DENIS PHOMBEAH KWA UFUPI
WanaMajlis,
Kuna mwenzetu mmoja kaniletea ujumbe huo hapo chini anataka
nimpe historia ya
Denis Phombeah:
smarte_r said:
mzee wangu mohamed said itakuwa vyema kama utamuelezea kiundani huyo mnyasa hapa jf.
binafsi nataka sana kumfahamu vizuri na kufahamu uhusika wake katika harakati za kisiasa ndani ya tanganyika.
niwie radhi kwa ombi langu maana siku hizi nimekuwa sivutiwi kusoma magazeti ya hapa nyumbani hususani gazeti la raia mwema.
Jibu langu hilo hapo chini:
Smarte,
Sina taarifa nyingi kuhusu
Denis Phombeah.
Phombeah kwa mara ya kwanza nimemsoma katika kitabu, ''The Making of Tanganyika,''
Chato and Windus, London 1965.
Kitabu hiki kiliandikwa na
Judith Listowel na alipokuja Tanganyika kufanya utafiti wake mwenyeji wake alikuwa
Ally Sykes kupitia kwa Peter Colmore, Nairobi.
Kitabu hiki ndicho pekee katika vitabu vilivyoandikwa kuhusu historia ya TANU na harakati za kudai uhuru ambacho kimekaribia sana kusema kweli.
Ndani ya kitabu hiki Listowel anahadithia uchaguzi wa mwaka 1953 Ukumbi wa Arnautoglo kati ya
Abdul Sykes na
Julius Nyerere kuwania urais wa TAA.
Kuna kisa cha kueleza vipi
Nyerere aliingizwa katika uongozi wa TAA kushindana na
Abdul Sykes mwenyeji wake.
Kisa hiki nishakieleza hapa Majlis mara kadhaa naanimi unakijua.
Sasa kwa kuwa
Denis Phombeah hakuwa anajua mipango iliyopangwa baina ya
Abdul, Hamza Mwapachu na
Ali Mwinyi Tambwe, yeye akitaka sana Nyerere ashinde uchaguzi ule akawa anawapitia wapiga kura kuwashawishi wamchague
Nyerere.
Katika uchaguzi ule Nyerere alimshinda
Abdul Sykes kwa shida sana kwa hiyo akawa Rais wa TAA.
Uongozi wa TAA 1953 kuelekea kuundwa kwa TANU 1954 ulikuwa kama hivi:
Viongozi hawa ni:
J.K. Nyerere, President;
Abdulwahid Sykes, Vice-President:
J.P. Kasella Bantu, General Secretary;
Alexander M. Tobias and
Waziri Dossa Aziz, Joint Minuting Secretary;
John Rupia, Treasurer na
Ally K. Sykes - Assistant Treasurer. Committee members
Dr. Michael Lugazia, Hamisi Diwani, Tewa Said, Denis Phombeah, Z. James, Dome Okochi, C. Ongalo na Patrick Aoko.
Huyu
Phombeah alikuwa mmoja kati ya vijana wa Dar es Salaam wa wakati ule ambao walikuwa katika siasa za TAA ingawa yeye alikuwa anatokea Nyasaland.
Kadi ya TANU ya
Denis Phombeah ni no. 5.
Baada ya kifo cha
Chihota kutoka Rhodesia ambae alikuwa meneja wa Arnautoglo Hall nafasi ile ikashikwa na Phombeah Mnyasa.
Chihota alifariki Uingereza mwanzoni mwa miaka ya 1950.
Phombeah rafiki yake mkubwa alikuwa
Oscar Kambona.
Baada ya
Oscar Kambona kwenda uhamishoni Uingereza mwaka wa 1967
Phombeah na yeye akamfuata huko.