Gharama za Kitanda Muhimbili, kama Hosteli!

Gharama za Kitanda Muhimbili, kama Hosteli!

Vyamavingi

JF-Expert Member
Joined
Oct 3, 2014
Posts
5,980
Reaction score
5,797
Gazeti la Mwananchi leo limeripoti kuwa gharama za kitanda kwa mgonjwa atakayelazwa zimepanda na atalazimika kulipia kitanda kwa bei ya elfu tano kila siku.

Hii ni nje ya gharama ya mlo mmoja ambayo ni shilingi elfu mbili. Hii ina maana kuwa iwapo mgonjwa atapata huduma ya kulala na malazi, itampasa kulipa si chini ya shilingi elfu tisa kila siku. Hapo ni nje ya gharama za matibabu-vipimo, ushauri, na dawa.

Najiuliza, kupanda huko kwa gharama za matibabu MNH kutaongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa? Je, vitanda vitaongezeka na tatizo la wagonjwa kulala wawili kwenye kitanda kimoja au kulala chini litaisha?

MY TAKE
Hili ni pigo kubwa kwa sekta ya afya nchini ambayo iko kwenye hali ngumu.

Kwa maana hiyo tutegemee yafuatayo:
1. Idadi ya vifo kuongezeka badala ya kupungua maana mgonjwa kutoka Nkasi hadi afikishwe Dar lazima ndugu wabanane kwa michango ya nauli kuja Dar.

2. Wagonjwa wanaotelekezwa na ndugu Muhimbili kuongezeka, kwani mgonjwa akifikishwa Muhimbili tu, ndugu waliomleta wanaweza kumwacha ili kuepuka gharama kubwa za matibabu.

3. Kuongezeka kwa imani juu ya miti shamba na matibabu mbadala kama tunavyosikia ongezeko kubwa la matangazo ya matibabu mbadala kwenye vyombo vya habari-Tvs na redio [Dk. Ndodi na wengineo]

4. Ongezeko la waganga wa jadi na matibabu mbadala kufuatia ongezeko la wagonjwa wanaokwepa gharama za Hospitali.

5. Ongezeko la Watanzania wagonjwa kutokana na wagonjwa wengi kutopona baada ya kukosa matibabu sahihi.

6. Umri wa kuishi kwa Watanzania kupungua kwa sababu hizohizo nilizoainisha.

==================================================
Gharama za kitanda zapanda Muhimbili
muhimbili+px.jpg
mnh.jpg


Zanzibar. Dar es Salaam,

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imepandisha gharama za huduma hospitalini hapo na sasa mgonjwa atakayelazwa atalazimika kulipa Sh5,000 kwa siku.

Gharama hizo zitalipwa kwa wagonjwa wote wa rufaa, ilisema taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela na kusambazwa kwenye vyombo vya habari.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa gharama mpya zilianza kutumika Oktoba 17, mwaka huu. Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua uamuzi wa kupandisha gharama hizo.

Alipofuatwa ili kutolea ufafanuzi mabadiliko hayo, Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesh hakuwa tayari kusema lolote, huku Dk Njelekela naye akishindwa kupatikana.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven Kebwe alisema hafahamu lolote juu ya ongezeko la bei hizo. "Sifahamu kuwapo na mabadiliko ya bei za matibabu, ninachojua mimi gharama bado ziko chini," alisema Kebwe.

Muuguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema gharama hizo zinahusisha malipo ya malazi ya Sh5,000 kwa siku na chakula Sh2,000 kwa mlo mmoja, gharama ambazo anasema hazikuwapo siku za nyuma.

Awali, wagonjwa walikuwa wanalipia gharama ya matibabu tu, huduma nyingine za malazi na chakula zilitolewa bure. Mabadiliko hayo sasa yatamlazimu mgonjwa aliyepewa rufaa kulipia gharama hizo bila kujali alikotoka.

Muuguzi huyo alisema idadi ya wagonjwa imepungua wodini kutokana na wengi wao kushindwa kumudu gharama.

Alisema tangu utaratibu huo uanze, kumekuwa na tofauti kubwa na zamani kwa sababu wagonjwa ambao hawana uwezo wa kulipia kiasi hicho, hawalali hospitali hata kama hali zao zingewataka kulazwa.

"Wagonjwa wa mikoani ndiyo wanaumia sana na mabadiliko haya, mtu anatoka Ruvuma anatumia nauli kubwa halafu anakutana na gharama nyingine za matibabu," alisema muuguzi huyo na kusisitiza kuwa baadhi ya wagonjwa wanaondoka na hali zao mbaya.

Aliongeza kuwa watu wa chini wanashindwa kumudu gharama hizo, wengine wakiamua kurudi nyumbani na wagonjwa wao. Baadhi ya watu wanaouguza wagonjwa wao walikiri kuwapo kwa malipo.

"Nalipia kiasi hicho cha fedha kwa sababu sina sehemu ya kumpeleka mgonjwa wangu. Ni fedha nyingi maana haijulikani atatoka lini," alihoji Yohana Alphonce ambaye anamuuguza baba yake.

Naye Said Zuberi kutoka Muheza alisema bado hajalipia fedha ya malazi lakini tayari alipata taarifa kutoka kwa wauguzi kuwa anatakiwa kulipia gharama za malazi na chakula katika kipindi chote atakachokuwa wodini.

"Nimemleta leo mgonjwa wangu, bado sijalipia hiyo pesa, lakini nimeambiwa nitatakiwa kulipia kila siku Sh5,000 na Sh2,000 ya chakula cha hapa hospitali," alisema Zuberi.

Mabadiliko haya yamekuja wakati ikielezwa kuwa sekta ya afya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa. Hii inatokana na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kusitisha utoaji wa dawa kwa sababu ya kudai deni la Sh90 bilioni.

Chanzo:Mwananchi
 
Back
Top Bottom