Faida na hasara za mwanamke anayekunywa pombe

Hivi punde

JF-Expert Member
Apr 1, 2017
2,554
8,581
Kupombeka na aibu ya mwanamke...!


Mwili wa mwanamke huathiriwa haraka na pombe, bila shaka hilo ni jambo linalofahamika kwa wale wanywaji na baadhi ya wasio wanywaji. Mwanamke ana mwili ambao kwa kawaida ni mwepesi kuliko wa mwanaume.


Mwili wake pia una mafuta kwa asilimia kumi zaidi ya ule wa mwanaume na maji kwenye mwili wa mwanamke ni kidogo kuliko yaliyoko kkwenye mwili wa mwanaume. Kuwa na maji kidogo hufanya mwili wa mwanamke kushindwa kuzimua pombe inayoingia mwilini mwake haraka.


Naweza nikasema mwanamke ana mwili ambao una kiwango kidogo cha kimeng’enyo cha kuvunjavunja sumu ya pombe mwilini ambacho hufahamika kama alcohol dehydrogenise (ADH). Kwa hiyo, pombe hukaa kwa muda mrefu kwenye tumboni la mwanamke kabla haijabadilishwa kuwa mkojo.Hali hii ndiyo ambayo inasababisha mwanamke kulewa haraka, lakini pia kulewa kwa muda mrefu zaidi ukilinganisha na mwanaume.


Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya kihomoni mwilini mwa mwanamke, kuna ugumu kidogo kwa mtu kuweza kutabiri namna pombe inavyofanya kazi kwenye mwili wa mwanamke. Lakini wale wanawake wanaotumia dawa za kuzuia ujauzito au vidonge vya uzazi kama vinavyofahamika, huwa wanalewa haraka zaidi na pombe hukaa mwilini kwa muda mrefu zaidi.


Hata kwenye maradhi yanayosababishwa na pombe, wanawake wanaonekana kuathirika haraka zaidi. Kwa mfano, maradhi ya ini hushambulia zaidi wanawake kuliko wanaume, hata kama wote wanakunywa kiwango sawa cha pombe. Bila shaka utashangaa ni kwa nini nimeanza kwa kuzungumzia pombe, tena kwa mwanamke.


Nimeamua kuzungumzia pombe kwa wanawake kwa sababu, siku hizi idadi ya ushawishi wa kimakundi unaowahimiza wanawake kuingia kwenye ulevi umekuwa mkubwa sana. Wanawake kwa wanawake wanashawishiana sana kunywa pombe, wanaume wengi zaidi wanawashawishi wanawake kunywa na hata matangazo ya biashara yanafanya hivyo.


Kwa kuangalia matangazo ya biashara ya pombe, mwanamke hujikuta akiamini kwamba, pombe inaweza kumpa hisia tofauti, kumpa moyo wa kutenda asiyoweza kuyatenda na kumfanya aonekane ni wa kisasa zaidi. Lakini wanaume huwashawishi wanawake kunywa pombe kwa sababu, wanataka kutumia pombe hiyo kama mtego wa kuwanasa kirahisi.


Kwa nini nasema hivyo, ni kwa sababu tafiti nyingi zinazohusu madhara ya pombe kwa wanawake, zinaonesha kwamba, matukio mengi ya kubakwa kwa wanawake na kudhalilishwa kwa aina mbalimbali, yanatokea kwenye mazingira ya pombe.


Lakini sio hivyo tu, utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Duke unaonesha kwamba, wanafunzi wa kike wanapokunywa pombe, hupoteza uwezo wao wa kushika masomo na hata kuvuta kumbukumbu ya kile walichokisoma.

Lakini pia wamegundua kwamba, pombe huongeza kiwango cha uwezekano wa mwanamke kupata kansa ya titi. Hivi sasa, pombe inahesabiwa kama kitu ambacho kinaweza kusababisha kansa kama ilivyo asbestos, benzene na vitu vingine vya aina hiyo.Haja yangu siyo kumtisha mwanamke, bali kumwambia kwamba, akienda kunywa pombe, ajue kwamba, anapalilia ama kuandamwa na mambo gani.

Tafiti zinaonesha kwamba, pombe ina mchango mkubwa katika kusababisha kujamiiana kusikopangwa na ubakaji. Kwa mjini, mwanamke ambaye anakunywa pombe, akikwambia hajawahi kufanyiwa jaribio la kufanyishwa mapenzi bila hiari yake, ni lazima atakuwa ananywea nyumbani kwake tu au anakunywa na mtu ambaye wanajuana na ni wapenzi na hakuna jipya kati yao.


Lakini hata kwa wapenzi wanaofahamiana kwa kila kitu ubakaji umeelezwa kutokea miongoni mwao.Pombe hutumika kama sababu au kama njia ya kuhalalisha klitendo cha kujamiaana, ambacho hakikupangwa au hata kubakwa. Wakati mwingine ni kweli, mwanamke alionesha kukubali kushiriki tendo, lakini kilichomuongoza ni pombe na siyo utashi wake wa kiakili.


Mwanamke akishakunywa kiasi fulani cha pombe, anakosa uwezo wa kujua au kuona dalili za kufanyiwa unyama kutoka kwa mwanaume. Kuna wakati uwezo wa kukataa iwe kimwili au kisaikolojia unakuwa umepotea.Pombe huharibu uwezo wa kuamua na kuhukumu kwa mnywaji kuhusiana na tendo la ndoa.

Hivyo watu wanapokwenda kunywa kukiwa na wazo dogo tu la kuhusu kujamiiana, wazo hilo hukuzwa sana na wanywaji baada ya kuaza kulewa. Hapo ndipo ambapo vurugu na udhalilishaji hutokea. Wanawake wanaokunywa pombe wanajua wanavyoamka asubuhi wakiwa na aibu na hali ya kuhisi dhaliliko kwa vitendo vilivyotokea usiku wakati wa kunywa.



Wale wanaokunywa kwa kupewa ‘ofa’ na jirani au rafiki wa kiume au wanaume wanaotaka kujenga nao urafiki, wengi huja kujutia jambo hilo.


Takwimu zinaonesha kwamba nusu ya wanawake wote wanaoambukizwa maradhi ya zinaa, huambukizwa maradhi hayo wakati wakiwa wamekunywa, ambapo uwezo wao wa kujikinga huwa chini sana.
 
Back
Top Bottom