'hadaa'- mfano wa mkasa wa mapenzi unaosababisha kuuana

Sep 17, 2013
12
4
UKIIPENDA TUMA SMS KWENDA giningiasilia@gmail.com then ntaitunga hadi mwisho na tutaangalia tunafanyaje.


HADAA!
Na Aloyce Eliah (Mginingi)
N

a bado kama kuna siku ambayo nitaijutia maishani mwangu ni ile niliyomtia machoni mwangu, siku ambayo hadi leo ninaposimulia mkasa huu, nikiwa Gereza la Maweni, moja ya magereza magumu Tanzania, nikitumikia miaka 30 na kazi ngumu kwa jambo ambalo hadi kesho ndugu, jamaa na marafiki hawaamini ni kwa jinsi gani nilifanya? Sitaisahu hadi nakwenda kaburini…kwasababu kwao nilikuwa ni mtu stahili asiye kifani, nilikuwa mfano, kamwe hawakuweza kuamini kama ningeweza kufanya kitendo hicho.
Lakini hata mshangao uje wa aina gani hakuna ambaye anaweza kubadilisha ukweli kuwa nilikuwa ndani ‘jehanamu’ nikitumikia miaka mingi ya kifungo na kazi ngumu. Hata iweje haiwezi kubadili ukweli kuwa nimekuwa mtu wa kula kwa filimbi, na kuamka kwa filimbi. Maisha ya jela, we acha tu! Leo asubuhi, tumeamshwa na bwana jela na kutakiwa kwenda kuvunja mawe. Moja kati ya shughuli ninazozichukia; ikianza asubuhi saa moja, ‘juu chini’ ‘juu chini’ ni mwendo wa kupinda mgongo hadi saa kumi na moja. Ukimaliza hapo, vidole havikunji, havifunguki, mgongo wauma kufu!Mwenzenu, shughuli za namna hii, zimeiharibu mikono yangu na imeota sugu kali. Ugumu unazidi kwasababu, kazi zangu zilikuwa za kushika peni na kubonyesha kompyuta. Kazi ndogo, mshahara mkubwa! Jumamosi na Jumapili, unapumzika, uko na mama watoto; kwa wenzangu na mimi wasiooa, ndio muda wa kuzunguka mara klabu hii, mara ile, unachagua; leo, Diamond anapiga wapi? Au kupoteza mawazo kwa Jide Mama Komando pale Victoria ‘Nyumbani Lounge’Maisha yangu ndiyo yalikuwa hayo. Kila Jumamosi nilikuwa niko na mke wangu, tukirivinjari jiji, lakini mara nyingi tulipenda kutulia Polisi Mesi-Oysterbay ambako tuliburudishwa na zilipendwa. Danga chee! Du kinaa! Vijana wanakwambia. Unamsikiliza Remi Ongara akilalamikia ‘kifo’
“

Siku ya kufa… siku ya kufa… siku ya kufa… wandugu kwaheri!Siku ya kufa nyama ya udongo…uzuri wote unaoza… ujana wote unakwisha, akili yote inakwenda!Nyumba nalijenga inabaki ooh! Watoto nazaa wanalia eeh! Nyumba nalijenga naoza ooh! Maiti haina rafiki eeh! Marafiki zangu watanikimbia Ooh! Tulikuwa tunakula pamoja eeh! Wanakuwa wananiogopa ooh!”Au akimsifu Mariamu wake:
“

