ELIMU DUNI NA OMBWE LA FIKRA

sammosses

JF-Expert Member
Jan 24, 2011
1,685
1,111
Shule ni kituo cha kuongeza maarifa na kufuta ujinga,kwa kutumia shule jamii husika ustaarabika na kujijengea misingi mizuri ya uelewa japo kuwa kuna jamii zingine ambazo hazijaelimika lakini zina weredi wa kutosha kutokana na akili yao ya kuzaliwa katika kuendesha shughuli zao za kila siku.

Tunapopima elimu yetu lazima tupime na weredi wa wasomi wetu,ikiwa weredi wa wasomi wetu unatengeneza ombwe la fikra yakinifu lazima tuhoji vituo vyetu vinavyotumika kutoa elimu hiyo. Hii ni kutokana na kuwa elimu bora hutoa wasomi na wanazuoni bora wenye maslahi mapana katika kulisaidia taifa na watu wake.

Nchi yetu ipo kwenye janga kubwa la kitaifa kwa wanazuoni na wasomi wetu kushindwa kusimamia fikra yakinifu zitakazojenga taifa kwa misingi mipana ya weredi wa kutosha ili kuleta ufanisi wenye tija katika kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu. Taifa kama hili lenye kuzalisha wasomi wachumia tumbo matokeo yake ni kuzalisha taifa la watu masikini wenye fikra tegemezi zinazojengwa na dhana nzima ya uvivu wa kutumia taaluma yetu na uvivu wa kufikiri pia.

Haingii akilini pamoja na rasilimali tulizonazo na wasomi wanaohitimu elimu ya juu kila mwaka lakini nchi yetu bado ni masikini wa kutupwa. Lazima tuhoji ubora wa elimu yetu ulioshindwa kufufua fikra yakinifu zitakazo kuwa chachu ya maendeleo ya nchi na watu wake. Kwa mantiki hiyo vyuo vyetu kiuhalisia vinazalisha wasomi wenye fikra za kuajiriwa zaidi na wenye uwezo wa kusomea mitihani zaidi kuliko kuibua mbinu endelevu za kufufa uchumi wetu,hali inayosababisha taifa kukubali kutengeneza tabaka ndogo lenye kushikilia akili za walio wengi.

Matokeo ya elimu isiyo na tija ni zalisho la jamii iliyogubikwa na uoga wa kutosha ambao unaojali angalau mlo mmoja hata kama uwezekano wa milo mitatu upo. Ndo maana leo hii unaweza kusikia msomi akatoa tamko ambalo haliendani na ubora wa elimu yake na tamko hilo likazua sokomoko kwenye jamii husika.

Tumeona makongamano makubwa yaliyoendeshwa na wanazuoni mbalimbali juu ya mustakabali wa nchi yetu,lakini mwisho wa siku tumeambulia nini zaidi ya kulalamika ikiwa na wanazuoni hao wamegeuka sehemu ya kutetea uchafu na matendo maovu yenye mwendelezo wa kubaka demokrasia yetu.

Ni lini basi elimu yetu itakuwa ndiyo suluhisho la matatizo yetu ikiwa wanazuoni wameacha kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora na kujikita kusimamia batili inayojengwa kwa maslahi ya kikundi cha watu wachache waliotanguliza maslahi tumbo mbele.

Wanazuoni hao ama kwa makusudi au kwa kutanguliza ubinafsi mbele wamejaribu hata kutoa matamko ya kuupotosha umma,mathalani mgogoro wa uchaguzi huko Zanzibar ambako halali inapokwa kwa makusudi na tafsiri ya sheria kupotoshwa kwa makusudi kwa lengo la kukibeba kikundi fulani.

Nani asiyeyajua maswahibu yaliyoukumba upande mmoja wa Muungano kwa mwenyekiti wa tume kufuta uchaguzi kwa kuwa tu ameamua kuidhoofisha elimu yake na kutanguliza maslahi ya kundi fulani ambalo kwa kutumia kundi hilo naye ananufaika bila kujali umma mzima unaathirikaje na maamuzi hayo.

