EALA: Tusilalamike, tulikosea, tujisahihishe

Mbase1970

JF-Expert Member
Jun 11, 2015
6,054
4,601
Wahenga hunena "Kutenda kosa sio kosa ila kurudia kosa ndio kosa".
Inawezekana watanzania tuliowengi tuna tatizo la kuwahi kusahau. Nimekuwa nikisoma hoja na malalamiko mbalimbali kutokana na uchaguzi wa marudio uliofanyika Bungeni jana kuwapata wawakilishi wa Chadema kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

Kuelewa zaidi wapi tulikosea na vipi tunapaswa kujisahihisha ili tusilalamike tena huko mbeleni nimeambatanisha andiko hili na Muongozo wa Ibara ya 50(1) ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (The EAC Treaty) na dondoo za Kanuni za Bunge la Jamuhuri ya Muungano kuhusu namna ya kuwapata wawakilishi wa nchi kwenye Bunge la Jumuiya (EALA) kama zilivyotolewa na Katibu wa Bunge na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Maelezo ya ibara ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanashabihiana sawia na kanuni za Bunge kuhusu wapi tunawapata wawakilishi wa Nchi (na sio wa vyama vya siasa pekee) watakaotuwakilisha ndani ya Bunge la Jumuiya (EALA). Tulikosea wapi?

Tulikosea kama tulivyokosea kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMLK). Makosa tuliyoyafanya kwenye BMLK yalitufikisha tulipoishia kwa kuikosa Katiba Mpya na hatukujifunza kutokana na makosa hayo tumeyarudia tena kwenye uchaguzi wa EALA tangu duru ya kwanza na hata hii duru ya marudio. Mchakato wa kupata wawakilishi wetu EALA umekamilika lakini tukubali kuwa uligubikwa na mapungufu mengi ambayo sasa ndio ndio wakati muafaka wa kujisahihisha kwa kuyatafutia ufumbuzi ili huko tuendako tusirudie makosa.

Wanasiasa wanatuangusha. Walituangusha kwenye Katiba Mpya na wametuangusha tena kwenye uchaguzi wa EALA. Tusilalamike, tulikosea, tujisahihishe.
Kwa waliosahau tujikumbushe.....

Wakati inatungwa sheria ya kuandika katiba mpya, wanasiasa ambao kwa hulka ni wabinafsi na wenye kuegemea maslahi binafsi au maslahi ya makundi (vyama vyao) huku wakiyaacha kando maslahi mapana ya Nchi na wakiwa ndio watunga sheria waliamua kuwa Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watokane na makundi matatu;

1. Wabunge wote wa Bunge la JMT
2. Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi
3. Kundi la 201

Baadhi yetu tulihoji na kutilia mashaka muundo huu wa aina ya wajumbe watakaobeba jukumu la mwisho la kuandika Katiba Mpya baada ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi
kuhitimisha jukumu lake kwa sababu tulikuwa na wasiwasi na wanasiasa kuwa huwenda kwa ile hulka yao ya kutanguliza maslahi binafsi na maslahi ya makundi (vyama vyao) badala ya maslahi mapana ya Nchi jambo jema la kupata Katiba inayokidhi matakwa ya wananchi linaweza kukwama. Hofu yetu ilikuwa sahihi Katiba Mpya ilikosekana na Taifa tumeingia hasara ya kuendesha mchakato wa mabilioni ya shilingi ambao mwishoe ulifeli. Siasa zilichangia kutuangusha na kututia hasara.

Wenzetu Kenya walipokuwa wanaandika Katiba yao mpya walifungua milango kwa wajumbe wanaotokana na uwiano wa uwakilishi wa makundijamii yote (wanasiasa ikiwa ni sehemu ya hayo makundi) ili kuupa mchakato wao sura ya uwakilishi wa kitaifa ambao utazingatia zaidi maslahi mapana ya Taifa lao.

Hawakuishia hapo sheria yao pia ikasema wazi kila atakayepata nafasi ya kushiriki kwa Bunge la Kuandika Katiba Mpya basi HATARUHUSIWA kuwania nafasi yoyote ya kuchaguliwa kisiasa kwa kipindi kisichopungua miaka mitano tangu itakapoanza kutumika Katiba mpya. Hii ilisaidia kuondoa mgongano wa kimaslahi (conflict of interests) miongoni mwa wajumbe wakati wa kuandika Katiba.

Mivutano ilikuwa mikali sana kule House of Bomas kiasi cha Bunge lile kutaka kuvunjika lakini mivutano hiyo ilikuwa ni kwa maslahi mapana ya nchi yao na sio ya wajumbe binafsi au makundi (vyama ama makabila) yao. Mwishoe waliafikiana na wakatoka House of Bomas wakiwa wamepata Katiba Mpya.

Sisi hapa kwetu tulikosea hatukuzingatia uwiano wa uwakilishi sawa wa makundijamii kwenye BMLK. Tulijaza utitiri wa wajumbe wengi wanasiasa (wabunge wote wa JMT, Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi na hata wale walioitwa kundi la 201 nao wengi wao waliteuliwa kulingana na itikadi zao za kisiasa).