Mariamu wangu eeh! …Waja leo, waondoka leo, mwenzenu sina pumzi, kujizuia siwezi…mwanamme barabara, kazi ya mume kwa mke…”Wataka yote… wakosa yote… wapita ukilalamika usijue la kufanya…, usijue la kufanyaa eeh…”“Niliyataka yote” ukweli mchungu huu.“Wewe vipi mbona hufanyi kazi?” Sauti kali ya nyapara inanistua toka kwenye dimbwi la mawazo. Aah! Nainua nyundo nzito na kuendelea kugonga mwamba huu bila matumaini ya kuupasua. Lakini sharti ya kazi hii; jiwe hata liwe jabari la namna gani mwishowe ni lazima limeguke na kuwa vipande vipande, la sivyo, utaambulia vipigo visivyo na idadi. Mshahara mdogo, kodi ya nyumba, ada za watoto waliozaliwa bila mpangilio. Kazi ngumu ya kushinda na wafungwa, vyote hivi vilizaa hasira, chuki na kisasi. Askari, angetafuta sababu hata isipokuwepo ya kukushushia kipigo. Mwingine leo, kakorofishwa na mkewe anayependa matumizi kupitiliza: ‘Mume wangu naomba pesa rafiki yangu ana mtoa mwanae…, mpenzi wangu nipe hela ya sare ya kitenge, Bi. Mwanaharusi wa mtaa wa Kipeta ana kitcheni pati na kanigandaa!’ Mume mi nimechoka kula dagaa! Nataka maini. Jehanam ndogo, siku zote wafungwa ndo tulilipa kadhia za maisha zilizowapata ‘wenzetu hawa wenye unifomu’Kama kuna yeyote ambaye naweza kumlaumu ama kumchukia kwa hali yangu hii basi ni Kuruthumu, mtoto wa Kizanzibari apataye miaka 18, shombe ambaye uzuri wake wa shani unaweza kumloga hata mwanamme aliyetoka kula yamini mbele ya padri au shekhe siku moja au mbili zilizopita, akajikuta akisahau mke.Kuruthumu ambaye alinifanya nimsafirishe mke wangu niliyesota naye miaka nenda rudi kwenye shida na raha, akiwa na mimba ya miezi minne na kumtelekeza kwa wazazi wake bila msaada wowote ili tu nilionje penzi lake.Kuruthumu aliyesababisha mke wangu ampoteze mtoto kwasababu ya matunzo duni. Kuruthumu aliyenitia kwenye kifungo cha miaka… jela huku nikipoteza karibu kila senti niliyowahi kuimiliki kwa kuhonga sehemu mbalimbali nikiepuke kifungo.Hapanaa! Namchukia Kuruthumu, pengine kuliko yeyote mwingine duniani; namchukia kwa mwili, akili, roho, nguvu, mawazo ya kina na kila kitu nilichokuwa nacho…Lakini simchukii hivi hivi tu, mambo aliyonifanyia, yeye na mama yake, mtego waliooniingiza, ndiyo unanifanya moyo wangu uamini kuwa duniani kuna binadamu wenye roho za kinyama na kishetani wanaompita Ziraili mtoa roho.Nakiri kuwa isingekuwa upendo wa mke wangu Jesca na roho yake ya kujali! Basi nilishafikia hatua ya kuamini kuwa wanawake wote duniani ni nyoka, swira wenye sumu kali, wanaosubiri kuuma wakati wote wayaonapo mawindo.Bali, ajabu ya dunia, mtu mmoja tu, Jesca, upendo wake uliopitiliza, kujali kwake kusiko kikomo, ndiye hasa anifanya nisiwe na imani hiyo. Aah! Jeska yule, mwanamke katika wanawake, mwanamke wa kweli kabisa!Lakini jesca nilimtenda, nimemtenda, ama nimejitenda?Hadi leo hii amekaaa ananisubiri, anasema hajaona mwanamme kama mimi, kwenye maisha yake, na ataendelea kunisubiri hata kama itachukua miaka dahari kuachiliwa gerezani, hatoenda na mwanamme mwingine.“Kichaa! Ama uwendawazimu? Ya nini kumsubiri mtu ambaye nusu ya maisha yake itaishia gerezani, na uhakika wa kutoka salama hauzidi ule wa kuozea huko,” ndivyo kila siku nakaa na kujiambia. Pia, mara zote, humwambia mke wangu mara anitembeleapo, lakini yeye hujibu:“Hapana nitakusubiri...”“Kwanini usitafute mwanamme mwingine, oana naye, tengeneza maisha, zaeni watoto, mpate familia na unisahau hayawani mimi!”“Nitakusubiri”Jeska angesisitiza kwa namna ambayo huniacha nikibubujikwa machozi moyoni. Na kadri nilivyotokwa na machozi kwa msimamo wa Jeska ndivyo nilivyozidi kumchukiaKuruthumu.Yaani, licha ya ugumu huu wa jela laiti kama leo hii ntapata msamaha wa raisin a kukutana hata kwa dakika mbili na kiumbe huyu, basi nitahakikisha nakikandamiza kishingo chake, kwa mikono hii iliyopasuka kwa suluba za jela, hadi pale povu la uhai litakapomtoka midomoni, puani na masikioni, baada ya hapo tu ndipo nitajisalimisha mbele ya sheria wanifanye watakalo, lakini kitu kimoja tu ambacho sina uwezo nacho kwa sasa ni nafasi.Sina nafasi ya kuweza kukutana tena na kiumbe huyu, tayari niko mikononi mwa sheria, miaka kadhaa ya suluba na tabu ikinisubiri mbele yangu, na kinachoniuma ni kwamba shetani huyu, wa kike anaendelea kutanua mitaani, akitumia kila senti yangu niliyoitolea jasho kwa miaka yangu yote thelathini na saba niliyopata kuishi duniani, na zaidi akinicheka na kunikebehi kwa ufala wangu wa kuingia kichwa kichwa kwenye mitego yake ya kilaghai, yeye na mama yake.

UNAIPENDA? NAMBA YANGU NI NTUMIE MESEJI giningiasilia@gmail.com ndo niko kwenye kuitunga ila naangalia mwitikio kama ina mvuto ntaitengeneza vizuri hadi mwisho na kuwaletea uhondo.
 
Back
Top Bottom