupo wapi?”
“Yupo jalalani.”
“Anafanya nini?”
“Kwani nzi makazi yake wapi?”
“Mungu wangu umemgeuza kuwa nzi?”
“Tena ana bahati angeendelea kuniletea ujeuri ningemgeuza kuwa funza na makazi yake yangekuwa kwenye kinyesi milele.”
“Sa...sa...”
“Ee...eeh! Hebu kula niondoke.”
Ashura hakuwa na jinsi alikula chakula kitamu na kuamini kama Balkis ameamua kumletea chakula ambacho hakuwahi kula katika maisha yake ya kibinaadamu, lazima atakuwa amerudiwa na roho ya huruma na kumsamehe.
Lakini dhana yake ilikuwa ni tofauti, baada ya kumaliza kula alirudishwa katika umbile lake la mbwa na kurudishwa alipotolewa na Balkis akatoweka.
****
Siku zilikatika huku adhabu ya Ashura na mwanaume wake zikiendelea, walikuwa wakiteseka kwenye maumbile yao ya mbwa na nzi. Maisha ya Tonny yalikuwa ya jalalani na chooni japo hakuweza kula uchafu.
Ashura maisha yake yote yalikuwa ni kuzurura jiji zima kutafuta sehemu iliyokuwa salama kutokana na kukimbizwa kila kukicha na watoto watukutu.
Mimba ya Balkis iliendelea vizuri na baadaye alijifungua salama salmini watoto mapacha wa kike na kiume, kila mmoja alifanana na mzazi wake mmoja.
Wa kike alifanana sana na mama yake na wa kiume alifanana na baba yake. Balkis alifurahi sana na kuamini dhamira yake ilitimia.
Aliamua kwenda chini ya bahari na wanawe kuwatambulisha kwa wazazi wake, wakati akiwa njiani kuelekea chini ya bahari.
Baba yake Mfalme Barami alikuwa na mazungumzo mazito na mkewe juu ya kukosa taarifa za Balkis.
“Mke wangu hivi huyu mtoto anataka kupimana nguvu na mimi?”
“Kwani tatizo ni nini?”
“Hulioni? Tangu nilipomueleza aachane na yule mwanaume amepotea, haleti tena vizazi vya wanawake mwaka unakatika.”
“Mume wangu jambo hili linatakiwa busara siyo kutumia nguvu.”
“Kama anaona ni utani, nitamtuma Pweku mtwana mkuu akamuulie mbali huyo mwanaume wake.”
“Mume wangu unatafuta vita mpya.”
“Na nani?”
“Siamini kama Balkis atakubali kirahisi mwanaume wake auliwe, atawamaliza watwana wako wote kwa kuwaua.”
“Inamaana sasa hivi mwanao anataka kunipanda kichwani?”
Walinyamaza kuzungumza baada ya kusikia kelele za chereko chereko nje, zilikuwa ni shamrashamra zilizowashangaza wote.
Msafara ulikuwa ukiingia ndani, ukiongozwa na vijakazi na watwana akiwemo mtwana mkuu Pweku, sherehe kama ile hutumika kukaribisha mgeni aliyezaliwa.
Balkis alionekana akiwa juu kwenye farasi mwenye matandiko ya dhahabu.
Mama yake Balkis Malkia Huleiya alipowaona watoto wa Balkis, alikimbia kwenda kumpokea mwanaye na wajukuu zake kwa furaha ya ajabu.
Mfalme Barami alikuwa amebaki njia panda, asielewe kilichokuwa kikiendelea mpaka wageni wale walipokuwa wakiingia ndani, hakujua watoto wale aliokuwanao Balkis walikuwa ni wa nani.