Ajabu hata kampeni meneja wa rais wa muungano naye anadondokea kwenye mtego huo huo kwa kuhalalisha batili hiyo inayokinzana na sheria ya uchaguzi. Kwanini wasomi wetu wanakuwa sehemu ya kupotosha jamii ilihali ukweli unajulikana.
Unapozungumzia uhalali wa kisheria weka na vipengele vyake kuliko ku generalize mambo kwa kufunika kombe mwanaharamu apite.

Haiwezekani mwenyekiti wa jumuiya nyeti ndani ya chama,jumuiya ya wazazi kuwa sehemu ya uwakilishi mbaya wa wazazi wa chama hicho kushabikia batili na kupotosha umma mamlaka halali ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar ilihali katiba inasomeka vizuri na inaeleweka vizuri.

Linapokuja suala la maamuzi yaliyofanywa na mwenyekiti huyo bwana Jecha kutamkwa na kutetewa kuwa ni halali hatuna shaka na hilo. Lakini shaka yetu inajengwa na mamlaka ipi aliyoitumia kutoa tamko hilo ambalo liko wazi kisheria. Huwezi kutuambia tu mwenyekiti ana mamlaka ya kisheria kufanya maamuzi ambayo hayawezi kuhojiwa na mtu yeyote au chombo chochote bila kututajia kipengele cha sheria kinacho mruhusu mwenyekiti huyo.

Mbaya zaidi mzee huyo toka kundi la wazazi anadiriki kumshambulia mwanazuoni aliyekataa utumwa wa kuidhoofisha elimu yake kusemea kile kilichotamkwa kisheria juu ya mamlaka na uwezo wa tume na mwenyekiti wake. Kwangu namuona mwenyekiti huyo wa wazazi ni mtumwa anayepambana na giza ilihali nuru imekwisha tanda.Lakini pia hongera kwa mwanataaluma huyo wa sheria bi Aisha Aman Karume kutumia haki yake ya kikatiba ya kutoa mawazo yake na kuieleza jamii husika juu ya uhuni huo unalazimishwa mbele ya wananchi walio erevuka. Lakini kumshambulia kuwa yeye ni mtoto wa aliyekuwa rais hakumpi haki ya kutoa mawazo yake na anayatoa kama nani ni kutokumtendea haki na kuvunja katiba ya JMT inayotoa haki hiyo.

Kwa mantiki hiyo basi utaona ni jinsi gani elimu yetu inayoshindwa kuwaandaa wasomi wazalendo wenye kuweza kusimamia maslahi ya taifa kwa kuitumia elimu waliyoipata kwa faida yao na faida ya wengine kwa maslahi ya umma. Tukiweza kujikomboa kwenye hili hakika nyeupe itabaki kuwa nyeupe na nyeusi kuwa nyeusi bila kigugumizi.

Tuna changamoto kama taifa ili kujenga nchi yenye heshima na yenye kudumisha ustawi wa maisha ya wananchi na mustakabali wa amani isiyotiliwa shaka pande zote kwa wasomi wetu kuwa chagizo la kudumisha ukweli na kutopotosha umma kwa kutumia udhaifu wa wengi waliyoikosa hiyo elimu.

Suluhisho kwa elimu yenye tija ni kwa taasisi zetu kuboresha mazingira rafiki ya elimu yenye kuzalisha uzalendo wa kweli na kuondoa dhana tegemezi kwa kuwaandaa vijana kujiajiri zaidi na kupata mafunzo yenye maarifa kuliko maarifa ya kujibia mitihani. Tukilifanya hili kwa dhati ya mioyo yetu tutafika mbali kama taifa na kuwa mfano wa kuigwa kwa majirani zetu.
 
Back
Top Bottom