Demokrasia ni chachu ya maendeleo

sammosses

JF-Expert Member
Jan 24, 2011
1,685
1,111
Wakati ni ukuta, ukishindana nao utaumia. Huu ndiyo wakati wenyewe muafaka wa kulijenga taifa letu imara katika kusimamia demokrasia na misingi ya utawala bora. Tukiweza kusimamia utawala wa sheria na kuheshimu demokrasia tutaweza kutimiza ndoto za kufikia uchumi wakati.

Tunapo zungumzia uchumi wa kati,si jambo la mchezo. Ni safari yenye matumaini kwa wananchi ikiwa misingi ya demokrasia itasimamiwa kwa haki pasi ya ubaguzi. Ubaguzi ni zaidi ya ukaburu, yapaswa kuogopwa kama ukoma. Tukianza kuwabagua wengine kwa itikadi za kisiasa mwisho wa siku tutabaguana miongoni mwetu hata kama ni waumini wa itikadi moja.

Ni ukweli taifa linapitia kipindi kigumu sana cha mpito kuelekea uchumi wa kati,ni ukweli pia kuelekea huko taifa linapaswa kujirekebisha kutoka kufanya kazi kwa mazoea na kufanya kazi zenye ufanisi kwa faida ya nchi na wananchi wake, lakini pia kuna ulazima wa serikali kusimama imara kusimamia ufanisi wa watendaji wake(close monitoring) kwa kufuata sheria za kazi bila idara husika kumuonea mtu, lakini haya yote yasipozingatia weredi katika kufuata mwongozo (katiba) tuliyojiwekea tukitegemea akili zetu binafsi tutaliingiza taifa katika mitafaruku isiyo na tija kwa taifa tukitegemea vyombo vyetu vya dola kuwalinda watawala kusimamia matakwa binafsi yanayopingwa na umma,hatimaye ndoto za kufikia uchumi huo kuwa hekaya.

Kuna ombwe kubwa la uongozi katika taifa letu, hali inayopelekea kila jambo kugeuzwa siasa hata kwa mambo yanayotaka utaalamu, matokeo ya kadhia hii ni mwingiliano wa madaraka unaozalisha umungu mtu ndani ya taifa hili. Mgawanyo wa madaraka umepoteza dira,taasisi za umma zinafanya kazi kwa uoga na kuviziana kwa kuwa taasisi kubwa kuliko zote imetengeneza utamaduni huo.

Hii ni sawa na mgomo baridi kwa watumishi wa umma kujazana maofisini lakini utendaji wao hauna ufanisi, ubunifu wa watendaji umepotea na kuachiwa mtu mmoja kuwa mbunifu wa kila kitu, hali inayomfanya hata rais kutamani kuwa IGP.

Tumejiandaaje kufikia malengo ya safari yetu? Lengo kufikia uchumi wa kati ni jema kabisa lakini mazingira yetu ni rafiki kufikia taifa kuwa la viwanda. Serikali ya viwanda haiwezi kutimiza unabii wake iwapo itashindwa kusimamia mapinduzi ya kilimo chenye tija,matumizi na uhakika wa maji ya kutosha na umeme wa kutosha wenye uhakika.

Serikali ilikwisha agiza mikoa yote kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya viwanda(EPZ) ,lengo ni kufikia safari ya uchumi wa kati. Pamoja na lengo hilo zuri sijaona uhakika katika suala zima la maji, ukizingatia kuna uhaba mkubwa wa miundo mbinu ya maji inayopelekea watu wèngi kukosa màji safi na sàlama kwa màtumizi ya kawaida.

Kilimo pamoja na kutengenezewa kauli mbiu kila awamu ya uongozi wa serikali, bado taifa limendelea kuwa muumini wa mvua za kudra ilihali nchi imezungukwa na vyanzo vya maji lakini hauonekani mkakati madhubuti wa serikali zaidi ya kutubadilishia mawaziri wenye dhamana.

Kwa mtazamo huu, tunategemea aina gani ya viwanda tuvitakavyo ikiwa changamoto nyingi zaidi ya mkakati wenyewe, kama lengo ni viwanda vya assembling sawa, vinginevyo tujikite kutengeneza viwanda vya majiko na vibatari.

Tuache kuwaaminisha wananchi kwa mbwembwe na kauli mbiu wakati uwezo wetu wa kuzikabili changamoto zinazotukabili ni mdogo, tuna tumiaje urafiki wetu na nchi kama China ikiwa tunashindwa kujifunza toka kwao. Kufikia walipo leo hawakufanya maigizo ndiyo maana Sera yao viwanda imeweza kuiletea nchi hiyo m maendeleo chanya.
 
Back
Top Bottom