Bahati mbaya sheria yetu haikuwadhibiti kama ilivyofanywa Kenya, matokeo yake wanasiasa wetu wakadhihirisha rangi zao (maslahi binafsi na ya vyama vyao) kwanza na maslahi ya Taifa (Maoni ya Wananchi) yakatupwa kando.

Wanasiasa wakahodhi mchakato wote wa Katiba wakaacha kujadili hoja wakaanza vioja, mipasho, matusi, lugha za kejeli, visa na mikasa wakatunishiana misuli na hatimaye wengine walipoona hawana ubavu tena wakatimka na kususia BMLK waliobaki wakaendelea na kugegedua maoni ya wananchi mwishoe TUMETOKA PATUPU tukakosa Katiba Mpya na hasara juu.

Haya ndio madhara ya SIASA na Wanasiasa kuteka na kuhodhi masuala ya msingi yenye kuhitaji maamuzi yanayozingatia maslahi ya Taifa.

Uchaguzi wa EALA umekamilika na Tanzania tayari imepata wajumbe wake Tisa watakaoiwakilisha kwenye Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Wengi wamebaki wanalalamika wanaona wawakilishi wetu waliochaguliwa hawana sifa kidhi za kutuwakilisha, wengine wanalalamika kuwa mchakato wa demokrasia ya kura bungeni unawanyima nafasi wenye sifa na kuchagua wagombea dhaifu, wengine wanalalamika vyama vinateua wagombea dhaifu kwa upendeleo, rushwa na kujuana, wapo wanaolalamika kwamba uwingi wa uwakilishi bungeni unatumika vibaya kwa siasa za kukomoana. Ilimradi kila MTU amelalamika kivyake na kwa hoja zake.

Kwa nini wanasiasa wanapenda kuingiza SIASA kwenye masuala yenye maslahi mapana ya kitaifa? Wanatuangusha. Inawezekana wao hawayaoni hayo kwa kuwa ndio wako mchezoni ila kwa sisi tulionje kama watazamaji ndio tunayaona vema mapungufu yao. Watusikilize. Wanatuangusha.

Ibara ya 50(1) ya Mkataba wa Jumuiya (The EAC Treaty) ikisomwa pamoja na Kanuni za Bunge la JMT kama zilivyotajwa na Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashilillah katika gazeti la Serikali zinaeleza waziwazi kuwa wajumbe wa EALA kutoka nchi wanachama wachaguliwe na Bunge la nchi mwanachama sio kutoka miongoni mwa wajumbe wake bali kwa kadiri itakavyowezekana watokane na:-

1. Vyama vya SIASA vyenye uwakilishi bungeni.
2. Makundi yenye maoni.
3. Jinsia.
4. Makundi yenye maslahi maalumu.

Bahati mbaya matakwa ya ibara hii na kanuni za Bunge hayakuzingatiwa na hapa ndio binafsi naona ilikuwa chanzo cha kusababisha malalamiko yote tunayoyasikia wengine wakienda mbali zaidi hata kukata tamaa na hali hii.

Wanasiasa kama kawaida yao na kwa kutumia mamlaka waliyonayo wameuteka mchakato wote na kuzifanya nafasi hizi za uwakilishi kwenye EALA badala ya kuwaniwa na makundi yote manne yaliyotajwa kwenye ibara ya Mkataba na Kanuni za Bunge zimegeuzwa ni ya haki kuwaniwa na kundi moja tu la Wanasiasa (i.e vyama vyenye uwakilishi bungeni).

Wanasiasa wanajiwakilisha wenyewe, wanawawakilisha makundi yenye maoni, wanawawakilisha makundi ya jinsia, wanawawakilisha makundi yenye maslahi maalumu. Kiufupi Wanasiasa wameuteka mchakato na kuuhodhi.

Madhara ya kuteka na kuhodhi huku ndio maana wanapofikia wakati wa kuchagua watu makini, wenye ufahamu ambao watakidhi sifa zakutuwakilisha na kutetea maslahi ya nchi wao huingiza SIASA, hutanguliza maslahi binafsi kwa kuteua wagombea dhaifu na wasio na sifa kidhi kwa kuwa wanajuana au kulipana fadhila na wanapofika kwenye maamuzi ya kura hugawanyika, huacha maslahi ya Taifa na kukumbatia maslahi ya vyama vyao na kupiga kura kwa misingi ya vyama, chuki, visasi, kukomoana na mwishoe kuchagua watu dhaifu na wananchi kubaki wanalalamika. Wanasiasa wanatuangusha.

Mytake: Tusilalamike, tulikosea, tujisahihishe. Kwa sasa uchaguzi umekwisha tumepata wawakilishi wetu tuwaunge mkono wanatuwakilisha kama Nchi.

Bunge linapaswa kuboresha kanuni zake ili matakwa ya Mkataba wa Jumuiya yaheshimiwe na yazingatiwe. Wanasiasa waache hulka ya kuteka na kuhodhi kila kitu.
Naomba kuwasilisha.

Na Saidi Msonga
Mchambuzi wa masuala ya Siasa na Jamii


 
Back
Top Bottom