DC Tunduru atoa matumaini kwa wananchi wake

kanywaino

Senior Member
Sep 10, 2010
171
19
DC TUNDURU ATOA MATUMAINI KWA WANANCHI WAKE

DSC_0431.JPG


Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera akizungumza na wananchi wa kijiji cha Msinji kata ya Ligoma, Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.​


DSC_0424.JPG


Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera akipokea risala toka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Msinji.​


DSC_0425.JPG


Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Tunduru Ndg. Abdallah Issa Mussa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Msinji,Kata ya Ligoma.




Mkuu wa wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Zuberi Homera akiambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, wamefanya Mkutano katika Kijiji cha Msinji, Kata ya Ligoma Tarafa ya Namasakata.

Mkutano huo ulifanyika katika Shule ya Msingi Msinji, lakini kabla ya Mkutano huo Mhe. Mkuu wa wilaya alienda kukagua miradi ya kijiji na kujionea hali halisi ya maisha ya wananchi, alipita katika kisima kinachotumiwa na wanakijiji kuchota maji pamoja na kukagua nyumba ya mwalimu ambayo bado haijakamilika na madawati yanayomaliziwa kutengenezwa kwa ajili ya kumaliza uhaba wa madawati.

Kijiji cha Msinji kinapatikana kilomita 34 toka makao makuu ya wilaya ya Tunduru, kina jumla ya wakazi 2,130, huku zao kuu la kibiashara likiwa ni Korosho pia wanakijiji wanalima mihogo, mpunga na mbaazi.

Changamoto kubwa inayokikabili kijiji cha Msinji ni Wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima, barabara kutopitika kipindi cha masika, wananchi hawapati maji safi na salama na zahanati ya kijiji haina umeme.

Akizungumza na wananchi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndg. Abdallah Issa Mussa, aliagiza Mkandarasi wa Wilaya kuangalia jinsi ya kukarabati barabara haraka iwezekanavyo ya kutoka Ligoma makao makuu ya kata hadi kijiji cha Msinji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Juma Homera akizungumzia tatizo la hifadhi ya msitu iliyopo kitongoji cha “Ndio kwa maana”, Mhe. Homera aliagiza iundwe kamati ya ardhi na misitu ili kuangalia tatizo hilo na ndani ya siku 7 waje na mapendekezo ili awezekuchukua hatua.

Akizungumzia swala la maji, alikiri tatizo la uhaba wa maji ni mkubwa sana katika Wilaya yake lakini tatizo kubwa lipo kwa kaimu Injinia wa maji wa wilaya, amekuwa mtu mzito sana kufuatilia miradi ya maji wilayani humo, alisema “Injinia wa wilaya tunampa nafasi ya mwisho, akishindwa kuendana na kasi yetu tutamuambia atupishe, namuagiza haraka aandike ripoti ya maji wilaya nzima pia na namtaka atoe taarifa ya mapato na matumizi ya miradi ya maji”.

Kuhusu tatizo la umeme Mhe. Homera alimuagiza Meneja wa Tanesco wilaya kuhakikisha vijiji vyote ambavyo havina umeme vinapata umeme katika awamu hii ya tatu ya REA ikiwemo tarafa ya Namasakata na vijiji vyake, huku akiwataka wananchi waandae elfu ishirini na saba (27,000) kwa ajili ya kuunganishiwa umeme majumbani mwao.

Mkuu wa Wilaya aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Msinji kwa kuchangia madawati zaidi ya 170 na alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ahakikishe nyumba ya mwalimu inakamilika haraka iwezekanavyo.

Akijibu suala la afya, Mhe. Juma homera aliwaomba wananchi waweze kuchangia bima ya afya ya Community Health Fund (CHF) ili waweze kupata huduma ya dawa katika Zahanati ya kijiji, na alimuagiza Mganga wa zahanati hiyo ahakikishe umeme wa jua (Sola) unafungwa ndani ya wiki moja na kitengenezwe chumba cha kupumzika wagonjwa, ambapo wanakijiji wafyatue tofali na serikali italeta vitu vya viwandani, kama bati, saruji na rangi.

Aidha, alisisitiza sana Vijana na akina mama wajiunge kwenye makundi ya wajasiriamali ili waweze kupata asilimia 5 ya mapato ya halmashauri ya wilaya.

Alimalizia kwa kusisitiza wanafunzi wote waende shule, mzazi yeyote atakaye kamatwa kwa kosa la kutompeleka mwanae shule sheria itachukua mkondo wake, huku akiwachia wananchi namba yake ya simu ya mkononi.

DSC_0423.JPG


DSC_0416.JPG


DSC_0412.JPG


DSC_0406.JPG


DSC_0407.JPG


DSC_0410.JPG
 
Safi sana wajue wananchi wao wanaishije na kutatua matatizo kwa urahisi.
 
Back
Top Bottom